Na Grace Michael, Kagera
MFUKO
wa Taifa wa Bima ya Afya umesema hautawavumilia watumishi katika
hospitali ya Mkoa wa Kagera wanaojihusisha na vitendo vya kughushi
nyaraka za kuchukulia dawa katika maduka ya dawa na kuusababishia Mfuko
kulipa fedha ambazo hazijatumika kihalali.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Bw. Michael Mhando ameyasema hayo mjini
hapa wakati akizungumza na uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Kagera kabla
ya uzinduzi wa mpango wa Madaktari Bingwa ambao wamepelekwa na Mfuko huo
kutoa huduma kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bw. Michael Mhando
akiongozana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Nasoro Mlambila kukagua
maeneo wanayofanyia kazi madaktari bingwa ambao NHIF imewapeleka katika
Hospitali ya Mkoa wa Kagera.
“Niseme
tu kwamba tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali zikiwemo za kuwaonya kwa
barua na wengine kuwafutia usajili na wengine kuwafikisha mahakamani
watoa huduma ambao wanajihusisha na vitendo vya udanganyifu lakini
niseme kwamba kwa hospitali hii natangaza rasmi kuwa kuanzia sasa naanza
kuchukua hatua kali kwa watumishi ambao watabainika kujihusisha na
udanganyifu wowote,” alisema Bw. Mhando.
Alisema
kuwa Mfuko unalo jukumu la kulinda fedha za wanachama wake na
kuhakikisha zinatumika katika matumizi sahihi hivyo hauko tayari
kuendelea kuvumilia watoa huduma ambao sio waaminifu.
“Nawaomba
sana toeni huduma kwa wanachama wetu na sio kutumia vitambulisho vyao
kughushi nyaraka mbalimbali zikiwemo za kuchukulia dawa katika maduka ya
dawa…sisi tuko tayari kusaidia kituo chochote katika uboreshaji wa
huduma zake ili wananchi wanufaike kwa ujumla na sio kikundi cha watu
wachache,” alisema Bw. Mhando.
Daktari
Bingwa wa Masuala ya Usingizi na Wagonjwa Mahututi Vence Sakwari
akijadili jambo na mwenyeji wake katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera
kabla ya kuanza kutoa huduma kwa wagonjwa wake.
Katika
hatua nyingine aliitaka Hospitali hiyo kuangalia namna ya uboreshaji wa
huduma zake hususan upatikanaji wa dawa ambao umeonekana kuwa tatizo
kubwa linaloikosesha mapato hospitali hiyo.
Alisema
kuwa mpaka sasa Hospitali ya Mkoa wa Kagera imekuwa ikipoteza mapato
mengi kutokana na ukosefu wa dawa na vipimo ambavyo ndivyo vinaingiza
fedha nyingi katika vituo vya kutolea huduma hali ambayo inakwamisha
uboreshaji wa huduma.
Sehemu ya wagonjwa wakisubiri kuelezwa utaratibu wa kuwaona madaktari bingwa waliofika hospitalini hapo.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...