MGODI
wa dhahabu wa geita (GGM), umezalisha ajira zaidi ya 200 kwa jamii baada kuwekeza zaidi ya Sh1.7 Bilioni kupitia programu ya Uchumi
na Maendeleo (GEDP) ambayo imelenga kusaidia wakulima na wajasiriamali wadogo
na wa kati, wanaoishi jirani na mgodi.
Akizungumza wakati Mkuu wa Mkoa wa Geita, Fatma Mwassa
alipotembelea mgodini hapo juzi, Makamu wa Rais wa Anglo Gold Ashanti/GGM, Simon Shayo alisema mpango umelenga
kubadili hali za maisha ya wakazi kuwa tofauti na ilivyokuwa kabla mgodi
haujaanza kufanyakazi.
Alisema mradi umewasaidia wakazi hao na familia zao kuwa
na fani ambazo wanazitumia kwa uzalishaji na mbinu za kujipatia masoko katika
mji wa Geita na maeneo mengine nje ya mgodi huo.
"Hiyo inatokana na ubora wa mafunzo ambayo tunawapa sanjari
na mbinu za biashara" alisema meneja huyo na kuongeza kuwa zaidi ya ekari
800 zimetengwa kwa ajili ya kilimo cha Alizeti, Mpunga na mazao mengine na
utafiti wa udongo umekamilika.
Pia utengenezaji wa miundombinu kwa ajili ya umwagiliaji
unafanyika na upande mwingine, ununuzi wa mashine za umwagiliaji, uchomeaji,
mashine za kuzalisha umeme, vyerehani na mashine za kudarizi kwa ajili ya
wananchi hao wa Geita vinafanyika.
Meneja huyo alibainisha kuwa lengo ni kuhakikisha kunakuwa na
mnyororo endelevu wa thamani ya mazao ya kilimo kwa kuongeza viwango vyao vya
ufahamu katika mfumo wa masoko na kuongeza ubora wa mazao na wigo wa biashara
kwa wajasiriamali hao wadogo na kati.
"Tunatumia programu hiyo kwa ajili ya kuwawezesha wakazi
iuchumi na pia kupunguza kiwango cha umaskini" anasema na kuongeza kuwa
mpango huo utapunguza idadi ya vijana wasio na ajira Geita na wengine ambao
wamekuwa wakijitumbukiza katka uhalifu mgodini.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Fatma Mwassa alisema kuna matumaini
makubwa kuwa jitihada hizo za GGM zitazidi kukua na kubadili maisha ya walio
wengi kwa kuwawezesha kiuchumi wananchi wa Geita.
"Naamini sasa watauza mazao na bidhaa zilizokamilika na sio
ghafi kama awali na sio kwa Geita pekee bali pia nchi jirani" alisema
Mwassa. Kulingana na takwimu za hivi karibuni, kilimo kimetoa ajira kwa
asilimia 88 ya watanzania nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...