Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Edwin Ngonyani ameitaka Bodi ya Mfuko wa Barabara kutotuma fedha za ujenzi wa barabara kwa halmashauri yoyote nchini ambayo imetumia fedha walizopelekewa kinyume na malengo yaliyokusudiwa. 
Na amemwagiza Meneja wa Bodi ya Mfuko wa Barabara kuzichukulia hatua halmashauri zote ambazo zimetumia fedha hizo tofauti na malengo yake ikiwa ni pamoja na kutopelekewa fedha mpaka hapo watakapozijeresha fedha walizozitumia. 
“Ongezeni nguvu zaidi katika kusimamia matumizi ya fedha za mfuko wa barabara kwa baadhi ya halmashauri ambazo fedha hizo zinatumika kwa shughuli zisizo za barabara”, alisisitiza Mhe. Ngonyani 
Ameyasema hayo wakati alipotembelea ofisi za Bodi ya Mfuko wa Barabara jijini Dar es salaam na kuelekeza Halmashauri zote nchini kutotumia Wahandisi ambao hawajasajiliwa na Bodi ya Wahandisi (ERB), kusimamia miradi katika halmashauri hizo. 
Naye Meneja wa Mfuko wa Barabara Joseph Haule ameelezea mafanikio ya bodi hiyo toka kuanzishwa miaka 15 iliyopita kuwa mapato yameongezeka kutoka sh bilioni 73 mwaka 2005 hadi sh. Bilioni 752. 
“Kutokana na mapato kupanda mtandao wa barabara umeboreshwa kwa kiwango kikubwa kwa kuwa barabara nyingi zimetengenezwa kutokana na fedha hizo”, alisema Meneja Haule. 
Hata hivyo, Bodi imeendelea kuhakikisha kwamba tozo za barabara zinakusanywa kikamilifu na kuwekwa kwenye mfuko. 
Pia imetoa maelekezo kwa taasisi ambazo zinakusanya mapato ya Mfuko kutumia mfumo wa kielektroniki badala ya kupokea fedha taslimu. Meneja Haule amemhakikishia Mhe. Ngonyani kuendelea kuwa na mahusiano mazuri na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Barabara (TANROADS) na Mamlaka za Udhibiti za EWURA na SUMATRA katika upatikanaji wa taarifa juu ya makusanyo ya fedha za Mfuko wa Barabara na kuhakikisha vyanzo vipya vya mapato vinapatikana.
 Aidha Meneja Wa Mfuko wa Bodi hiyo aliiongeza kuwa Bodi itaongeza mkazo katika ufatiliaji wa matumizi ya fedha za mfuko wa barabara ili kodi za wananchi ziweze kutumika kama ilivyo kusudiwa na tayari mfuko huo umeanzisha kitengo cha Tathimini na Ufuatiliaji wa fedha hizo. 
Katika kuhakikisha ufatiliaji na usimamizi wa fedha hizo unatekelezwa Bodi tayari imeshachukua hatua kwa Halmashauri tatu zikiwemo Halmashauri ya Kinondoni, Songea Vijijini na Bukoba vijijini ambazo zimetumia fedha za mfuko wa barabara kinyume na malengo yaliyokusudiwa. 
Bodi ya Mfuko wa Barabara imeanzishwa rasmi kwa lengo la kukusanya mapato, kufuatilia matumizi ya fedha hizo na kugawa fedha kwenye taasisi ambapo asilimia 63 zinapelekwa TANROADS kwa ajili ya matengenezo ya barabara kuu na za mikoa, asilimia 30 katika Halmashauri 166 kwa ajili barabara Halmashauri, na asilimia 7 zinapelekwa Wizara ya Ujenzi.
Meneja wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), Joseph Haule akitoa taarifa ya utendaji kazi wa bodi hiyo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Edwin Ngonyani mara baada ya kutembelea ofisi hizo na kuangalia jinsi inavyofanya kazi, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Edwin Ngonyani akisisitiza umuhimu wa kufatilia fedha za mfuko wa barabara kutumika katika shughuli za barabara kama ilivyopangwa kwa mujibu wa sheria kwa watendaji wa bodi hiyo.
Meneja wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB), Joseph Haule (wa kwanza kulia) pamoja na maafisa wa mfuko huo wakisikiliza kwa makini maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Edwin Ngonyani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...