Pamoja
na kupanda kwa bei za pembe za ndovu kuanzia mwaka 2010 kufikia mwaka
2014, thamani ya meno ya tembo imeshuka kwa kiasi kubwa nchini China
jambo ambalo ni habari njema kwa Tanzania katika harakati zake kukomesha
ujangili wa pembe za ndovu.
Taarifa
mpya ya utafiti uliofanywa na watafiti Esmond Martin na Lucy Vigne wa
shirika la Save the Elephants na kutolewa wiki hii imeainisha kwamba bei
za meno ya tembo ghafi nchini China zimeshuka kwa zaidi ya nusu katika
kipindi cha miezi 18 iliyopita kutoka dola za Marekani 2,100 kwa kilo
moja hadi kufikia dola 1,100.
Katika utafiti wao uliofanya katika majiji nane nchini, watafiti hao
wamegundua kwamba mahitaji ya meno ya tembo na bidhaa zitokanazo na
pembe za ndovu yanaendelea kushuka kwa kasi kubwa kuliko ilivyowahi
kutokea.
Viwanda
vinavyotengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na pembe za ndovu
vimeripoti kuwepo na uhaba wa pembe za ndovu na vibali vinavyotolewa na
serikali kuwaruhusu wafanyabiashara kuuza pembe za ndovu kihalali
vimecheleweshwa.
Matokeo ya utafiti huu mpya yanaenda sanjari na ongezeko kubwa la uelewa
wa watu nchini China ambapo sasa sehemu kubwa ya jamii inaelewa madhara
ya tatizo la ujangili kwa tembo wa Afrika na uelewa huu umeongezeka
maradufu kati ya mwaka 2012 na 2014 kwa mujibu wa taarifa ya Wildaid,
Save the Elephants na African Wildlife Foundation.
'Wakati
hali hii ikijitokeza, serikali ya China imepiga hatua kubwa katika
kudhibiti soko la pembe za ndovu tangu mwezi Septemba ambapo Rais wa
nchi hiyo Xi Jinping alitangaza kwamba China na Marekani zitashirikiana
kukomesha biashara ya pembe za ndovu.
Akizungumza kuhusu utafiti huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la
Wildaid, Peter Knights amesema:
“Kuanguka
kwa bei ya pembe za ndovu nchini China ni habari nzuri tuliyotaka
kusikia japo bado kuna kazi kubwa hii ni hatua muhimu sana katika
kukomesha janga la ujangili. Kupigwa marufuku biashara hii nchini China
na Marekani vitatoa shinikizo kwa Hong Kong, Thailand na Japan nazo
kupiga marufuku biashara hii. Pia hii itazipa moyo nchi za Kenya na
Tanzania kuendelea kupambana na ujangili.”
Tangu
mwaka 2012, mashirika ya WildAid, Save the Elephants na African
Wildlife Foundation yaliungana kufanya kazi ya uhamasishaji juu ya
ujangili nchini China kwa kuwatumia watu maarufu nchini humo kama Yao
Ming mcheza mpira wa kikapu NBA zamani na muigizaji Li Bingbing ambao
kupitia matangazo mbalimbali wamekuwa wakihamasisha jamii kuacha
kununua, kugawa au kupokea pembe za ndovu kama zawadi.
Mashirika makubwa ya habari nchini China ya CCTV na Xinhua nayo yametoa
msaada mkubwa katika jitihada hizi kwa kutoa matangazo yenye thamani ya
dola za Marekani milioni 42 bure ambapo matangazo hayo yamewafikia
mamilioni ya wananchi wa China.
Vilevile
jitihada hizi pia zimesaidiwa na Mwanamfalme wa Uingereza Prince
William ambaye alitoa hotuba ya kihistoria mwezi Oktoba na kuwaomba
wananchi wa China kukataa kabisa biashara ya pembe za ndovu.
Akizungumza kuhusu anguko hilo la bei ya meno ya tembo Balozi wa WildAid
Jacqueline Mengi amesema:
"Upunguaji
wa mahitaji ya pembe za ndovu huko nchini China ni ishara kwamba
jitihada za Wildaid pamoja na serikali za nchi tofauti zinaendelea kuzaa
matunda. Mwaka jana tulizindua kampeni maalum ya kuongeza ufahamu na
kuielimisha jamii kuhusu tatizo la ujangili linaloikabili Tanzania. Kwa
matokeo ya utafiti huu ni dhahiri kwamba mwamko wa kulinda tembo wetu
umeongezeka.”
Mashirika
ya WildAid, African Wildlife Foundation na Save the Elephants yamekuwa
yakiipa shinikizo kubwa Hong Kong nchi inayodaiwa kuwa kituo kikubwa cha
biashara hiyo duniani. Baada ya mashirika hayo hivi karibuni kutoa
filamu iliyochukuliwa kwa siri ikionyesha jinsi ambavyo Hong Kong
imeshindwa kudhibiti biashara hiyo haramu, maafisa wa serikali hiyo
wameonyesha dalili za kuwa tayari kukomesha biashara hiyo jambo ambalo
linaungwa mkono na Baraza a Sheria la Hong Kong.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...