Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli , leo mchana amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kukutana na hali ya kumsikitisha.

“ Rais  amesikitishwa na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan wanaolala chini. Pia amekasirishwa na hali ya kutokujali wala kushughulikia vifaa vya kufanyia kazi ambapo amekuta mashine muhimu za uchunguzi wa magonjwa kama vile MRI na CT-SCAN zikiwa hazifanyi kazi kwa muda wa miezi miwili sasa, ilihali mashine kama hizo katika Hospitali za binafsi zinafanya kazi na wagonjwa wanaelekezwa kwenda kutafuta huduma huko”.  Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema na kutoa maelekezo yafuatayo :
Rais, Dkt. John Pombe Magufuli akimjulia hali mmoja wa wagonjwa waliolazwa kwenye kwenye wodi ya sewahaji, kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es salaam leo wakati wa ziara yake ya kushtukiza .

Rais amevunja Bodi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo ilishamaliza muda wake na amemteua Prof. Lawrence Mseru , kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Muhimbili kuanzia kesho tarehe 10 Novemba, 2015.

Dkt. Hussein L. Kidanto ambaye ndiye anayekaimu hivi sasa, amehamishiwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambako atapangiwa kazi nyingine.

Balozi Sefue pia amesema,   Rais ametoa wiki moja na kwa vyovyote si zaidi ya wiki mbili kwa uongozi mpya wa Muhimbili kuhakikisha kuwa mashine zote za uchunguzi wa magonjwa ambazo hazifanyi kazi zinafanya kazi na kuhudumia wananchi kama ipasavyo.

Tayari Wizara ya Fedha imetoa shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kazi hiyo na kulipa madeni ya ukarabati wa mashine za uchunguzi wa magonjwa nchini.

Hata hivyo Katibu Mkuu Kiongozi amesema kuanzia sasa hospitali zote nchini zinatakiwa kutenga fedha kutoka kwenye mapato yao wenyewe na kuhakikisha mashine na vifaa vyote vya kazi vinafanya kazi wakati wote (Regular Maintenance).

Balozi Sefue pia metumia nafasi hii kuwaagiza watendaji na viongozi wote katika sehemu za kazi kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo na kazi za umma zinatekelezwa ipasavyo.

“Hakutakuwa na huruma kwa watumishi wa Umma wasiojali wananchi na mahitaji yao” Amesisitiza Balozi Sefue.

Imetolewa na; 

Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
9 Novemba, 2015

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 16 mpaka sasa

  1. The mdudu, hivi hawa watumishi wa umma wana matatizo gani na wanachi? Mbona wanakua kama wanyama nakuomba sana Rais wetu Magufuli tusiludie tena makosa ya nyuma mtumishi au watumishi wa umma wanapo fanya makosa dawa yao iwe ni kufukuzwa kazi haipendi watu kama hao uwahamishie sehemu nyingine dawa kubwa kwao ni kufukuzwa kazi samba mba na kufungwa kwenye magereza

    ReplyDelete
  2. Anon 1, kumfukuza mtu kazi ni shurti ufuate sheria na taratibu za kazi. Na kumfunga mtu lazima kuwe na ushahidi na mahakamani lipatikane kosa kisheria, linalowezesha mtu kufungwa. Kama ni vitendo vya rushwa, uzembe wewe na mimi ndiyo wenye ushahidi, hivyo tunapaswa kuwafungulia mashtaka hao watendaji na tuwasilishe ushahidi wetu. Sio kila kitu Raisi, wewe pia una wajibu wako, tekeleza!

    ReplyDelete
  3. naona Dk Magufuli kawasahau dada na mama zetu kule kwa wazazi kuna madudu ya kila aina , na kuteswa na wakunga , tunaomba siku nyengine awakurupukie bila taarifa wala mikwaruzo akagufulike nao.

    ReplyDelete
  4. God Bless You Mr President!!! We are heading to the right direction. Hapa Kazi Tu!!!!!!!!! I'm pumped with this new Tanzania.

    ReplyDelete
  5. Greedy, Greedy, Greedy . watanzania tumeingiwa na greedy ya hali ya juu.tunauwa huduma za umma maksudi ili tunufaishe wachache.
    Ukiangalia namna ambayo mashirika yetu ya umma yalivyohujumiwa makusudi ili kutoa mwanya wa wafanyabiashara wachache wafaidi wao na familia zao. Ukiangalia kwa makini kila shirika la umma lililokufa iliota kampuni ya mtu binafsi.Mfano ni
    NBC - NMB, CRDB nk
    ATC - Precision Air
    Reli ya kati/ Tazara - mabasi ya watu binafsi.
    National Milling - Azam / MELT
    RTC -
    UDA-
    Na mengineyo .

    ReplyDelete
  6. Mashallah wewe ndio kiongozi tunaekuhitaji inshallah mungu akupe nguvu,ujasiri hekima imani, ili uweze kutambua mazila tunayoyapa sisi raia wako hususan wanyonge na masikini jitahidiii baba uwe mfano wa kuigwaaa na mungu akusaidiee ili tufikie malengo mema kwa nchii yetu amina!!!!!

    ReplyDelete
  7. Mungu akuzidishie baba akupe ujasiri na nguvu kulitumikia taifaa lako na wananchiiii waako naomba mheshimiwa rais kamba iyo iyo zidishaaa uwe mkali kwelikweli kwa hao watumishiii wa umma mungu akubariki nimeguswaaa sanaaa na jitihada zako kutaka kutuletea maendeleo hapa ni kazi tuu lazima tujivunieeee rais wetu wa mabadilikooo yaaanakuja inshallah hakuna kulala

    ReplyDelete
  8. Moto mzuri wa kuanzia. Ila tu usije fifia hii ikawa ni danganya toto.

    ReplyDelete
  9. I love this president. Tz sasa tutaendelea. We been so sleepy. Mr. Pres. Naomba madeni ya zabuni yalipwe ili wafanyabiashara wanaoidai serikali waweze kuendesha biashara na kuongeza ajira. Walimu walipwe on time from now bcse pale wizarani wanakalia pesa ili wazungushie kwenye biashara zao binafsi.

    ReplyDelete
  10. Kumbe hela zipooo ila hadi Rais aseme!! mmhhh kweli tushazoea kuendeshwa kwa fimbo kama punda

    ReplyDelete
  11. MH. TUSAIDIE KIMARA TUPATE MAJI.

    ReplyDelete
  12. Mto wa mkulima huyo. Hakuhonga wala hataki kuhongwa. Hakupewa ki-memo. Kajaaliwa kufika hapo. Anajuwa kuwa mkulima kunavyoumiza.

    ReplyDelete
  13. Dkt Rais.
    Adhabu ziko mbili.
    1) Adhabu hafifu hapa duniani: jela, magereza, kufilisi, kufutwa kazi.
    2) Adhabu nzito ya Jehanam baada ya kufufuliwa.

    Wewe kazi yako ni kuadhibu adhabu ya kwanza. Usiache na kusema eti adhabu ya pili ipo. Hawatajifunza kuacha uovu. Na itakuwa mfano mbaya kwa kizazi kijacho kwamba ukifanya kosa basi kiongozi anakuacha ili ukaadhibiwe na Mungu.

    ReplyDelete
  14. Inabidi Wizara ya Afya ifungue Kituo cha Matengenezo Ya Vifaa vya Wauguzi.

    Kituo Hicho kiweze kukarabati vifaa vilivyo na matatizo vya Hospitali za Serikali Tanzania Nzima.

    ReplyDelete
  15. Mimi nilikuwa Chadema muda mrefu, ila nilikoma baada ya kusikia Ccm imempitisha Mzee Magufuli. Siku zote nilikuwa nahisi Ccm haiwezi simamisha mtu makini kama Magufuli. Jamaa si fisadi, si brazamen, just a simple guy, mchapakazi na pia hana urafiki na wazembe. Huyu ndo Magufuli nimemfahamu siku zote na sitegemei jamaa atabadilika. So kwa wale wanaodhani hii ni nguvu ya soda, no no no siyo kwa Magufuli bana,... pale #KAZI TU

    ReplyDelete
  16. Hiyo kazi aliyofanya Rais hapo Muhimbili, ingeweza kufanywa mapemma na na huyo Katibu Mkuu Kiongozi akisaidiana na Waziri wa Afya, bila hata ya kumhusisha Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu. Lakini wao ni kukaa maofisini na kuvaa matai ili wafuje gharama za air-conditioners zinazokula umeme kwa gharama kubwa.

    Pengine, madudu mengi yakionekana katika wizara na mashirika ya umma, yafaa huyo Katibu Mkuu Kiongozi atolewe, kama alivyokuwa akifanya Rais Nyerere kutangaza kwa njia ya RTD viongozi wapya kila siku ya Jumapili jioni. Kwa Nyerere, kufurunda kazi iikuwa ni tikiti ya kuhamishwa au kufukuzwa kazi mara moja.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...