Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa akizungumza wakati wa Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Maendeleo. Mkutano huo wa siku mbili umefanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani
Na Mwandishi Maalum, New York
Wanawake na watoto wa kike
wanaelezwa kama kundi ambalo bado
halijanufaika ipasavyo na
matumizi ya Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano ( TEHAMA)
Na kwa sababu hiyo, wito umetolewa kwa nchi Wanahama wa Umoja wa Mataifa, Asasi
za Kiraia naTaasisi za Kimataifa kuhakikisha kwamba panakuwep na mikakati na mipango ya ziada yenye lengo la kupunguza pengo la matumizi ya TEHAMA kati ya
wanawake na wanaume.
Hayo yamejiri wakati wa Mkutano wa siku mbili wa Ngazi ya Juu wa Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa uliokuwa ukitathmini utekelezaji wa Teknolojia
na Habari na Mawasiliano kwa Maendeleo,
ikiwa ni miaka kumi tangu mchakato wa kuhakisha kuwa jamii
inapata fursa ya kupata na
kutumia TEHAMA ambayo itakuwa ni jumuishi na yenye gharama nafuu.
Wajumbe wa mkutano huu walikuwa ni Mawaziri wanaohusika na masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, na Rais wa Baraza kuu la Umoja wa
Mataifa, Bw. Monges Lykketofts ni baadhi ya viongozi wakuu waliozungumza wakati
wa ufunguzi wa mkutano huu.
Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Balozi Tuvako Manongi,
Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika
Umoja wa Mataifa.
Katika hotuba yake mbele
ya wajumbe wa Mkutano, Balozi
Manongi, amesema Serikali inalichukulia
kwa umuhimu wa kipekee suala upatikanaji, uboreshaji, usambazaji na matumizi ya TEHAMA kwa wananchi wake.
Akasema katika kuhakikisha
kuwa TEHAMA inakwenda na wakati na
inawafikia wananchi wengi na kwa gharama nafuu, serikali imekuwa ikishirikiana
na kufanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali wa ndani na nje.
Akasema kama ilivyo kwa
nchi nyingine zinazoendelea, Tanzania ingependa kuona panakuwapo na
ushirikiano zaidi na wenye tija baina ya mataifa yaliyoendelea na yanayoedelea hususani katika eneo la uwezeshawaji wa kiteknolojia,raslimali fedha
na mafunzo.
Balozi Manongi, na kama iliyokuwa
kwa wazungumzaji wengine, amesema ingawa matumizi ya TEHAMA yamekuwa na manufaa
makubwa kwa mwanadamu katika Nyanja mbalimbali, lakini pia pamekuwapo na
changamoto kadhaa zitokanazo na matumizi
mabaya.
Baadhi ya changamoto hizo ni matumizi yasiyo sahihi ya mitandao, ukiwamo uhalifu
wa mitandao , ugaidi, uingiliaji wa
masuala binafsi ya mtu, ukiukwaji wa maadili, usambazaji wa matamshi ya chuki na misimamo mikali.
Akabainisha pia kuwa
pamezuka tabia sugu ( addiction) ya
matumizi ya TEHAMA kiasi cha kudhoofisha
mahusiano miongoni mwa familia na jamii kwa ujumla.
Kama hiyo haitoshi matumizi
sugu ya TEHAMA yamezalisha tatizo
jingine la watu kujikuta wakipata magonjwa yasiyoambukiza kutokana na kwamba
wamekuwa wakitumia muda mwingi kwenye TEHAMA pasipo kuishughulisha miili yao.
Mwakilishi huyo wa Tanzania akasema panahitajika juhudi
za pamoja katika kuzikabili changamoto hizo na nyingine nyingi.
Wazungumzaji wengi
katika mkutano huo pamoja na
kubainisha kuachwa nyuma kwa
wanawake na watoto wakike katiika
matumizi ya TEHAMA, walieleza pia kwamba kundi jingine ambalo nalo
halijanufaika na TEHAMA ni watu wenye ulemavu.
Pia ilielezwa wakati wa
mkutano huo kuwa ingawa asilimia 40
ya idadi ya watu wote duniani wamepata
fursa ya kutumia TEHAMA, bado kuna pengo kubwa baina ya watumiaji kati ya
mataifa yanayoendelea na yale yaliyoendelea.
Halikadhalika imebainishwa
kwamba kuna pengo pia miongoni wa
watumiaji hao kati ya wale wa mijini na vijijini lakini pia uwezo wa kipato
nalo ni tatizo linalosababisha siyo kila mtu anakuwa na uweze wa kumudu gharama
za matumizi ya TEHAMA.
Baadhi ya wazungumzaji
wengine walikwenda mbali Zaidi kwa kueleza kwamba TEHAMA ni muhimu sana kwa utekelezaji wa ajenda mpya ya maendeleo endelevu lakini pia
ni muundombinu muhimu ambao hauna
tofauti na miundombinu mingine kama vile barabara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...