Watanzania wametakiwa kuwekeza kwa kuwapatia vijana wao elimu ya juu ili kuwawezesha kuwa na maarifa yatakayowasaidia katika maisha yao na kutoa mchango kwa taifa. 
 Akizungumza katika mahafali ya 14 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Josephat Itika alisema elimu bora ndio njia ambayo itaweza kuwezesha vijana kufanikiwa na taifa kupata maendeleo endelevu. 
 “Elimu ndio chachu ya kweli ya maendeleo, ni lazima wazazi na walezi kuzingatia hili,” alisema Prof. Itika mwishoni mwa wiki. 
 Aliongeza kusema kuwa Mzumbe imekuwa kielelezo na kitovu cha elimu bora katika kutoa mchango wake kwa taifa kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Katika Mahafali hayo, Mkuu wa Chuo hicho, Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samatta aliwatunuku wahitimu mbalimbali katika Kampasi Kuu Mzumbe baada ya kuhitimu masomo yao. 
 Jumla ya wahitimu wote walikuwa 1990; wanawake wakiwa 900 sawa na asilimia 45.2 na wanaume 1090 sawa na asiliamia 54.8. 
 Pamoja na changamoto zilizopo, Profesa Itika alisema chuo kimepata mafanikio mengi na kinazidi kuimarisha miradi ya miundombinu yake, rasirimali watu na vitendea kazi kwa kampsi na vituo vyake vyote. 
 Alitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni ufinyu wa bajeti ambao unaathiri uendeshaji wa shughuli za kawaida za chuo na pia shughuli za ukarabati wa miundombinu. Pia kuna uchakavu wa miundombinu ikiwemo mabweni, kumbi za mihadhara, madarasa na nyumba za wafanyakazi na upungufu wa huduma ya maji. 
 Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Profesa Daniel Mkude alisema chuo kitaendelea kutekeleza kwa uadilifu mkubwa sera, mikakati na maelekezo ya serikali ili kiendelee kuwa kitovu cha elimu bora, hasa kuendelea kuweka mkazo katika fani za utawala na menejimenti. Pia aliwapongeza wahitimu kwa kusoma kwa bidii hadi kufikia hatua ya kuhitimu na kuwataka kwenda kuwa mabalozi wazuri wa chuo chao katika kazi. 
 “Mkatumikie vyema stadi mlizopata na epukeni kujitumbukiza katika vitendo vya rushwa, uvivu, uzembe, kufanya kazi kwa mazoea na mkawe mabalozi wetu wazuri,” alisema. 
 Profesa Mkude aliwakumbusha wahitimu hao kufahamu kuwa elimu haina mwisho na kwamba wana wajibu wa kuendelea kusoma machapisho, vitabu na makala mbalimbali ili kuzidi kupata maarifa na kutoa mchango wao kwa jamii.
 Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mkuu mstaafu Barnabas Samatta (katikati) akimtunukia Shahada ya Udaktari wa Falsafa, Bahati Ilembo katika mahafali ya 14 ya Chuo Kikuu Mzumbe mwishoni mwa wiki mjini Morogoro.  Kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho, Profesa Daniel Mkude na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Josephat Itika (kushoto).
 Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mstafu Barnabas Samatta, akimtunukia Shahada ya Udaktari wa Falsafa, Thobias Nsindagi katika mahafali ya 14 ya Chuo hicho mjini Morogoro mwishoni mwa wiki.  Wa pili kushoto ni Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Josephat Itika na Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Profesa George Shumbusho (kushoto).
 Wahitimu wa mahafali ya 14 ya Chuo Kikuu Mzumbe wakifurahia kutunukiwa shahada mbalimbali wakati wa mahafali ya 14 ya Chuo hicho mwishoni mwa wiki mjini Morogoro.
Wahitimu wa mahafali ya 14 ya Chuo Kikuu Mzumbe wakifurahia kutunukiwa shahada mbalimbali wakati wa mahafali ya 14 ya Chuo hicho mwishoni mwa wiki mjini Morogoro.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...