Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim, Selemani Ponda (katikati) akiongea na waandishi wa habari kutangaza uuzaji wa dhamana ya kwanza ya muda mrefu nchini Tanzania yenye kuwezesha ushiriki wa wawekezaji wadogo ili kupata kiasi cha shilingi bilioni 15. Ameambatana na Meneja Benki ya Exim (uwekezaji), George Assenga (kulia), Meneja Miradi na Biashara wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, Patrick Mususa (wa pili kulia),  Mkurugenzi Mkuu wa Core Securities, George Fumbuka (wa pili kushoto) ambao ndio wenye dhamana ya uuzaji wa dhamana hizo na Mkuu wa matawi ya benki ya Exim, Agnes Kaganda.
 Mkurugenzi Mkuu wa Core Securities, George Fumbuka (wa pili kushoto) akiongea na waandishi wa habari kutangaza uuzaji wa dhamana ya kwanza ya muda mrefu ya benki ya Exim nchini Tanzania yenye kuwezesha ushiriki wa wawekezaji wadogo ili kupata kiasi cha shilingi bilioni 15. Ameambatana na Meneja Miradi na Biashara wa Soko la Hisa la Dar es Salaam, Patrick Mususa (kulia),  Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim, Selemani Ponda (wa pili kulia) na Mkuu wa matawi ya benki ya Exim, Agnes Kaganda.

Benki ya Exim Tanzania imetangaza uuzaji wa dhamana ya kwanza ya muda mrefu nchini Tanzania yenye kuwezesha ushiriki wa wawekezaji wadogo ili kupata kiasi cha shilingi bilioni 15. Benki imepanga kukusanya kiasi icho kwa ajili ya kuwekeza katika shughuli mbalimbali za ukuaji wa benki.

Hii ni dhamana ya aina yake na ya kwanza kutolewa nchini Tanzania inayowawezesha wawekezaji wenye kiasi kuanzia shilingi milioni moja kuwekeza kwenye dhamana zitakazoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Dhamana hii itawapa wawekezaji uhakika wa kupata riba ya 14% kwa mwaka isiyokuwa na makato ya kodi, itakayolipwa kila baada ya miezi 6 kwa kipindi cha miaka 6. Zaidi ya hayo, Wawekezaji wanaweza kutumia dhamana zao kwa ajili ya kuombea mikopo yoyote kwa kuzingatia taratibu zilizoko katika soko la Hisa la Dar es Salaam.

"Dhamana ya muda mrefu inayotolewa na benki ya Exim inawapatia wawekezaji wadogo na wa kati wasiokuwa na fursa za uwekezaji sawa na wawekezaji wakubwa, nafasi ya kipekee kupata gawio lisilo na kodi la asilimia 14 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka sita", Alieleza Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki hiyo, Bw. Selemani Ponda, wakati wa hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam jana.

"Kama ilivyo kwa mipango yetu mingi tuliyokwisha ianzisha, utoaji huu wa dhamana kwa umma unadhihirisha uvumbuzi wa Benki ya Exim katika kuendeleza soko la uwekezaji katika dhamana nchini Tanzania ili kuwezesha watanzania wote kupata huduma za kifedha, ''  alisema

"Tunayofuraha kubwa kuzindua dhamana ya kwanza ya muda mrefu kwa wawekezaji nchini Tanzania. Nina hakika kwamba dhamana hii itawavutia wawekezaji wadogo, ikiwa na marejesho mazuri, uwezo wa kuuzwa katika soko la hisa la Dar es Salaam na kuweza kuitumia kama dhamana ya kupata mikopo kutoka taasisi mbalimbali huku ikitoa fursa adhimu ya kushiriki kama mdau katika ukuaji wa moja ya benki tano zinazoongoza nchini Tanzania," alisema Bw. Ponda.

Kwa kiwango cha chini cha shilingi Milioni 1, riba ya 14%  isiyokuwa na makato ya kodi ni ya  ushindani sana ukilinganisha na  kiwango cha wastani wa 8% kwa mwaka kinachotolewa na taasisi nyingi, kwa mujibu wa Bw. Ponda.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Core Securities, ambayo ndio yenye dhamana ya uuzaji wa dhamana hizo, Bw. George Fumbuka, alisema mauzo yataanza kufanyika tarehe 23 Novemba, 2015 na kufungwa tarehe 18 Disemba mwaka huu.

“Katika kuhakikisha ushiriki wa wawekezaji wadogo ambao baadhi hawana akaunti za benki, Maombi ya ununuzi yanaweza kufanywa kupitia simu za mkononi kwa kupiga *150*36#, pia kupitia mawakala waliochaguliwa au katika matawi yote ya benki ya Exim yaliyosambaa nchi nzima. Kiwango cha chini katika uuzaji huu wa umma ni shilingi milioni moja,” alibainisha.

Bw. Fumbuka alisema wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika dhamana hizo wanaweza kupata fomu za maombi na taarifa muhimu za uwekezaji katika matawi yote ya Benki ya Exim na mawakala waliochaguliwa.

Bw. Fumbuka alibainisha kuwa kampuni yake kama wauzaji wakuu, iko tayari kuuza na kununua dhamana kutoka kwa wawekezaji muda wowote.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...