Ndugu Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, 

Nachukua fursa hii kukupongeza kwa kuchaguliwa kuliongoza taifa letu la Tanzania kama Rais wa awamu ya tano.

Nianze barua yangu kwa kugusia changamoto ya ajali nchini. Ajali limekuwa ni tatizo sugu licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na wadau mbalimbali kutoka taasisi binafsi na serikali. Ni hivi karibuni ripoti ya mwenendo wa ajali za barabarani imetolewa na Tanzania ikishika nafasi ya tano kwa kuwa na matukio mengi ya ajali barani Afrika. 

Ajali hizi zimekuwa zikipoteza raslimali nyingi sana ikiwepo raslimali watu na raslimali mali. Hii ni vita inayohitaji juhudi za wadau mbalimbali kupambana nayo kama ilivyo mapambano dhidi ya Ukimwi, Malaria, Rushwa n.k

Barua yangu inalenga kutoa ushuri katika mambo 16 ya fuatayo;
1.      Katika kuunda wizara zako, napendekeza kuwe na “Wizara ya Ujenzi ya Majiji” hii iwe maalumu katika kuratibu shughuli zote zinazohusu Masterplan ya Majiji yetu mbalimbali yaliyopo na yanayochipukia.Hii ijihusishe katika ujenzi wa barabara za kisasa kwaajiri ya miaka 50 ijayo.
2.      Miji yote mikubwa ijengwe “Ring roads” ili kupunguza misongamano ya magari isiyo ya lazima
3.      Taa za barabarani zibadilishwe kwa kuweka taa zinazohesabu kutoka 10 mpaka 0, ili dereva aweze kukadiria kama anaweza kuwahi taa pasipo kuleta madhara kama ilivyosasa.
4.      Maeneo ya Makazi au maeneo ya watu wengi kama Buguruni, Manzese, Mbezi ya Kimara, Mwenge na maeneo ya Mashuleni kama ilivyo Makongo na kwingineko kama maeneo haya yajengwe madaraja “FOOT -BRIDGES” ili watu wavuke maeneo hayo, tofauti na ilivyosasa watu wanavuka barabara huku mioyo wameshika mkononi.
5.      Kwa faida ya wengi, nyumba zilizokaribu na miundo mbinu ya barabara watafutiwe mbadala na kufidiwa kwa haki kulingana na thamani ya eneo lake kwa ajili ya kupisha barabara zinazofaidisha wengi.
6.      Vivuko maalumu viwepo kwenye barabara kwa ajili ya kuwapisha walemavu wanapotaka kuvuka barabara hizo.
7.      Kuwekwe Kamera barabara za mijini ili kuwawezesha askari wa barabarani wafanye kazi wakiwa ofisini badala ya kusimama juani kama ilivyo sasa.
8.      Kushughulikiwa swala la rushwa sehemu za mizani, Checkpoints ambapo ulegevu wa usimamazi wa sheria umesababisha barabara nyingi kuharibika kutokana na magari kuzidisha mizigo na kuruhusiwa kupita kwa urahisi maeneo hayo.
9.      Serikali na taasisi zake kufungua milango ili kuweza Kushirikiana kwa ukaribu na wadau wa Usalama barabarani kama ilivyo “Dereva Makini Tanzania”, “Road Safety Ambassadors Tanzania (RSA)”, “Amend Tanzania”, Safespeed Foundation n.k
10.  Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa watumiaji wa barabara mpya za mradi wa mwendo kasi kuwa ni nyembamba hususan maeneo ya Kimara, tunashauri usanifu wa barabara zingine katika miradi kama hii izingatie upana unaobaki kati ya gari moja na jingine ili kuondoa ajali zinazoweza kuzuilika.
11.  Tunakuomba ushughulikie kwa ukaribu sana tatizo ambalo linaonekana kuwa sugu linalo leta ajali za kuumiza sana, Malori yenye makontena (Semi-Trailers) kudondokea na kuyafunika magari madogo.
12.  Tunaomba pia liangaliwe upya swala la alama na blocks zinazowekwa kwenye makutano ya barabara na reli ikibidi kuwe na automatic blocks kuzuia magari treni inaposogea karibia na makutano haya.
13.  Tunakuomba uumalize mgogoro sugu uliopo kati ya madereva, serikali na waajiri kwakuwa tunaoumia ni sisi maskini tunaotegemea usafiri wa mabasi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
14.  Wachungulie kwa ukaribu wauza vipuli vya mabasi na ubora wa vifaa hivyo kupitia TBS kwa kuwa kuna watu wanapiga deal kwenye maisha ya watu.
15.  Yamulike makampuni ya mabasi na ya bima kuhakikisha wanakata bima kubwa kwaajiri ya mabasi yao, ili wahanga wa ajali walipwe stahili zao kama inavyostahili kuliko kama ilivyosasa kampuni ya bima inapiga deal na mmiliki wa mabasi.
16.  Angalia uwezekano pia wakuingiza technolojia ya Usafiri wa majini kupitia fukwe zetu mbalimbali za Bahari ya Hindi,Ziwa Nyasa,Victoria,Tanganyika na Rukwa yaani “AMPHIBIOUS BUS TECHNOLOGY” ambayo italiongezea taifa pesa kupitia Utalii wa majini "Ocean Tourism"

KWA HESHIMA NA TAADHIMA NAWASILISHA

Peter George Nzunda,
Mdau wa Usalama barabarani
+255687 966 638

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. umesahau mdau ,kumwambia dk magufuli askari wake wa barabarani wasumbufu mno mnoooo , wanaleta kero kubwa kwa wenye vyombo kila siku kusimamishwa na kuangaliwa leseni , bima nk , ikiwa tunapeleka vyombo kuchekiwa na kupewa stika ya usalama barabarani hio si tayari imetosha? huku kusumbuana awaambie hawa watu waangalie usalama na kuongoza magari na sio kuleta usumbufu na vitabu vyao vya risiti kutafuta watu kuwabambikizia makosa yasiyokuwepo , halafu ole wako uwe na rangi nyeupe au uwe mwanamke utajuta kuendesha chombo
    inspection ya magari au vyombo ifanyike mara moja kwa mwaka tu! tusisumbuane jamani hapa kazi tu , kama hawa matrafiki wako wengi naombe mkawape kazi nyengine vituoni au muwapunguze kazi ili serikali iokoe gharama za mishahara nk

    ReplyDelete
  2. Mdau,
    Ajali haziishi kwa kuwa sababu ya ajali hizo haijajulikana. Na juhudi zote za ufumbuzi zinatoa ufumbuzi ambao siwo wa kweli japo wafumbuzi wanaamini hivyo. Na kwamba wafumbuzi hao ni wadau tu wa usalama lakini si wataalamu wa usalama wa barabarani. Kuwa trafik polisi sio kuwa mtaalamu wa usalama. Wapo wabongo wengi wamesomea PhD katika fani ya usalama barabarani huko UDSM na vyuo vya nje lakini hatuoni wakishirikishwa kufanya tafiti za kisayansi ili kugundua tatizo badala yake ufumbuzi unakuwa wa nasibu tu. Watu wanagombea ulaji badala ya kufumbua tatizo la uhai wa raia.

    Hata wewe mdau, haya mashauri yako yametokana na uchunguzi wa kisayansi au hisia na dhana tuu?

    Rais ni PhD na nadhani atalitatua hili kisayansi kwa kutumia wataalamu PhD wenzake waliobobea katika fani ya usalama Bararabani.

    ReplyDelete
  3. Mdau namba mbili hujatoa suluhisho lo lote kuhusu usalama wa barabarani, umeendelea kulaumu tu. Afadhali hata huyo namba moja ametoa ushauri wenye muelekeo.

    ReplyDelete
  4. The mdudu, Asante sana mdau NZUNDA kwa maono yako mimi ntayapigania sana mpaka kieleweke coz yamenigusa vilivyo from number 1, 2, 3 and 4 wadau huu ndio mwanzo wa kuijenga Tanzania yetu kisasa kabisa so open letters kama hizi kwa rais wetu msikivu tena mchapa kazi usiku na mchana Tanzania yetu itabadilika kwa muda mfupi ujao sasa swali langu kwenu wadau wote number gani hapo mnazo zikubari? na mnao weza kuandika ma open letters kama hayo jitokezeni kwa wingi ili zimfikie kwa wingi kwa jinsi rais Magufuli alivyo lazima atazisoma na kuyafanyia kazi haya mapendekezo

    ReplyDelete
  5. Mdau wa tatu,
    Nimesema ufumbuzi wa ajali utokane na utafiti wa kisayansi utakaofanywa na wataalamu wa ajali za barabarani na siyo dhana na hisia za kinasibu za wasiokuwa wataalamu wa usalama wa usafiri. Mfano, kuwa askari polisi wa trafiki sio kuwa mtaalamu wa usalama. Bali ni msimamizi wa sheria za barabarani.

    Na hivi kwa nini kulaumu ni kubaya? Kama kanuni hiyo ipo basi ni mbaya. Unataka nshangilie kosa juu ya kosa? Kutotumia wataalamu na kupoteza fedha kwa ku-implement myths za wanaodhani wanajua usalama bararabani huku maisha ya watu yakiendelea kupotea.

    Ajali hazitoisha mpaka utafiti wa kisayansi ufanywe na wataalam (PhD na Professors). utafiti huo ni gharama hasa lakini si gharama kama maisha ya watu. Kwa hiyo hamna ufumbuzi wa bure. Tulipe fedha za utafiti au tupoteze maisha.

    Yaani unashangaza eti jamaa mtaalamu aje aandike ufumbuzi wa ajali kama mchango kwenye uzi katka blog. Haya mambo yako formal zaidi kuliko unavyofikiria. Utashambulia au utaelewa? najuwa sisi waswahili ni wazuri wa kuzungumza hata kama si msingi. Kubishia wataalam. Kuwa na imani potofu.

    Hebu angalia video za Prof. Kitila huko youtube. Hakuna majibu rahisi kwani rahisi inagharimu maisha.

    Uzuri, rais ameahidi kutumia wataalamu kutatua matatizo.

    Mdau wa pili.

    ReplyDelete
  6. Anon wa 3 na etc.
    Huwezi kutibu ajali kienyeji. Kienyeji nkimaanisha kwa kutumia mawazo yasiyo ya wataalam wa usalama wa usafiri. Hiyo itakuwa sawa na kuumwa ukaenda kwa mganga wa kienyeji na kuagua (ramli) badala ya kwenda muhimbili ukapigwa MRI au CT-Scan na daktari ajue unahitaji upasuaji, mionzi, au vidonge tuu. Unapoteza mda kwa mganga wa kienyeji mpaka hali inakuwa mbaya, badala ya kwenda sibitali, we unaendeleza kubadili waganga wa kienyeji.

    Kuwa na ajili nyingi haitokani na kulogwa au kutofata maelekezo ya askari trafik. Inatokana, kiasi, na kutotumia ufumbuzi wa kitaalam. Hatutatibu ajali kwa kuagua (ramli) au kubahatisha.

    Tena, kauli yangu haimaanishi kukunyima uhuru wa mawazo na uhuru wa kauli bali ni kukupa wazo kwamba tumia ufumbuzi sahihi kwa tatizo sahihi. Ama una uhuru wa maoni na kauli. Oni na kauli vikiwa havifai utapuuzwa na vikiwa vizuri utasifiwa.

    Michuzi naomba upeleke hii post mbele ili watu wasome zaidi na kuchangia. Maana kama mwandishi alivyosema, watu hawaoni ajali ni tatizo. Mpaka iwatokee wao. Na jawabu lao ni kwamba imetokea kwa bahati mbaya. hawataki kuepuka eti hazina kinga, wakati derea kalewa.

    Tufike mahali tusiamini bahati. Aje? Kwa kutumia sayasi kusoma tatizo na kufumbua. Wasomi wapo. Wanahitaji vifaa na uhai, watavipataje bila fedha? Watoe fedha zao? Wakati shule wamelipa ada yao? Si wazalendo kwa sababu walitakiwa kujitolea? Nchi haziendelei kwa zawadi zinaendele kwa kufanya kazi. Hamna fedha? Mbona mafisadi wanazo.

    Hapa kazi siyo kubahatisha.

    Mdau wa pili.

    ReplyDelete
  7. Nadhani umesahau kuwa wenye mamlaka ya kusimamia vyombo vya moto wanaitumia vbaya hiyo mamlaka waliyopewa kwa kugeuza ni sehemu ya wao kujiingizia kipato nje ya mshahara badala ya kusimamia wajibu wao.Bila ya kuweka mikakati ya kudhibiti rushwa kwa polisi ni ngumu sn kudhibiti ajali barabarani kwa vyombo vya moto. Traffic huwa wanawaandikia watu notification inayoonyesha makosa yalikutwa kwenye gari alilolikagua barabarani lakini wanachua fedha na hawatoi risiti ya serikali(ERV) na kuikosesha mapato serikali. Mfumo kuwa dhaifu wasimamizi nao wanaufanya kuwa fursa kwao sioni sababu ya Traffic Police kuwa na kitabu Notification lakini hana kitabu cha risiti(ERV)na kila siku wanachukua pesa za watu na hazifiki serikalini tutawezaje kuzuia ajali na kuongeza wigo wa mapato serikalini? Halafu tunasema nchi haina pesa mpaka wafadhili, ni kiasi gani cha fedha serikali inapateza katika chanzo tu cha faini za barabarani. Mhe. anakazi kubwa ya kubadili mifumo ya utendaji wa watu na taasisi wanazozisimamia.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...