THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea
kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Waziri wa Viwanda na Biashara,
Mheshimiwa Dkt. Abdallah Omari Kigoda ambaye aliaga dunia jana, Jumatatu,
Oktoba 12, 2015 katika Hospitali ya Apollo mjini New Delhi, India, ambako
alikuwa amelazwa kwa matibabu tokea Septemba 19, mwaka huu. Alikuwa na umri wa
miaka 62.
Katika
salamu za rambirambi ambazo amemtumia Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Peter
Kayanza Pinda, Rais Kikwete amesema: “Kwa hakika, nimeshtushwa na kuhuzunishwa
mno na taarifa za kifo cha Waziri Kigoda ambacho nimetaarifiwa kuwa kimetokea
India ambako alikuwa anapata matibabu tokea mwezi uliopita.”
Ameongeza
Rais Kikwete katika salamu zake hizo za rambirambi: “Kama unavyojua, namfahamu vizuri
Mheshimiwa Kigoda. Alikuwa Waziri wangu. Nimefanya kazi naye kwa karibu na kwa miaka mingi ndani ya
Serikali yetu. Alikuwa mtumishi hodari, mtumishi mwaminifu na mwadilifu kwa
wananchi wa Tanzania, na hasa wananchi wa Jimbo la Handeni, ambao
aliwawakilisha kwa miaka mingi akiwa Mbunge wao. Tutakosa utumishi wake mahiri
sana.”
“Nakutumia
wewe Mheshimiwa Pinda, Waziri Mkuu wa nchi yetu salamu za rambirambi za dhati
ya moyo wangu kuomboleza kifo cha Mheshimiwa Kigoda. Aidha, kupitia kwako
namtumia rambirambi nyingi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Anna Semamba Makinda na Wabunge wote kwa kuondokewa na mwenzao.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Nakuomba pia unifikishe salamu zangu za rambirambi kwa wananchi wa
Jimbo na Wilaya ya Handeni ambao wamepoteza Mbunge wao aliyewatumikia kwa
ustadi mkubwa kwa miaka mingi. Aliwawakilisha vizuri na kujali sana maslahi yao.
“
Amesisitiza
Rais Kikwete: “Kupitia kwako, Waziri Mkuu pia naitumia familia, ndugu, jamaa na
marafiki wa Mheshimiwa Kigoda kwa kuondokewa na mhimili wa familia na rafiki yao
mpenzi. Yajulishe makundi yote hayo kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa,
uchungu wao ni uchungu wangu na majonzi yao ni majonzi yangu. Nawaombea kwa Mwenyezi
Mungu awape subira na nguvu ya uvumilivu katika kipindi hiki kigumu na cha
majonzi. Pia naungana nao kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema peponi roho ya
Dkt. Abdallah Omari Kigoda”. Amen.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
13 Oktoba, 2015
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...