Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Maliasili Dr. Bakar Ased akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar umuhimu wa eneo ya hifadhi ya Misitu la Muyuni kwa ustawi bora ya maisha ya wananchi wa ukanda wa Kusini Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akitembelea msitu wa hifadhi Muyuni kuangalia maeneo ambayo baadhi ya watu wameamua kulima kilimo chengine mchanganyiko. Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Kilimo na Maliasili Mh. Sira Ubwa Mwamboya na kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dr. Idriss Muslim Hijja.
Othman Khamis Ame
Tamaa za baadhi ya watu katika kutaka kujimilikisha maeneo ya ardhi kwa nia ya kupata utajiri wa haraka hapo baadaye ndio chanzo kikuu kilichosababisha uchafuzi wa mazingira katika hifadhi ya msitu wa Muyuni Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja. .
Kauli hiyo ilitolewa na baadhi ya wana Kamati na wananchi wa shehia ya Muyuni “B” ambayo ilionyesha mgongano baina yao wakati wakimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika katika Msitu huo kuangalia maeneo ya Hifadhi ya Msitu ambayo baadhi ya wahusika hao wameamua kuyatumia kwa kuendeleza kilimo.
Eneo hilo la ardhi lililokubalika kutumiwa kuwa hifadhi ya Msitu na Wananchi wote wa Shehia Tatu za Muyuni A,B na C kwa takriban miaka 10 limekuwa na mgogoro wa matumizi kwa miaka minane sasa tokea kutolewa uamuzi wa kila shehia iunde Kamati yake ya Uhifadhi badala ya ile ya pamoja ya shehia hizo.
Wana Kamati hao pamoja na wananchi ambao mpaka ziara hiyo inamazliza wakihitilafiana walisema baadhi yao wamekuwa na malengo ya kuyatumia maeneo hayo na baadae kuyauza kwa vile tayari yamekuwa rasilmali kubwa katika masuala ya uwekezaji vitege uchumi vya sekta ya Utalii.
Walisema tabia ya baadhi ya wananchi wenzao ya kuanza kilimo cha minazi na miti mengine ya matunda na biashara pamoja na kisingizio cha sababu za kushutumiana kwa itikadi za kisiasa imechangia kuvuruga eneo kubwa la hifadhi hiyo muhimu kwa hatma yao na vizazi vijavyo.
Akitoa nasaha zake kwa wana Kamati pamoja na Wananchi hao wa Muyuni “ B “ Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa ushauri kuhusiana na mgogoro huo wa hifadhi ya Msitu wa Muyuni hapo baadaye.
Balozi Seif alisema utaratibu maalum utaandaliwa katika kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo kwa kuhusisha Viongozi wa Taasisi za Kilimo, Ardhi na Maingira ambapo wahusika hao watakuwa na uamuzi wa kuwaita watu waliohusika na mgogoro huo katika kuwahoji na kutaka ufafanuzi.
Alisema nia ya Serikali Kuu ni kuona hifadhi ya Msitu wa Muyuni inaendelea kubakia kwa maslahi ya Wananchi wa eneo hilo pamoja na Taifa zima kwa vile eneo hilo tayari limeshatangazwa ndani ya Gazeti la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Wananchi hao kwamba Zanzibar ikiwa niongoni mwa baadhi ya Mataifa ya Bara la Afrika imebahatika kuwa na rasilmani nzuri za maumbile lakini baadhi ya watu wamekuwa na tabia mbaya ya kuharibu kwa makusudi rasilmali hizo.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Mali asili Zanzibar Dr. Bakar Ased alisema eneo hilo la hifadhi hivi sasa baadhi ya sehemu linatumika kwa shughuli za kilimo kinyume na lengo lililokusudiwa kwa makubaliano ya Wananchi wenyewe na idhini ya Serikali.
Dr. Ased aliwatanabahisha Wananchi hao kwamba licha ya eneo hilo kulengwa kuwa hifadhi ya misitu lakini pia wataalamu wa mazingira na hali ya hewa wamefanya utafiti na kutoa ripoti iliyoeleza kwamba Ukanda wa Kusini ni eneo zima lenye Hewa safi.
Alisema kuvurugwa kwa hifadhi hiyo kwa shughuli nyengine za kilimo kunaweza kukasababisha kuwa chanzo cha uchafuzi wa hali ya mazingira na matokeo yake ni athari kwa viumbe hapo baadaye.
Kuna sehemu kubwa ya Eneo la hifadhi ya misitu la Muyuni ambayo kwa sasa in atumika kwa shughuli za kilimo mchanganyiko kama miembe, Minazi, Mivinje ,Migomba pamoja na mazao madogo madogo ya mizizi.
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
29/11/2015.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...