
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Stephen Wasira
Na Eleuteri Mangi MAELEZO
Na Eleuteri Mangi MAELEZO
29/09/2015
Serikali ya Tanzania na Poland zimeingia makubaliano ya ushirikiano
yatakayosaidia kukuza sekta ya kilimo kwa kuwawezesha wakulima kupata zana bora
za kilimo kupitia Kampuni ya kutengeneza
Matrekta ya Ursus kutoka nchini Poland itakayoanza kufanya kazi zake nchini
Tanzania mwanzoni mwa mwaka 2016.
Akizungumza mara baada ya kufanyika kwa mkutano wa
makubaliano hayo kati ya Serikali ya Tanzania na ujumbe wa wataalam wa kilimo kutoka nchini Poland
ulioongozwa na Waziri wa Kilimo na Maendeleo Vjijini wa Poland Bi. Zofia Szalczyk
jana jijini Dar es salaam, Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Stephen Wasira
alisema kuwa makubaliano hayo yanalenga kuinua sekta ya kilimo na kurahisisha
upatikanaji wa matrekta hapa nchini.
Alisema Kampuni ya kutengeneza Matrekta ya Ursus kutoka Poland imepewa jukumu la kuleta vipuri vya matrekta
na kuviunganisha hapa hapa nchini ikishirikiana na Shirika la Uchumi na
Maendeleo la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT).
“Tumeingia mkataba na Seikali ya Poland ili kuinua na kuimarisha
sekta ya kilimo nchini kupitia uundwaji
wa matrekta haya hapa nchini, kazi hii itasaidia kupunguza kilimo cha jembe la mkono ambacho kinafikia asilimia
62 na asilimia 38 iliyobaki inajumuisha kilimo cha
jembe la kukokotwa na wanyamakazi “plau” pamoja na matrekta” Alisema.
Aliongeza kuwa Serikali itawajengea uwezo SUMA JKT ili
waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kuondoa hali iliyopo ya uagizaji wa matrekta
yaliyounganishwa ambayo hutumia gharama kubwa
na kusababisha wakulima wengi hushindwa
kumudu gharama ya kuyanunua.
“Wakulima wataunganishwa na Benki ya kilimo nchini kwa
kupewa mikopo mbalimbali ya kununua vifaa vya kutendea kazi mbegu pamoja na
mbolea ili kukifanya kilimo kiwe cha kisasa zaidi” alisema Wasira.
Wasira alisema kuwa Maghala yaliyopo nchini yanauwezo wa
kuhifadhi chakula tani 240,000 baada ya kukamilika ujenzi wa maghala hayo
kutakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 446,000 za chakula ambapo zitatumika Dola
za Kimarekani milioni 110 katika ujenzi wa maghala hayo.
Aidha, Wasira aliongeza kuwa ili kuwa na mafanikio katika
sekta ya kilimo nchini, Serikali itapeleka wataalamu wa matrekta kila mkoa.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo na Maendeleo Vjijini wa Poland
Bi Zofia Szalczyk alisema kuwa hatua iliyofikiwa na Serikali ya Tanzania ni ya
muhimu katika katika kuongeza tija katika uzalishaji kupitia sekta ya kilimo.
Alisema Poland imefanikiwa katika sekta ya kilimo kwa sababu
inashirikiana na taasisi za kifedha za kimataifa ambapo ameisifu Tanzania
kuchukua uamuzi huo ambao utaiwezesha kuwa na kilimo chenye tija.
Adha, ameishukuru Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa
Kilimo, Chakula na Ushirika pamoja na Waziri wa Fedha nchini na kuahidi
kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili katika masuala mbalimbali
ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...