Dar es Salaam, TANZANIA.  Leo asubuhi, Balozi wa Tanzania nchini Tanzania Mark Childress amewaapisha wafanyakazi wa kujitolewa wa Kimarekani (Peace Corps Volunteers) wapatao 59 ili kuanza huduma yao ya miaka miwili nchini Tanzania. Hafla ya kuwaapisha wafanyakazi hao ilifanyika katika viwanja vya Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Ukaguzi wa Shule ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk. Edicome Cornel Shirima, Mkurugenzi Mkazi wa Peace Corps nchini Tanzania Dk. Elizabeth O’Malley, watu waliowahi kuwa wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps katika sehemu mbalimbali duniani na maafisa wa taasisi wabia wa kiserikali na taasisi nyingine za kujitolea.
Katika hotuba yake, Balozi Childress aliwaambia wafanyakazi hawa wapya wa kujitolea wa Peace Corps kuwa “Mojawapo ya maneno yanayonivutia sana ninayoyasikia mara kwa mara nchini Tanzania ni neno pamoja. Neno hili linawasilisha moyo wa ushirikiano baina ya nchi zetu mbili na miongoni mwa Watanzania. Na hivi sasa mnapoanza safari na rafiki na wabia wenu wa Kitanzania, ninachoweza kuwaambia kuwa kwa pamoja mtakuwa na safari yenye kusisimua sana.”
Katika hotuba yake kwa wafanyakazi wapya wa kujitolea Dk. Shirima alirejelea maoni ya Balozi, akiwaasa kuwa “fanyeni kazi kwa bidii, fanyeni yaliyo mema, yafanyeni hayo kwa moyo wote, enzini uzoefu mtakaoupata na kuhusiana vyema na watu wa Tanzania. Kwani mtakuwa mkiishi na kufanya nao kazi  bega kwa bega katika shida na raha. Furahieni muda wenu mtakaokuwa hapa Tanzania.”
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Peace Corps Dk. Elizabeth O’Malley alisema “Kwa niaba ya Peace Corps Tanzania, ninapenda kutambua na kushukuru kwa ushirikiano mkubwa tunaoendelea kuupata kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa upande wa Zanzibar na Bara, hususan kutoka kwa Wizara za Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wizara ya Afya.  Aidha, napenda kuwashukuru Maafisa Elimu wa Wilaya na Wakuu wa Shule wanaotoa msaada mkubwa kwa watendaji wetu na wafanyakazi wetu wa kujitolea.”
Wafanyakazi wa hawa 59 wa kujitolewa walioapishwa leo watapangiwa kufanyakazi katika wilaya za Karatu, Kongwa, Chamwino, Mufindi, Iringa Vijijini, Hai, Rombo, Lushoto, Wete na  Nzega. Wengina watapangiwa katika wilaya za  Moshi Vijijini, Same, Ruangwa, Nachingwea, Hanang, Babati, Kiteto, Tukuyu, Kyela, Chunya, Mbarali, Masasi, Newala na Mtwara Vijijini. Wengine watakwenda katika wilaya za Mbinga, Shinyanga, Kishapu, Maswa, Singida vijijini, Iramba, Nzega na Lushoto.
Wafanyakazi hawa wa kujitolea wa kimarekani watatoa huduma kwa wanafunzi wao, shule na jamii watakazokuwa wakiishi kwa kufundisha masomo darasani pamoja na kuendesha miradi mbalimbali ya kijamii mathalan ile inayohusu lishe bora, stadi za maisha, afya bora, mazingira na mafunzo ya kusoma na kuandika.  Aidha, kwa miaka miwili ya kuwepo kwao hapa nchini, wafanyakazi hawa watachangia katika jitihada za Tanzania za kuongeza idadi ya walimu wa hisabati, Sayansi na Kiingereza hususan katika maeneo ya vijijini.

Peace Corps ni taasisi ya Serikali ya Marekani iliyoanzishwa na Rais John F. Kennedy mwaka 1961 ambayo hivi sasa inahudumia zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea zaidi ya 8,000 katika zaidi ya nchi 75 duniani. Kwa miaka 48, Peace Corps imekuwa taasisi inayoendesha shughuli za mabadilishano ya kiufundi na kitamaduni zisizoegemea mrengo wowote wa kisiasa na kidini.  Jumla ya wafanyakazi wa kujitolewa wapatao 189,000 wamehudumu katika nchi zipatazo 138. Peace Corps ina dhamira ya kukuza amani na urafiki duniani kwa kutekeleza malengo matatu yafuatayo:
·         Kutoa wafanyakazi wa kujitolea wa Kimarekani watakaochangia kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi itakayohitaji wafanyakazi hao;
·         Kukuza uelewa kuhusu Wamarekani miongoni mwa watu katika jamii zinazohudumiwa na Wafanyakazi wa kujitolea;
·         Kuimarisha uelewa wa Wamarekani kuhusu dunia na watu wake.
 Zaidi ya Wafanyakazi wa Kujitolea wa Peace Corps wapatao 2,000 wamehudumu nchini Tanzania toka mwaka 1962. Peace Corps hutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa kujitolea wa Marekani wanao fanyakazi katika jamii katika Nyanja za elimu ya sekondari (wakifundisha hisabati, sayansi na teknolojia ya mawasilianoa), afya na elimu ya mazingira.

Kwa taarifa Zaidi, tafadhali wasiliana na Japhet Sanga (SangaJJ@state.gov), Afisa Habari Mwandamizi wa Ubalozi wa Marekani

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...