TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za
Rambirambi Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Peter Kayanza Pinda, kufuatia kifo
cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mheshimiwa
Celine Ompeshi Kombani.
“Pokea
rambirambi zangu za dhati, sote kwa pamoja tumepoteza mama mchapakazi, hodari
na aliyependa kushirikiana na wenzake katika kazi zake, hakika tutamkumbuka
siku zote” Rais Amesema.
Rais
Pia amemtumia salamu za pole mume wa marehemu Kombani, Bwana Swaleh Ahmad
Pongolani, watoto, ndugu na jamaa wa
Mama Kombani.
“Nimepokea
taarifa za kifo cha mama Kombani kwa huzuni kubwa, najua machungu na maumivu
mliyonayo kwa kuondokewa na kiungo muhimu katika familia yenu, poleni sana, mama
ni nguzo ya familia, niko nanyi katika msiba huu mzito kwenu”
Rais ametuma salamu hizo kwa Mume wa Marehemu Celine, Bwana Pongolani, watoto,
wajukuu na ndugu wa Marehemu mama Kombani.
Rais
amesema pamoja na kwamba kifo hakiepukiki, bado ni kitu ambacho kinashtua, kuhuzunisha
na kuleta unyonge mkubwa kwa wafiwa katika jamii.
Marehemu
Kombani pia alikua ni mgombea ubunge wa jimbo la Ulanga Mashariki kwa tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi, ambapo amekwisha kulitumikia jimbo hilo kwa kipindi cha
miaka 10 iliyopita.
“Naungana
nanyi katika kipindi hiki kigumu kumuombea Mama Kombani ili mwenyezi Mungu ampe
mapumziko mema ya Milele” Rais amesema na
kuwaombea wana familia na ndugu wa Marehemu “Mwenyezi Mungu awatie nguvu,
awape uvumilivu na subira katika kipindi hiki”.
“Niko
nanyi katika kipindi hiki kigumu kwa hali na mali, nawaomba msijisikie wapweke”
Rais amesema na kuwatakia utulivu na amani katika kipindi hiki cha msiba mkubwa
kwa familia ya mama Kombani
Marehemu
Mama Kombani amefariki jana tarehe 24 Septemba, 2015 nchini India ambapo alikua
anapatiwa matibabu baada ya kugundulika kuwa na kansa.
Marehemu
Kombani alizaliwa Juni 19, 1959 ameacha Mume, watoto watano na wajukuu wane.
Mwili
wa marehemu unatarajia kuwasili nchini kesho mchana na anatarajiwa kuzikwa
Mkoani Morogoro katika shamba lake.
Mungu
ailaze Roho ya Marehemu Celine Kombani mahali Pema Peponi, Amina.
Imetolewa na:
Premi
Kibanga,
Mwandishi
wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu-DSM.
25
Septemba, 2015
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...