Gazeti la Mwananchi la Tarehe 14/9/2015 toleo namba 5529 ukurasa wa 25 liliandika habari kuhusu Mwenge wa Uhuru chini ya kichwa cha Habari “Anayeumba Mwenge wa Uhuru” huyu hapa

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (WHVUM) ambayo ndiyo yenye dhamana ya Mwenge wa Uhuru inapenda kuufahamisha umma kwamba habari hiyo sio ya kweli na ni ya upotoshaji.

Mwenge wa Uhuru ni Chombo maalum na moja ya alama nyeti za Taifa la Tanzania. Mwenge wa Uhuru ni chombo chenye hadhi ya pekee na hivyo dhamana ya kukitengeneza haiwezi kupewa mtu binafsi kama alivyodai Ndugu Shaban Mwinchumu na kuandikwa kwenye gazeti la Mwananchi. Kwa sababu hiyo, kitendo cha kutengeneza au kuigiza chombo chenye dhana na falsafa ya Mwenge wa Uhuru ni ukiukwaji wa sheria za nchi.

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ingependa kuufahamisha umma kuwa Mbio za Mwenge wa Uhuru zilianzishwa rasmi mwaka 1964  na sio mwaka 1961 kama ilivyoandikwa katika toleo lililotajwa. Ieleweke kwamba, Mbio za Mwenge wa Uhuru tangu kuanzishwa kwake zimekuwa zikitumika katika kuwahamasisha wananchi wa Tanzania kuendelea kujenga upendo, umoja na mshikamano wa Kitaifa bila ya kubaguana kwa misingi ya kidini,rangi, jinsia, ukabila na itikadi za kisiasa.

Vilevile, Mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa zikitumika kuhamasisha na kuchochea  shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi kiuchumi na kijamii kupitia kwenye ujumbe maalum unaotolewa kila mwaka na miradi ya maendeleo inayobuniwa .

Wizara pia, inapenda kuufahamisha  umma wa Watanzania kuwa michango ya fedha inayotolewa na wananchi kwa ajili ya Mbio za Mwenge wa Uhuru si kwa ajili ya kugharamia mafuta ya Mwenge wa Uhuru unaokimbizwa kama ilivyodaiwa na gazeti la Mwananchi. Fedha zinazochangwa ni kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo hubuniwa na wananchi wenyewe. Aidha,  michango hiyo hutolewa  kwa hiari kutoka kwa mwananchi mmojammoja, Vikundi, Taasisi za Umma na Binafsi, Wadau wa Maendeleo, Serikali Kuu na Halmashauri za Wilaya.

Kwa Taarifa hii Wizara inasisitiza kuwa madai ya Ndugu Shaban Mwinchumu ni ya upotoshaji na hayana uhusiano wowote na masuala ya Mwenge wa Uhuru. Pia, Ndugu Shaban Mwinchumu hajawahi kupewa kazi ya kutengeneza Mwenge wa Uhuru anayodai kuifanya kwa muda mrefu kupitia Wizara ya Kazi, Ajira na Manendeleo ya Vijana kwani hakuna Wizara hiyo kwenye orodha ya Wizara za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mwisho kabisa Wizara inawataka waandishi wa habari na wahariri wa vyombo vya habari  kuandika habari kwa usahihi  zenye kujenga Umoja wa Kitaifa kwa kupata ufafanuzi wa kila upande ili habari itoe picha halisi badala ya kuegemea upande mmoja kwani kwa kuegemea upande mmoja hupotosha jamii na si maadili ya taaluma ya habari.


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Mimi sina chama (party) kikundi (group) au kijiwe (faction) cha siasa. Ni mpenda Tanzani yetu moja.

    Lakini naomba ufafanuzi (pengine, kutoka serikali au tume ya uchaguzi) kukataa habari za uwongo zinazotolewa na baadhi ya wapinzani kuwa kuwa CCM haijafanya lolote la maendeleo tangu uhuru. Huu ni uchochezi wa juu hasa unaolenga vijana wetu walozaliwa hivi majuzi ili kuikataa CCM na kuona Tanzania yetu kwa macho au darubini finyu ya wapinzani.

    Kama sio maendeleo, hao wapinzani wasingejulikana. Ajabu ni kusikia akina Mbowe, Lissu, na hata Esther Bulaya, Lowassa na huyo Sumaye naye anaiga wimbo wa mdundiko wa kuidhalilisha CCM. hawa wasingejulikana leo hii kama si kwa ajili ya bidii za CCM za kuleta wote pamoja nchini. Ni mawazo ya mende kufikiria kuwa maendeleo ya nchi yanapimika kwa darubini ya uchumi wa ki-quantity; na sio vingine. Maendeleo mengine sio lazima yawe ya kiuchumi; yanaweza kuwa ya kisiasa, kijamii, kisaikolojia, na kadhalika.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...