Waziri
wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Mpango (kushoto) akiongea na waandishi wa
habari (hawamo pichani)jijini Dar es Salaam, kuhusu hatua zilizochukuliwa na
Serikali dhidi ya Benki ya Stanbic Tanzania kutokana na ushiriki wake katika kuwezesha
mkopo wa Serikali wa Dola za Kimarekani Milioni 600 na Kulia kwake ni Naibu Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania(BOT) Bw. Lila
Mkila.
Utangulizi
1. Mwezi
Julai 2013, Benki Kuu ya Tanzania kupitia ufuatiliaji wa kawaida wa shughuli za
mabenki iligundua matatizo yaliyohusiana na hasara itokanayo na mikopo na pia
kuacha na kuondolewa kazini kwa viongozi waandamizi wa Stanbic Bank Tanzania
Limited (Stanbic) katika muda mfupi. Kutokana na hilo, Benki Kuu iliamua
kufanya ukaguzi wa kulenga (Targeted Examination) katika benki hiyo. Ukaguzi
huo ni kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa Benki Kuu chini ya Kifungu 47 cha Sheria
ya Benki Kuu ya mwaka 2006 na Kifungu 31 cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za
Fedha ya mwaka 2006.
Matokeo
ya Ukaguzi wa Benki Kuu
2. Katika
ukaguzi huo, wakaguzi wa Benki Kuu, pamoja na mambo mengine walibaini miamala
ya kutia shaka iliyohusu malipo kwa kampuni ya kitanzania ya Enterprise Growth
Market Advisors (EGMA). Kampuni ya EGMA ilihusika katika uwezeshaji wa upatikanaji
wa Mkopo kwa Serikali ya Tanzania ambapo Standard Bank Plc (ambayo kwa sasa
inajulikana kama ICBC Standard Bank) na Stanbic Bank Tanzania Limited kwa
pamoja walikuwa “Mwezeshaji Mkuu” (Lead Arranger). Malipo hayo kwa kampuni ya
EGMA yalikuwa yamefanyika kinyume na taratibu za kibenki na yalihusisha uongozi
wa benki ya Stanbic. Jumla ya malipo yalikuwa ni kiasi cha dola za kimarekani
milioni 6, na zililipwa katika akaunti ya EGMA na kutolewa kwa muda mfupi kwa
njia ya fedha taslimu (cash) ambayo ni nje ya taratibu za kibenki.
3. Taarifa
ya ukaguzi huo iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic kwa mujibu wa taratibu, na Benki
Kuu iliiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo kuchukua hatua stahiki za
kurekebisha kasoro zilizoonekana. Aidha, benki ya Stanbic iliagizwa kutoa
taarifa kwa Kitengo cha Financial Intelligence Unit (FIU) kilichopo Wizara ya
Fedha na Mipango kuhusiana na miamala hiyo yenye mashaka katika akaunti ya EGMA
kama Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu ya mwaka 2006 (The Anti-Money
Laundering Act, 2006) inavyoelekeza. Benki ya Stanbic ilitekeleza maagizo na
kutoa taarifa FIU kuhusu miamala inayotiliwa shaka.
4. Mnamo
29 Septemba 2015, Benki Kuu ilipokea barua toka Idara ya Serikali ya Uingereza
inayohusika na Upelelezi wa Makosa ya Kugushi na Rushwa (Serious Fraud Office -
SFO) ikiiomba Benki Kuu ruhusa ya kutumia ripoti yake ya ukaguzi kama ushahidi
katika kesi dhidi ya Standard Bank Plc ambayo ilikuwa ni mshirika wa Stanbic
Bank Tanzania Limited katika kuwezesha mkopo wa dola za kimarekani milioni 600
kwa Serikali na kwamba ripoti hiyo ingekuwa wazi kwa umma. Benki Kuu iliijibu
SFO kuwa kwa mujibu wa Sheria ripoti za Benki Kuu zinatolewa tu kwa benki au
taasisi ya fedha inayohusika, hata hivyo, Benki Kuu haikuwa na pingamizi kwa SFO kutumia taarifa za ripoti hiyo kwa
kuzingatia chanzo cha ripoti hiyo.
5. Hatimaye,
Standard Bank Plc ilikubali makosa na ilitozwa faini ya jumla ya dola za
kimarekani milioni 32.20, ambapo kiasi cha dola za kimarekani milioni 7
zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania (dola za kimarekani milioni 6 zilikuwa ni
fidia na dola za kimarekani milioni 1 ni riba).
6. Kwa
kuzingatia mapungufu ya kufanya miamala iliyohusisha EGMA na pia kutokuweka
taratibu madhubuti za udhibiti wa ndani, na kwa kuzingatia Kifungu 67 cha
Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu imeiandikia benki
ya Stanbic barua ya kusudio la kuitoza faini ya shilingi bilioni 3. Sheria inaitaka
benki ya Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha siku ishirini (20) ambacho
kitaisha tarehe 30 Januari 2016. Endapo
Benki Kuu haitaridhika na utetezi, benki ya Stanbic italazimika kulipa faini
hiyo.
Hitimisho
7. Benki
Kuu imechukua hatua hizo kama onyo kwa benki ya Stanbic na ili iweze kuwa
makini katika kuhakikisha kuwa shughuli zake zinaendeshwa kwa mujibu wa
taratibu za kibenki na kuzingatia Sheria.
8. Aidha,
hatua hii ni onyo kwa mabenki na taasisi za fedha zisijihusishe na makosa ya
aina hii ambayo ni kinyume cha taratibu za kibenki na ni uvunjaji wa Sheria za
nchi. Hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa benki au taasisi ya fedha yoyote
itakayobainika kwenda kinyume na taratibu za kibenki na Sheria ya Mabenki na
Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.




Sawa Egma vipi? au wao wako sawa kwa mgao huo
ReplyDeleteOnyo onyo onyo, na issue ya escrow je? Fungia tu ili muonyeshe hapo kazi tu
ReplyDeleteHawa walilala usingizi wa pono.
ReplyDeletekwanini bot hawakuchukua hatua toka mwaka 2013 mpaka leo hii?
Stanbic wasingebanwa na waingereza na taarifa za kubanwa huko zisingetangazwa na waingereza bila shaka bot wasingechukua hatua yoyote ile.
1. Bado hatua dhidi ya STANBIC (na benki zingine)kwenye skandali ya ESCROW na kuhusika kwake kwenye utakasaji pesa
ReplyDelete2. Bado hatua ya dhidi ya Federal Bank of the Middle East na utaksaji pesa.
3. Hatua hii dhidi ya STANBIC ni ya upole mno maana ni wavunja sheria na kanuni wazoefu na kwa namna mbalimbali- k.m kutakasa pesa na kukwepesaha kodi (haikukata withholding tax kwenye skandali za ESCROW na hii ya EUROBOND.
4. Serikali iliwakumbatia makaburu kama ndugu zao. Siyo ndugu, Kaburu matata!
Kwa hio hatua gani zitachukuliwa dhidi ya Bw Harry Kitisa na wenzake wanaomiliki EGMA? au wameachwa scot free?
ReplyDeleteStanbic Tanzania walipata $4.1 million as fee income kutoka dili hiyo. Binafsi nigependa faini ingekuwa zaidi ya TSh 3 bilioni [$1.35 milioni].