Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akizungumza na Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini leo Ikulu jijini Dar es salaam kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.
Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli  katika picha ya pamoja Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu, Watendaji Wakuu serikalini leo Ikulu jijini Dar es salaam baada ya kukutana nao na  kupanga mikakati ya kuendesha serikali kwa weledi, nidhamu na moyo wa kupenda kazi.
PICHA NA IKULU
Kwa picha zaidi BOFYA HAPA


     Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli leo asubuhi katika Ikulu ya Dar es Salaam  amefanya kikao na Makatibu wakuu, Manaibu Makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu Prof. Benno Ndulu na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)  ili kutoa uelekeo wa Serikali anayoitaka  mara baada ya  kuapishwa.
     “Nataka Serikali iendelee kwa nguvu zote na katika kutekeleza dhana ya ‘HAPA KAZI TU’ na viongozi kuzingatia na kukumbuka ahadi nilizotoa ili zianze kuonekana na kufanyiwa kazi mara moja” Rais Magufuli amesema.
     Katika Kikao chake, Rais ametoa mwongozo na kusisitizia kuwa ni lazima kila mtendaji Serikalini kuuzingatia, kufuata sheria na taratibu ili taifa lisonge mbele kwa ufanisi zaidi.
     Katika kikao hicho Rais ameelekeza mambo kadhaa ambayo watendaji hao wanapaswa kuyasimamia, kuyawekea mikakati na kuyapanga vizuri ili atakapo teua Baraza lake la Mawaziri mambo hayo yawe tayari ili Mawaziri watakaoteuliwa waweze kuyasimamia bila kukosa.
     Mambo hayo muhimu ni kama ifuatavyo:
1.      Kuanzia mwezi  Januari mwaka 2016, wanafunzi wote wanaoanza shule watasoma bure bila kulipa ada, Katika jambo hili, Rais amewataka watendaji kuanza kuliwekea mikakati tayari kwa utekelezaji
2.      Suala la mikopo ya wanafunzi nalo lifanyiwe kazi na mipango yake ikamilike kwa ajili ya utekelezaji mzuri zaidi
3.      Amefuta safari zote za nje ya nchi kuanzia leo hadi hapo atakapolitolea suala hilo maamuzi mengine na kueleza kuwa shughuli zote zinazotakiwa kufanywa nje ya nchi zifanywe na kusimamiwa  na mabalozi wa Tanzania  wanaowakilisha nchi  huko nje.

Pengine patokee jambo la dharura sana na hata hilo lazima kibali kitolewe na Rais au Katibu Mkuu Kiongozi. Badala yake Rais amewataka watendaji hao kufanya zaidi ziara za kwenda vijijini ili kuzijua na kutatua kero za wananchi wa Tanzania.
     Katika Kikao hicho, Rais amemtaka Kamishna wa TRA, Ndugu Rished Bade kusimamia kwa makini zoezi la ukusanyaji wa mapato nchini na kuhakikisha kero ndogo ndogo kwa wananchi lianze kutekelezwa kama alivyo ahidi kwa  kufanyiwa  kazi mapema  zaidi.
     Rais ameitaka TRA kukusanya mapato hayo kutoka kwa wafanya biashara wakubwa zaidi na wale wanaokwepa kodi bila kuogopa mtu wala taasisi yoyote hapa Tanzania na kusisitiza kuwa katika Serikali hii wa kutoa maamuzi vinginevyo zaidi ya haya ni yeye Rais  ama Makamu wake.
     Rais Magufuli pia ameagiza usimamizi katika suala la manunuzi ambalo limekuwa likitumika vibaya na kuwa mwanya wa kuibia Serikali  kwa watu kuongeza bei ya vitu hata kama ni vya bei ndogo kabisa katika jamii.
     “Ikitokea suala hilo likagundulika kwa watu kuongeza bei ya vitu, watendaji watawajibishwa mara moja”. Rais amesema, na kuwataka watendaji hao kufanya kazi zao kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo na kuzingatia maadili mema ya kazi.

Imetolewa na Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

7 Novemba, 2015
 .




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 10 mpaka sasa

  1. Nimeipenda hii. Naona ufisadi unaanza kuyoyoma.

    Mdau ughaibuni.

    ReplyDelete
  2. Umuhimu wa thana ya "HAPA KAZI TU" nchini ni sawa na umuhimu wa moyo mwilini. Japo mapapa waliyozowea kutula sisi samaki wadogowadogo watakwazika na dhana hiyo, lakini mapapa hao hawana hati miliki ya kumiliki nchi yetu wala kibali cha kutukoseshea mapato yakutuhudumia katika uchumi, elimu, afya n.k. Hivyo utekelezwaji wa dhana hiyo unahitaji kufanyika kwa spidi 700 kama ile ya ndege ya kivita.

    ReplyDelete
  3. Umeanza vizuri ndugu rais. Ukiendelea na mwendo huu, watanzania wataanzania tutaanza kunufaika na nchi yetu

    ReplyDelete
  4. misamaha mingi ya kodi wanapewa watu wa mashirika NGO na watu wa mashirika ya kidini , hii ifutwe pia kama kukusanya kodi iwe kwa wote sio kuwanyonya wafanyabiashara tu. Muache kuwanyonya watu wa rangi fulani fulani kuwa ndio wakutoa kodi na wa rangi nyengine wasitoe , usawa kwa wote. Na kutoa ruzuku kwa mashirika ya kikiristo peke yake pia ifutwe , au mashirika ya dini zote wapewe mgawo sawa kama makundi ya waisilamu , kuna wahindu , mabohora , mashia , ma agakhan nk huo ndio utakuwa usawa , au wote wasipewe. Serikali iliyoingia madarakani iache upendeleo kwa dini ya kikiristo , wafanyakazi asilimia zaidi ya 90 serikalini ni wao , jee hii ni haki na usawa? naomba Dk Magufuli aliangalie vizuri ili arekebishe kwa maarifa na vitendo.

    ReplyDelete
  5. Safi Sana magufuli waliokuwa Na tenda Za kifisafi Za viongozi kwishaa Watu wasiwe comfortable mfano kiongozi ticket yake NI $2000 kwasababu serekali hailipii Hapo Kwa Hapo Basi wajanja wanalipia Alafu wanachaji serekali $8000 per ticket piga viongozi wote WA serekali wanaosafiri NI billion ngapi zinapitea Hapo viva pombe

    ReplyDelete
  6. pamoja na hayo yote, hiyo baraua pepe ya kutumia googlemail.com sijui ikoje. Kwa nini isitumike: ?

    Manake hiyo ya googlemail.com huenda ni ya bure na huku, pengine, ikulucommpress waliomba pesa za kulipia na kuendelea kulipia gharam ayake. I may be wrong!

    ReplyDelete
  7. The mdudu, Asante sana rais wetu haya ndio mambo tuyatakayo sasa wafanyakazi wote ndani ya Tanzania mjenge utamaduni wa kufanya kazi kwa kujituma na kwa uzalendo wa hali ya juu kabisa na muondokane na mambo ya vishawishi na uzembe mtu yeyote akikushawishi mfanye jambo baya huku ukijua unaweza kujikuta kwenye janga la kujitakia mlipoti huyo mtu kwa bosi wako ili uwe salama kabisa ni hayo tu kwa wafanyakazi wote hapo Tanzania sisi wote tuko nyuma yenu so pigeni kazi kwa mwendo wa HAPA KAZI TU

    ReplyDelete
  8. Naamin sasa tutanufaika na raisi wetu atalifikisha taifa sehemu mzuri na kuendeleza alipoishia dk kikwete

    ReplyDelete
  9. Tunaiman kubwa sana na raisi wetu Dk magufuli atalifikisha taifa hili mahala.pa zuri na kuendeleza mema aliyoyacha dk jakaya

    ReplyDelete
  10. We anon wa hapo juu. Tuliza boli. Naamini Magufuli ndo mtu anayeweza kuleta usawa kwa kuondoa imbalance ya ajira iliyopo baina ya wakristo na waislamu. pia atatoza kodi kiadilifu si kuwaumiza wahindi wakati wengine laa. pia ruzuku za dini zitarejewa upya (MOU). Pia mikataba ya madini nk.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...