Baadhi ya Watanzania walioko Hijja na ambao wamenusurika na maafa ya msongamano wa watu huko Mina jana. Kulia nia Bw. Yahaya Sameja, kushoto ni mwigizaji mchekeshaji Bw. Amri Athumani al maarufu kama King Majuto. Wa katikati  jina lake halikuweza kupatikana.
------------------------------------------------------------------------------------

Bismilah Rahman Raheem
Assalaam alaykum warahmatullahi wa barakaatuhu.

Taarifa hii inahusu tukio lilitokea jana Mina Saudi Arabia wakati mahujaji wakielekea kwenye Jamaraat , palitokea msongamano mkubwa ( stampede) na kupelekea mahujaji zaidi ya 700 kufariki na mamia kadhaa kujeruhiwa.

Tayari tumethibitisha kutokea vifo vya watu watano waliotokea Tanzania miongoni mwao mmoja ni raia wa Kenya na wengine  wanne ni Watanzania.
Watanzania waliotambuliwa hadi jana usiku wametajwa kuwa ni Bi Mwanaisha Hassan Juma, Mkungwe Suleiman Hemedi na Sefu Saidi Kitimla.
Mwanamke mwingine mmoja Mtanzania jina halijaweza kupatikana hadi Alhamisi usiku wakati tukiandaa taarifa hii.

Raia wa Kenya ametambuliwa kwa jina la Bi Fatuma Mohammed Jama.
Kuna taarifa ya mahujaji wanawake wawili ambao hadi Alhamisi usiku walikua hawajapatikana hivyo hatukua na uhakika juu ya usalama wao hadi tutakapowaona ama kupata taarifa zao. Ifahamike kuwa majina yamepatikana kupitia vitambulisho vyao ambavyo wahanga wa tukio hili waliweza kuvichukua kutoka kwenye miili ya marehemu.

Nimepokea taarifa za majeruhi miongoni mwa mahujaji wetu wa Tanzania na baadhi ya majeruhi hao nimeonana nao mara baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Vilevile nimeagiza maafisa wetu wa Bakwata nilionao hapa Mina kuendelea kufuatilia habari na taarifa za mahujaji wetu katika hospitali na sehemu za kuhifadhia maiti. Nimefanya hivyo ili niweze kuwa na uhakika juu ya usalama wa mahujaji wetu.

Katika kipindi hiki cha taharuki kubwa tunafanya mawasiliano na wizara husika hapa Saudi Arabia kwa kushirikiana na serikali yetu kupitia ubalozi wetu hapa Saudi Arabia. Natambua uwepo wa mkanganyiko wa taarifa ambazo zinazidisha taharuki kwa ndugu na jamaa wa mahujaji wetu. Nachukua fursa hii kuwaomba ndugu na jamaa wa mahujaji kuwa watulivu na kuwa na subra katika wakati huu mgumu sana kwetu sote.
Tunaendelea kufuatilia kwa karibu sana na Insha Allah mara tu tukipata taarifa za uhakika basi tutawafahamisha.

Kutokana na idadi ya maiti kuwa kubwa serikali ya Saudi Arabia wanaendelea na zoezi la kutambua uraia wa kila mwili ili waweze kutoa taarifa tunatarajia wakati wowote tutakuwa tumepata taarifa zaidi.

Wabillahi Tawfiiq.


Sheikh Abu Bakari Zuberi
Mufti wa Tanzania.
MECCA, Saudi Arabia

 Mahujaji wakiwa Mina Saudi Arabia kwenye Jamaraat 
 Mahujaji wakiwa na marehemu na majeruhi katika msongamano wa Mina jana
Hali ya taharuki baada ya msongamano mkubwa ( stampede) huko Mina uliopelekea mahujaji zaidi ya 700 kufariki na mamia kadhaa kujeruhiwa.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Innalillah waina illah rajiun
    Allah awape subira wafiwa na awarehemu

    ReplyDelete
  2. La! poleni. Nimefarijika kumwona mzee wetu "King Majuto" akiwa fit kabisa. Be careful wazee wetu.

    ReplyDelete
  3. Haya matukio yanatokea kila mwaka, hivi serikali ya huko ina mpango gani kudhibiti umati kila mwaka? Wanajua watu wangapi wanakuja kuwepo na udhibiti wa umati.

    ReplyDelete
  4. Mbona wako tumbo wazi, inakubalika hii? poleni kwa wafiwa na majeruhi.

    ReplyDelete
  5. Inna Lillahi Wainna Ilayhi Rajiun. Yarabi wapumzishe katika kivuli chako, warehemu Yaa Arhama R'rahimina na uwaghufirie kwa yote na kesho Yaumul Hisabu wawe ni miongoni mwa mashahidi wako na waja wako wema utakaowaingiza katika yako Jannatu N'naeem - AMEEN YAA RABBAL ALAMINA.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...