Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya mrisho Kikwete amesema kuwa atastaafu rasmi nafasi yake kama Rais wa Nne wa Jamhuri ya Muungano Alhamisi ya Novemba 5, mwaka huu, 2015, wakati Rais mpya na wa tano atakapoapishwa. 
 Aidha, Rais Kikwete leo, Oktoba 25, 2015 amepanga foleni kwa kiasi cha dakika 16 pamoja na wapiga kura wengine wa kijiji cha kwao cha Msoga, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani kwa ajili ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika leo. 
 Rais Kikwete akifuatana na Mama Salma Kikwete amewasili katika Kituo cha Kupigia Kura cha Hospitali ya Msoga kiasi cha saa sita na dakika 21 mchana na kwenda moja kwa moja kwenye foleni ya wapiga kura akiwa na watu kiasi cha 12 mbele yake. 
Akiwa anaendelea na mazungumzo na baadhi ya wanakijiji kwenye foleni, baadhi ya wapiga kura wenzake walianza kujisikia vibaya kuwa mbele ya Rais na kuanza kudai kuwa kuwemo kwake kwenye foleni kulikuwa kunachelewesha foleni na kuwa foleni ingekwenda kasi zaidi kama angetangulia kupiga kura. 
Kusikia hiyo, Rais aliomba radhi na kwenda moja kwa moja kwa msimamizi wa kituo hicho cha kupia kura kwa ajili ya kupiga kura. 
 Msimamizi wa kituo hicho alisoma nambari ya kadi ya uandikishaji wa kupiga kura ya Rais Kikwete kwa sauti ya juu ili mawakala wote waisikie – nambari 100377167974 - ikahakikiwa na baadaye akapewa karatasi za kupigia kura. 
Alifuatiwa kwenye kupiga na na mtoto wake wa kiume, Ali Kikwete. Mara baada ya kupiga kura, Rais Kikwete amewaambia waandishi wa habari kuwa tarehe yake rasmi ya kustaafu ni Alhamisi ya Novemba 5, mwaka huu, siku 11 kutoka leo, wakati Rais mpya wa Tanzania, Rais wa Tano atakapoapishwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. 
 “Nimetimiza haki na wajibu wangu kama raia wa nchi yetu kwa kupiga kura na sasa natamani kuwa siku yangu ya mwisho kazini ingekuwa kesho. Kwa bahati mbaya bado iko mbali na nalazimika kusubiri mpaka Novemba 5, wakati nitakapokabidhi madaraka kwa Rais wetu ajaye,” amesema Rais Kikwete na kuongeza: 
 “Nafurahi kuwa mpaka sasa hivi taarifa nilizozipata zinasema kuwa zoezi la upigaji kura linaendelea vizuri nchi nzima. Hakuna matukio yoyote ya matatizo. Ni utulivu mtupu kila mahali.” 
 Amesema kuwa atakuwa na mapumziko ya kiasi cha miezi mitatu mara tu baada ya kuondoka madarakani na baada ya hapo ataanza kazi ya kuunda na kujenga taasi yake mpya ya maendeleo. Alipoulizwa na mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha Citizen cha Kenya kama ataendelea kujihusisha na kujishirikisha na masuala ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), Rais Kikwete amesema: 
 “Tatakuwa na Rais mwingine ambaye ataendelea kuiwakilisha Tanzania katika shughuli za EAC. Mimi nimetoa mchango na imetosha. Naondoka mwenye furaha sana kuwa na mimi nilipata nafasi ya kuwatumikia wana-Afrika Mashariki. Kubwa ni kwamba nitaendelea kutoa mchango wangu kwa maendeleo ya nchi yetu kwa namna nyingine na katika nafasi nyingine kama raia maarufu wa nchi yetu.” 
 Mara baada ya kupiga kura na kuzungumza na waandishi kwa muda mfupi, Rais Kikwete ameondoka kituoni kwenda nyumbani kwake kuendelea na shughuli zake nyingine.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika foleni akisuburi zamu yake ya kupiga kura leo katika kituo cha hospitali ya kijiji cha Msoga kata ya Msoga wilayani Bagamoyo leo.
 Ofisa katika kitu cha kupiga kura akimkabidhi Rais Kikwete karatasi za kupiga kura.
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiandika kura yake ya siri.
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akipiga kura ya Rais Mbunge na Diwani katika kituo cha kupiga kura cha hospitali ya kijiji cha Msoga,Kata ya Msoga wilayani Bagamoyo leo.

KWA PICHA ZAIDI BOFYA HAPA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...