Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu maafa imeanza mkakati wa menejimenti ya maafa ya ukame kwa kuwawezesha wananchi wanao kabiliwa na njaa kuweza kukabili maafa hayo kwa kuwagawia wananchi hao mbegu bure za mazao yanayohimili ukame katika halmashauri husika.
Kufuatia hali ya ukame ambao umezikumba baadhi ya halimashauri hapa nchini katika msimu wa 2014/2015, baadhi ya halmashauri hizo zilipata upungufu wa chakula hali iliyopelekea halmashauri hizo kuomba chakula cha msaada Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Uratibu maafa.
Akiongea wakati wa ziara ya kukagua hali ya upungufu wa chakula katika kata ya Malengamakali, wilayani Iringa Tarehe 11 Januari, 2016, Mkurugenzi wa Idara ya uratibu maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Mbazi Msuya amebainisha kuwa mkakati uliopo ni kuwahamasisha wananchi walime mazao yanayohimili ukame.
“Nashauri watendaji wakuu wa Halmashauri na mikoa kupitia kamati za maafa waorodheshe wananchi wote wanaohitaji mbegu hizo na kuwasilisha katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu maafa na Ofisi yangu itatuma fedha za kununua mbegu hizo ili zigawiwe bure kwa wananchi wengine wenye upungufu wa chakula, tunahitaji wananchi wote wawe na uhakika wa chakula .” amesema Brig. Jen. Msuya.
Awali akiongea katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Halmashauri ya Iringa, Richard Kasesela, alibainisha kuwa katika kukabiliana na upungufu wa hali ya chakula halmashauri hiyo imefanya uhamasishaji wa kilimo cha zao la Mtama amabalo ni zao linalovumilia ukame na mazao mengine yanayokomaa kwa muda mfupi kama vile viazi vitamu.
“Uhamasishaji umefanyika katika Tarafa za Isimani, Idodi, Pawaga na Kalenga (mfyome), tumeanzisha na sheria ndogo ya kilimo ambayo inaitaka kila kaya kulima mtama ekari mbili katika kata hizi na atakayekiuka sheria hii adhabu yake ni kulipa kiasi cha fedha shilingi 50,000/=” alisisitiza Kasesela.
Katika kukabiliana na upungufu wa chakula Halmashauri ya Iringa iliomba chakula cha msaada kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu Maafa, ikiwa hadi kufikia Disemba 2015, tayari tani 4, 546 zilikuwa zimeletwa wiliyani humo ambazo zimesambazwa katika Kata 11, vijiji 42 katika maeneo yenye upungufu wa chakula.
Mkurugenzi Idara ya Uratibu maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Brig. Jen, Mbazi Msuya akisisitiza umuhimu wa kulima mazao yanayohimili ukame wakati alipotembelea kijiji cha Iguluba, kata ya Malengamakali wilayani Iringa, tarehe 11 Januari, 2016.
Mkazi wa kijiji cha Iguluba, kata ya Malengamakali wilayani Iringa, Alduvina Mchande akieleza hali ya upungufu wa chakula kijijini hapo, wakati Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya uratibu maafa ilipotembelea kijiji hicho kufuatilia hali ya upungufu wa chakula tarehe 11 Januari, 2016.
Mkazi wa kijiji cha Iguluba, kata ya Malengamakali wilayani Iringa, Peter Nyaulingo akiomba Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya uratibu maafa kuwapelekea chakula cha msaada kingine wakati Ofisi hiyo ilipotembelea kijiji hicho kufuatilia hali ya upungufu wa chakula tarehe 11 Januari, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...