Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Michael Mhando
akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mikakati ya Mfuko huo ya
ujenzi wa Vituo vya mfano vya matibabu.
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unatarajia kuanza
ujenzi wa vituo vya matibabu vya mfano katika mikoa ya Mtwara na Kigoma katika
mwaka huu wa fedha wa 2015/2016.
Mikakati hiyo imesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF,
Michael Mhando wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na mikakati ya Mfuko katika uboreshaji wa miundombinu ya Matibabu.
“Tunatarajia kuwanza ujenzi wa Kituo cha matibabu
cha mfano mkoani Mtwara na hasa kwa kuzingatia kuwa Wizara
yetu ya afya pia inao mpango wa kujenga Hospitali mkoani humo.
Tunawasiliana na
Wizara ili tuunganishe nguvu zetu. Eneo tayari lipo na Mfuko umetenga kiasi cha
Tsh bilioni 3 kwa mwaka 2015/16,
lakini pia ujenzi Kituo cha Matibabu cha Mfano Mkoani Kigoma ambacho
kitatoa huduma kwa wanachama na wananchi wa mkoa huo na mikoa ya jirani,” alisema Bw. Mhando.
Aidha Mfuko umejipanga kupunguza msongamano wa wagonjwa katika
Mkoa wa Dar es Salaam ambapo umeanza kushirikiana na Uongozi wa mkoa ili
kuziwezesha hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke kuwa na vifaa vya kisasa
zaidi ili kuhudumia wanachama
wengi kupitia
huduma za matibabu na kliniki maalum zitakazokuwa zinaendeshwa na madaktari
bingwa wa hospitali hizo.
“Katika Jiji la Dar es Salaam mfuko utajenga kituo cha madaktari bingwa (Doctors Plaza)
katika eneo la Ubungo Maziwa ambako mfuko utaweka pia miundo mbinu kwa
ajili ya huduma mbalimbali. Kituo hicho kitawawezesha wanachama na wananchi
kupata huduma za kuwaona madaktari bingwa wa fani mbalimbali kwa urahisi na
katika eneo moja, hali ambayo itapunguza msongamano wa wagonjwa katika baadhi
ya vituo na kuboresha huduma jijini.
Bw. Mhando alisema kuwa mbali na juhudi za
uboreshaji wa huduma za afya zilizotajwa hapo juu, Mfuko pia umewekeza katika
ujenzi wa Ofisi zake katika Mikoa ya Mbeya, Dodoma na Tabora ambapo majengo
hayo yatawezesha upatikanaji wa nafasi kwa huduma za Hospitali za Doctors Plaza
ambazo zimekuwa zikihudumia wanachama wengi wa Mfuko.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...