Mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mh. Bernard Membe akiwasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kushiriki katika kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa. ( Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog).
Na Mwandishi wetu
JUMUIYA ya Kimataifa imetakiwa kuwajibika kuhakikisha kwamba wanaweza kuwepo na amani na usalama kwa kuwa hilo ndilo tatizo kubwa duniani.
Hayo alisema Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mh. Bernard membe katika kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa.
Hafla hiyo imefanyika viwanja vya Mnazi Mmoja mapema zaidi kuliko tarehe iliyopaswa ya Oktoba 24 kutokana na Tanzania kuwa katika mchakato wa uchaguzi.
Waziri Membe alisema kwamba dunia kwa sasa ipo katika changamoto kubwa ya usalama kutokana na mizozo inayoendelea katika nchi kadhaa duniani.
Alisema kumekuwepo na wimbi kubwa la mapigano ndani ya nchi mbalimbali katika nchi mashariki ya kati, Ulaya na hata Afrika, kukua kwa ugaidi na siasa za kibaguzi.
“ Sote tunafahamu shida iliyopo katika nchi kama Syria, Iraq, Somalia, Libya, Afghanistan, Yemen na jamhuri ya Afrika Kati” alisema waziri Membe na kuongeza kuwa matukio ya vita ya mara kwa mara, misimamo mikali na ugaidi vimekuwa vikisababisha vifo vingi na mateso kwa jamii.
Kutokana na hali ilivyo kwa sasa dunia haiko katika hali ya amani na hivyo juhudi zaidi zinatakiwa kufanyika ili kurejesha amani ambayo ni kiungo muhimu katika maendeleo.
Pamoja na kuzungumzia haja ya amani kutokana na dunia sasa hivi kufikia kiwango cha juu cha wakimbizi ndani na nje ya nchi zao, Waziri Membe alihimiza mabadiliko katika uendeshaji wa Umoja huo ili kuleta uwiano wa uwajibikaji kimataifa.
Mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mh. Bernard Membe akisalimiana na baadhi ya wakuu wa Mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa nchini huku akiwa ameambatana na pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Liberata Mulamula (kushoto).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...