Na Nyakongo Manyama Maelezo
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa tamko kuhusu hali ya ugonjwa wa kipindupindu ulioanza agosti 15 mwaka huu katika mkoa wa Dar es Salaam na kusambaa kwa kasi katika mikoa mingine 20 nchini.
Akitoa tamko hilo mbele ya waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alisema kuwa kwa wastani ugonjwa wa kipindupindu umepungua katika mkoa wa Dar es salaam na kwa mikoa ya iringa na Moshi kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kudhibiti ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa taarifa tarehe 15 Disemba kumekuwa na wagonjwa wapya 141 na kufanya jumla ya wagonjwa waliokuwa wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye vituo vya kutolea huduma katika mikoa yote iliyoathirika kuwa 184 na vifo vipya viwili.
Aidha Waziri Ummy Mwalimu amepiga marufuku uuzaji wa matunda yaliyokatwa na vyakula maeneo ya wazi (barabarani) na watakaokiuka wachukuliwe hatua mara moja ,na kuwataka waganga wakuu na mikoa na wilaya wasimamie utekelezaji wa mikakati yote ya kudhibiti mlipuko huu ikiwa ni pamoja na kusimamia kanuni za afya na kuhakikisha kuwa wanadhibiti ugonjwa huu
“ Nahitaji nipate taarifa ya utekelezaji kila siku kutoka kwa waganga wakuu wa mikoa na wilaya na serikali haitasita kuchukua hatua kwa viongozi ambao watashindwa kudhibiti ugonjwa huu katika maeneo yao” alisema Waziri Ummy.
Pia amewashukuru wadau wa maendeleo kama vile Shirika la Afya Dunia (WHO), CDC,USAID,MSF,Red cross na UNICEF kwa ushiriki wao katika kukabiliana na mlipuko huu na kuwataka wahusika kwenye vyombo vya habari wasaidie kutoa taarifa na kuelimisha jamii kuhusu kipindupindu.
Tangu ugonjwa huu uanzae jumla ya watu 11,257 walipata ugonjwa huu na kati yao jumla ya watu 177 wameshafariki kwa ugonjwa huo ambayo ni sawa na 1.5% ya waliougua, na katika swala la kukabiliana na ugonjwa huu ni muhimu kwa sekta zote husika ikiwemo Maji,Elimu,Mawasiliano,Uchukuzi na Ujenzi hazina budi kushirikiana kwa pamoja kutokomeza ugonjwa huu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Katikati) akielekezwa jambo kuhusu ufanyaji kazi wa mashine za MRI na CT Scan na mtaalam kutoka kitengo hicho Dkt Majid Msemo alipotembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Kulia) Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Ya Muhimbili Prof Lawrence Mseru .
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiangalia mazingira alipotembelea eneo la ubungo Jijini Dare s salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Katikati) akimjulia hali mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika kambi ya kipindupindu iliyopo Mburahati Jijini Dare s salaam. Picha na Raymond Mushumbusi - Maelezo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...