Serikali imedhamiria kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini nchini ili kukuza uchumi wa Taifa, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema kwenye kikao chake na wachimbaji wadogo wa madini kutoka mikoa ya Simiyu na Mara.
Profesa Muhongo alisema sekta ndogo ya madini nchini inao mchango mkubwa kwenye pato la Taifa wa kuondoa umasikini nchini na hivyo Serikali kwa jitihada mbalimbali itahakikisha wachimbaji wadogo wananufaika ipasavyo pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi.
“Tutawakaribisha wachimbaji wakubwa lakini tunataka na nyie wachimbaji wadogo mchangie ukuaji wa uchumi; mchangie upatikanaji wa ajira kwa vijana wetu,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa uchimbaji mdogo wa madini, Serikali imeamua na imedhamiria kuwaheshimu na kuwatambua wachimbaji wadogo.
Waziri Muhongo aliwataka wachimbaji hao kubadilika na sio kuendelea kulalamika badala yake wajitume na kufanya kazi kwa uadilifu huku wakitanguliza suala la uzalendo na pia kuamini kwamba Serikali inayo nia thabiti ya kuwasaidia.
Aliwatoa hofu na kuwahakikishia kuwa Serikali inaendelea na juhudi za kuwatafutia maeneo zaidi ya uchimbaji madini na vilevile soko la uhakika ili kuongeza kipato chao na wakati huo huo kuliingizia taifa mapato zaidi.
"Msiwe na wasiwasi, fanyeni uchimbaji wa uhakika; Serikali hii ni yenu; itawasaidia masuala mbalimbali pamoja na kuwatafutia ruzuku, masoko, mafunzo na pia kuwatafutia maeneo zaidi kwa ajili ya shughuli zenu," alisema.
Aliwataka kuachana na fikra potofu kuwa Serikali haiwajali badala yake waiamini Serikali yao kwamba ipo kwa ajili ya kuwasaidia na huku wakijituma kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uaminifu.
“Matatizo ya zamani ya uchimbaji mdogo tuachane nayo, lazima ulipende taifa lako; huwezi ukawa mchimbaji wa dhahabu ya Tanzania unaipeleka Kenya; halafu inauzwa kama imetoka humo hili ni kosa kubwa,” alisema.
Aliwaasa kuepuka kutorosha madini nje ya nchi; aliongeza kuwa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) limepewa jukumu la kuwatafutia bei ya madini kusudi madini yanayopatikana nchini yauzwe nchini na yanunuliwe hapa hapa; iwe ni malighafi ya Tanzania.
Aidha, Profesa Muhongo alimuagiza Meneja wa Tanesco Kanda ya Ziwa Mhandisi Amos Maganga kutembelea maeneo yote ya wachimbaji wadogo ili kujua mahitaji yao ya umeme pamoja na kutathmini namna ya kuwaunganisha na huduma ya umeme.
Rais wa Wachimbaji wadogo wa Madini Tanzania, John Bina akizungumza wakati wa kikao na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wanne kutoka kushoto).
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akizungumza wakati wa kikao chake na wachimbaji wadogo wa madini, Mkoani Mara.
Professor Muongo. Ni vema uelewe kwamba Tanzania ina sera mbovu na ukiritimba mkubwa na wenye kero nyingi kwa mfanyabiashara mdogo. Ndio maana inawawia vigumu wafanya biashara wadogo kupiga hatua. Nchi jirani na Tanzania hazina sera za-kijinga za kibiashara kama Tanzania. Mpaka sera hizi mbovu mziondoe ndio wafanyabiashara wadogo watathamini kufanya biashara kwa uadilifu. Mimi binafsi siungi mkono tabia ya mtu yeyote kutoroshea mali za Taifa nje ya nchi. Wakati huo huo siafikiani na sera mbovu za madini na biashara hasa zinazokumbatia wazungu na wadosi na kuwanyanyasa wazawa wenye nchi yao. Tuache kasumba ya kukumbatia wadosi na wazungu kama ndio wanaoweza kufanya biashara huku tukiwapa wakati mgumu wazawa wenye nchi yao.
ReplyDelete