Na Bashir Yakub.
Masuala ya msingi yanayohusu ardhi za vijiji yanasimamiwa na sheria namba 5 ya ardhi za vijiji. Sheria hii ilitungwa mwaka 1999 na kuanza kutumika rasmi Mei 2001. Upo mwamko mkubwa wa wananchi hasa wa maeneo ya mijini na wale walio nje ya nchi wa kununua maeneo ya vijiji kwa ajili ya shughuli mbalimbali za uwekezaji na uchumi kwa ujumla.
Hata hivyo wengi wao wamekumbwa sana na migogoro huko wanakonunua. Sababu za migogoro hii ni nyingi. Lakini mojawapo ni kutokuzingatia mambo ya msingi na ya kisheria wakati wa kupata ardhi hizo.
Nani asiyejua sasa kuwa migogoro baina ya wawekezaji na wanavijiji ni janga,hakika hakuna.
Ni aghalabu kufungulia runinga au redio usisikie mgogoro wa ardhi baina ya wanakijiji na mwekezaji. Ni sababu hii inayopelekea makala haya na makala nyingine zilizopita kueleza japo baadhi ya mambo ya msingi na ya kuzingatia unapoelekea kumiliki ardhi ya kijiji.
1.NANI ANA HAKI YA KUTOA UMILIKI WA ARDHI YA KIJIJI.
Kifungu cha 25 cha sheria ya ardhi ya vijiji kinasema kuwa Halmashauri ya kijiji ndicho chombo chenye mamlaka ya kutoa umiliki wa ardhi ya kijiji. Usikubali kuuziwa ardhi ya kijiji na chombo kingine chochote mbali na chombo hiki.
Wengi wamenunua ardhi kwa kuuziwa na mtendaji kata, sijui mwenyekiti, sijui balozi wa nyumba kumi na hata wengine wameuziwa na watu binafsi. Ardhi ya kjiji hutolewa na halmashauri ya kijiji na hii ni kwa mujibu sheria.
Utakapokuwa umeuziwa na chombo tofauti , tafsiri yake ni kuwa hujanunua umegawa hela. Maana yake ni kuwa muda wowote wanakijiji na serikali yao wataomba kurudushiwa ardhi yao. Umakini unahitajika sana eneo hili kwakuwa wengi wameuziwa na mamlaka/watu ambao hawana uwezo wa kuuza ardhi ya kijiji kisheria. Migogoro mingi ina sura ya mtu kumiliki ardhi katika kijiji huku kijiji kikidai kutomtabua. Sababu ni hii kuuziwa na watu wasio na mamlaka.
2. NI NYARAKA IPI UNAYOIPATA UNAPONUNUA ARDHI YA KIJIJI.
Kipo kitu kinaitwa cheti cha hakimiliki ya kimila( customary right of occupancy). Hiki ndicho kitu kinachotakiwa kutolewa unapokuwa umenunua ardhi ya kijiji. Cheti hiki ndicho nilichosema hapo juu kuwa kinatolewa na halmashauri ya kijiji. Usikubali kuambiwa umenunua ardhi ya kijiji bila kupatiwa cheti hiki. Hii ni kwakuwa uhalali wa umiliki wako unategemea hiki cheti.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...