Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe (MB) ameitaka Bodi ya Utalii Tanzania- TTB kuendelea kutumia vyombo vya habari vya Kimataifa kama vile CNN, BBC n.k kuitangaza Tanzania kama eneo la Utalii duniani sambasamba na kuweka makala na matangazo ya utalii wetu katika majarida ya Kimataifa yanayoandika habari za Utalii na usafiri (Travel Magazine) ambayo ndiyo husomwa na watalii wengi duniani.

 “Kama kweli tunataka kupata watalii wengi zaidi pamoja na mambo mengine ni lazima tutumie vyombo vikubwa vya Kimataifa vinavyofikia watu wengi zaidi duniani” alisema na kuongeza kuwa pamoja na njia nyingine zinazotumiwa katika kuitangaza Tanzania kimataifa, mbinu hii ya kutumia vyombo vya habari yaweza kuwa na ufanisi mkubwa zaidi .

Waziri Maghembe ameyasema hayo leo alipotembelea Bodi ya Utalii Tanzania na kukutana na Menejimenti  ya TTB kwa lengo la kujitambulisha na kubadilishana mawazo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Bodi katika utangazaji utalii ndani na nje ya nchi.

Akizungumzia kuhusu madeni makubwa yanayoikabili TTB,  Mh. Profesa Jumanne Maghembe ameahidi kuwa Wizara yake itachukua madeni yanayoikabili TTB na hasa yaliliyotokana na maelekezo ya Wizara ya kama yale yaliyotokana na kuitaka Bodi iingie mikataba ya kuweka matangazo katika ligi kuu ya Uingereza na klabu za mpira wa mguu na Sunderland Football Association pia ya nchini Uingereza. 

Amesema Wizara ni lazima ilipe madeni hayo ili kulinda taswira ya Bodi ya Utalii kwa wadau na kuiondolea Bodi mzigo wa kuhangaikia madeni hayo badala yake ijikite zaidi katika kutangaza utalii.Kuhusu ukuzaji na uendelezaji wa utalii nchini Profesa Maghembe amebainisha kuwa pamoja na uwepo wa mashirika mbalimbali ya ndege yanayokuja hapa nchini lakini kuna haja kubwa Tanzania kuwa na shirika lake imara la ndege ambalo litasaidia sana kukuza utalii nchini kama ilivyo kwa nchi nyingine kama Kenya na Afrka ya Kusini. 

Aidha amesema kuna haja pia ya kuboresha na kuendeleza zaidi  vivutio vyetu vya utalii na mazao mengine ya utalii kama vile Utalii wa fukwe na  Utalii wa utamaduni sambasamba na kukamilisha zoezi la uwekaji madaraja hoteli zetu na kutoa elimu kwa wenye hoteli kuboresha zaidi hoteli zao na hudiuma watoazo.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na viongozi wengine kutoka Wizarani akiwemo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Bw. Ramo Makani, Naibu katibu Mkuu Bi Angelina Madata na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii Bw. Zahoro, Waziri Maghembe amesema anataka kuona idadi ya watalii ikiongezeka kutoka 1,100,000 ya sasa na kufikia Milioni 3,000,000  mwaka 2018.

Mapema kabla ya kumkaribisha waziri kuzungumza na Menejimenti, Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Bi Devota Mdachi alimwelezea Mh. Waziri mafanikio kadhaa ambayo Bodi imeyapata ikiwa ni pamoja na kuanzisha onesho la Utalii la Kimataifa la Swahili Swahili International Tourism Expo (S!TE) linalofanyika kila mwaka jijini Dar es salaam, kuanzishwa kwa tovuti maalumu (Portal) ya kuitangaza Tanzania na kulipia huduma nyingine za utalii moja kwa moja , uwekaji wa matangazo sehemu mbalimbali duniani.  

Bi Devota alimfahamisha pia Mh. Waziri kuwa TTB imechaguliwa kuwa miongoni mwa Bodi za Utalii tatu bora barani Afrika ambazo zinashindanishwa kumpata mshindi wa kwanza na wa pili. “Mh. Waziri, pamoja na matatizo mengi yanayoikabili TTB lakini tunafurahi kukujulisha kuwa TTB ni miongoni mwa bodi za utalii tatu zilizoingia katika hatua ya mwisho ya kutafuta mshindi wa Bodi ya Utalii borani Afrika tukishindana na Bodi za utalii za Afrika ya Kusini na Namibia katika shindano linaoendeshwa na taasisi ya Travvy ya Marekani” alidokeza Bi Mdachi.

Kaimu Mkurugenzi  huyo alidokeza pia kuhusu changamoto kadhaa zinazoikabili Bodi kubwa zaidi ikiwa ni madeni makubwa ya nje na ndani, na bajeti ndogo ya utangazaji. 
 Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Profesa Jumanne Maghembe akizungumza na Menejimenti ya Bodi ya Utalii leo jijini Dar es salaam.
 Kamimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania Bi Devota Mdachi akitoa taarifa ya masuala mbalimbali yahusuyo Bodi yake mbele ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Profesa Jumanne Maghembe wakati wa mkutano na Menejimenti ya TTB leo. Kulia kwa Bi Devota ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bibi Agelina Madata.
Wajumbe wa Menejimenti ya TTB wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Bw. Ramo Makani  (wa pili kulia katika meza kuu) leo  jijini Dar es salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 9 mpaka sasa

  1. Waziri mtaalam wa misitu,Naibu waziri injinia,Katibu mkuu..Afande..unatraji utalii uongezeke kwa miujiza?

    ReplyDelete
  2. Muheshimiwa Rais JPM tenganisha utalii na Maliasili tafadhali,ili utalii uongezeke na maliasili iwe chini ya wizara ya mazingira.Ili hotel,restaurant,travel com,tour operators wakaguliwe na kupewa viwango ya ufanisi sasa hivi waizara iko busy kutoa vibali ya miti tu

    ReplyDelete
  3. TTB inapasa kuvunjwa na kuwa chini ya wizara kama moja ya idara ya kutangaza utalii nje na ndani,kuwa board pembeni ni upotezaji fedha za umma na kazi wanazofanya zinajirudia na wadau wengine.Wizara ya utalii itapunguza marudio ya kazi muhimu.

    ReplyDelete
  4. Youtube ipo buree, mpate wataalamu wa kufanya video clip nzuri za ubora mkubwa kuanzia muonekana, mawasilisho na sauti nzuri.

    ReplyDelete
  5. Kwani ela wanayopata kupitia watalii haitoshi kulipia madeni mpaka yalipwe na serikali? Sasa hiyo ni biashara gani!

    ReplyDelete
  6. Anonymous wa January 06,2016.

    Jaribu kabla ya kutoa maoni yako kufikiria kile unachotaka kukiandika. Tunaelewa watanzania wengi wanapenda kukosoa serikali bila ya kuwa na tafiti au weledi wa kile wanachokikosoa. Unasema waziri wa utalii ni mtaalamu wa misitu sasa bila ya misitu na wanyama pori huo utalii ungekuwepo? Au naibu waziri wake ni injinia wewe kwako umeona kicheko usiojua maana.sasa bila wa yakuwa na miundo mbinu ya uhakika huo utalii utafanyika vipi? Lazima mtaalam wa miundo mbinu wa uhakika atakae hakikisha hao watalii wanatembelea sehemu za vivutio vya nchi bila usumbufu wowote. Na mwisho kuhusu kuwepo kwa katibu mkuu afande. Wewe umeona ni kitu cha kubeza . Ndio maana baadhi ya watu hawana hata haja ya kupoteza muda wao kuangalia mitandao kutokana na wanamichepuko ya aina mchangiaji ninae mzungumza hapa. Watalii wote wanaokuja Tanzania naweza kusema asilimia 95% wanakuja kuangalia wanyama pori. Na tunaelewa jinsi gani wanyama pori hao wanavyo ishi na hali tete ya kuangamizwa na majangiri na wahalifu wengine kila kukicha sasa bila ya kuwa na wataalam wa kweli katika masuala ya ulinzi kutakuwa na myama atakae atakaebakia kweli?
    Je vipi kuhusu usalama wa hao watalii wenyewe wanapokuwepo huko porini?
    Watanzania tuache kutoa maoni pumba yalioambataba na siasa za majitaka. Ukiangalia utaona jinsi gani magufuli alivokuwa makini katika kazi yake.

    ReplyDelete
  7. Kuna uhuru wa mawazo na wa kuongea pia,swala la kukosoa ni sehemu ya kujifunza na kurekebisha ukiona inafaa.Kuhusu utaalam wa waziri wa misitu,nafikiri ujawahi sikia kuna shahada za utalii na uongozi wake.Misitu sio ndio sababu pekee ya kumfanya aongoze utalii.Injinia alitakiwa wizara ya miundo mbinu bora mtu mwenye shahada za biashara ili kuongeza ufanisi ktk biashara ya utalii,na katimu mjeshi,kama utafuatilia shirika la hifadhi za taifa (TANAPA)kwa sasa imekuwa ktk mfumo wa kijeshi nafikiri pale ndio huyu meja jeneral alitakiwa kuongoza,maana shirika lilipoteza malengo yake kwa muda mrefu na wanyama walipote ktk mikono yao.Utalii unahitaji marketing strategy,branding na vitengo vya kuvutia utalii kwa njia tofauti michezo,mikutano,matamasha na kila aina ya njia ili wageni waje.Kwa ufupi tu nchi kama Tunisia au kenya wanatupita kwa idadi ya watalii wakati sisi tunaongza kwa vivutio vya utalii Africa.Ktk seven wonder za Africa Tatu ziko Tanzania lakini sisi bado utalii tunaona ni wizara ya kuunganishwa na upandaji miti

    ReplyDelete
  8. Kama kuna uhuru wa mawazo na kuongea ndio maana mkosoaji kajibiwa. Unasema labda sijawahi kusikia kama kuna shahada ya utalii na uongozi wake. Unauhakika gani na taaluma yangu katika masuala ya utalii? Hiyo mihemko ya kujiropokea vitu usivyovijua mwanzo wala mwisho wake ni kwa watu walio na tabia ya uwongo. Tourism and hotel management is my professional. Na ndio maana najaribu kukufahamisha ya kuwa nchi yeyote duniani yenye viongozi wenye kujitambua wanapoamua kuingia katika biashara ya utalii hawaangalii utalii pekee yake kama unavyouangalia wewe yaani uwe na watu wenye taaluma ya utalii tu la hasha. Tourism industry ni taasisi pana sana hasa kama nchi husika imeamua kuufanya utalii kuwa moja ya nguzo muhimu ya pato lake la taifa kwani kuna changamoto nyuni sana ndani yake. Sielewi kiwango cha elimu yako lakini aliesoma kasoma na muheshimiwa Magufuli ni msomi wa kiwango cha juu kabisa nna uhakika anajua nini anachokifanya kwa manufaa ya Taifa. Wizara au taasisi inayojihusisha na utalii wa nchi mara nyingi inaundwa na wataalam wa taaluma mbali mbali ili kudhibiti athari zinazoweza kujitokeza katika biashara ya utalii ili utalii huo uwe na tija na taifa. Kusema wakenya wanatupita kiutalii? Idadi ya watalii wengi wasioiingizia nchi mapato stahiki ni upuuzi mtupu. Wakenya wameibinafsisha nchi yao kwa asilimia kubwa, serikali ya kenya na watu wake wananufaika kwa kiwango kidogo sana. makampuni mengi ya utalii ni ya kigeni watalii wengi wanaingia kenya wanakuwa wameshalipia huko wanakotoka na kuikosesha serikali ya kenya mabilioni ya pesa. Kama utalii ungelikuwa na maslahi stahiki kwa wananchi wa kenya na serikali yake kutokana na idadi ya watalii wanaoingia kenya kama unavyoelezea basi usingekuja kumuona mkenya hata mmoja akija kuhangaika hapo Tanzania.

    ReplyDelete
  9. NashuKuru mdau kwa mchango wako nimezungumzia vitu vingi sana,naona umesimama ktk kumtetea Rais,yeye ni binadamu na anahitaji michango yetu ili aweze kufanya uhamuzi stahiki.Elimu ya Rais inatambulika na wala sio mjadala hapa,ila wizara ya sheria badala ya mwanasheria unamuweka daktari wa watu sio sawa,Swala tufocus jambo muhimu ktk wizara husika,Hiyo elimu yako ya tourism na hospitality management ya kiwango gani?Nilitoa mfano wa Kenya na Tunisia,umefocus kwenye kenya tu,Hivi unatambua vinara wa biashara ya utalii kwa Tanzania?na mapato yanayopote kwa kuwa hao ndio wamiliki wa makampuni hayo?kama ulitambui nitakufahamisha,hizo leankeage hapo nyumbani zipo sana,ingawaje mbuga zetu ni za Taifa lakini mahotel ni ya binafsi na mtalii anapokuwa hotel ndio anatumia sana pesa,serikali yenye malengo ilitakiwa kuwa ktk PPPPublic private sector partnership) investments in tourism ili
    kuzuia pesa kutoka nje.Kwa kufikiri unahitaji watu tofauti hilo ni jambo la kawaida ila wakuu lazima wawe na taaluma husika.Nimekupa mfano wizara ya katba na sheria usio mpa mwanasheria utapotea tu.Muhimu kutambua utalii pekee ni mpana sana na una vitu vingi kufikia kiwango cha kimataifa,kama tuna lengo la kuvuka idadi za namba za watalii wa sasa.Mdau na taaluma yako ya utalii unaona sawa wizara kuongoswa na viongozi walio nje ya taaluma husika.Labda kama una maslahi unayapata na system ya sasa kwa maana utalii hauwezi kusonga kwa kupeleka focus ktk miti instead of inspecting hotels na tour companies ambazo nyingi ni fake ambazo hazina viwango.Nimeshuhudia uzembe huo kwa baadhi ya watalii kuachwa bandarini.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...