Na Rahma Khamis -Maelezo, Zanzibar
Waalimu Nchini wametakiwa kuwapa fursa na kuwahamasisha wanafunzi wa Skuli mbalimbali kushiriki katika michezo ili kuwezesha kupata timu nzuri na kushiriki katika mashindano ya Kimataifa.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Wizara ya Habari Utamaduni Wasanii na Michezo Tanzania Leonaed Thadeo katika Uwanja wa Amani nje wakati alipokua akifunga Shamrashamra za Tamasha siku ya Walimu Duniani.
Amesema nchini Tanzania wananchi wengi hulalamika kwa kutofanya vizuri katika michezo kutokana na Waalimu kusahau wajibu wao wa kuwajenga wanafunzi wao kimichezo tangu wadogo wakati wapo Maskulini jambo ambalo linarejesha nyuma maendeleo ya michezo hiyo.
Aidha amefahamisha kuwa iwapo jamii itashiriki katika michezo mbalimbali itaweza kujiepusha na mararadhi sambamba na kujenga afya hivyo zoezi hilo liwe endelevu kwani kufanya hivyo kutasaidia walimu kuwa imara kimichezo.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo amewataka waalimu kutoa fursa kwa kushirikiana na Wizara huusika kwenda kusoma katika Chuo cha Maendeleo ya michezo Tanzania Bara ilikuongeza uwezo na idadi ya waalimu wa michezo.
Kwa upande wake mwalimu Mussa Abdulrabi kutoka Wizara ya Elimu amesema lengo la kufanya tamasha hilo ni kuwafanya walimu kushiriki michezo mbalimbali na kuonesha vipaji vyao katika michezo hiyo.
Amesema katika mwaka huu hakuna changamoto zilizojitokeza hivyo wanajiandaa mwakani ili wawe na uwezo wa kufanya vizuri zaidi katika tamasha lijalo .
Sambamba na hayo mwalimu huyo ameaahidi kuwa watawashajiisha walimu wenzao kwenda kujiunga na Chuo cha Maendeleo ya Michezo ili kupata walimu wengi kwa ajili ya michezo kwani Serekali ina nia ya kuendeleza Michezo .
Wakielezea furaha zao washindi katika Tamasha hilo wameiomba Wizara kuangalia suala la michezo zaidi kwa kuandaliwa mafunzo maalum ili kuweza kushiriki katika mashindano mbalimbali.
Katika shamrashamra hizo kumefanyika michezo ya ikiwemo kuvuta kamba, Mpira wa Mkono, mbio za Gunia pamoja na Mpira wa miguu kutoka katika Mikoa mitatu ya Zanzibar ikiwemo Mkoa Kusini Unguja , Kaskazini Unguja na Mkoa wa mjini Magharib ambapo Mkoa wa Kaskazini na Mjini ndio walioibuka washindi ikifuatiwa na Mkoa wa Kusini Unguja.
Walimu walioshiriki mashindano ya michezo mbalimbali wakionyesha vipaji vyao katika mashindano yaliyofanyika viwanja vya nje Amani Mjini Zanzibar
Walimu walioshiriki mashindano ya michezo mbalimbali wakishindana kuvuta kamba
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo Tanzania Leonard Thadeo akitoa maneno ya shukurani wakati wa kuwakabidhi zawadi washindi wa mashindano mbali mbali ya Walimu kutoka Wilaya 3 Kaskazini, Mjini na Kusini huko katika viwanja vya nje Amani Mjini Zanzibar.
Washindi walishiriki katika mashindano mbali mbali wakipewa zawadi na Mgeni Rasmi Leonard Thadeo mara baada ya kumaliza mashindano hayo
Washindi walishiriki katika mashindano mbali mbali wakipewa zawadi na Mgeni Rasmi Leonard Thadeo mara baada ya kumaliza mashindano hayo
Picha zote na Miza Othman - Maelezo, Zanzibar
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...