Rais Kikwete (Kushoto) na Ridhiwan Kikwete (Kulia).

MKAZI wa mjini Moshi, Kyefa Joachim Makundi (33), amepandishwa kizimbani akikabiliwa na mashitaka ya kumtukana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya  Kikwete.

Mbali na shitaka hilo, mshitakiwa huyo amesomewa shitaka lingine la kumtukana Ridhiwan Kikwete ambaye ni mtoto wa Rais Kikwete ambaye pia ni Mbunge wa Chalinze anayemaliza muda wake.

Mshitakiwa huyo amefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama ya mkoa Kilimanjaro, Joachim Tiganga na kusomewa mashitaka hayo na wakili wa Serikali Kanda ya Moshi, Agatha Pima.

Wakili Pima amedai mahakamani kuwa Oktoba 17 mwaka huu katika baa ya Harambee iliyopo katikati ya mji wa Moshi, mshitakiwa alitumia lugha ya matusi dhidi ya Rais Kikwete na mwanae Ridhiwan.

Ingawa matusi hayo hayakuandikwa kwenye hati ya mashitaka, lakini wakili Pima amedai kitendo hicho ni kinyume cha kifungu 89(1) (a) cha kanuni ya adhabu kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Chini ya kifungu hicho, mtu yeyote anayetumia lugha ya matusi, kuudhi, au kudhalilisha dhidi ya mtu mwingine katika hali ambayo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani anatenda kosa la jinai.

Adhabu inayotolewa kwa mtu anayepatikana na hatia katika kosa hilo ni kifungo cha miezi sita jela.

Hata hivyo, mshitakiwa amekana shitaka hilo ambapo mahakama imesema dhamana ilikuwa wazi ikiwa mshitakiwa atakuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya dhamana ya Sh1.5 milioni kila mmoja.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Wacha sheria ichukue mkondo wake. Tuondoe chuki binafsi

    ReplyDelete
  2. Kama alikuwa anajiamini kwa nini akane shiitaka akubali

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...