Kampuni ya Koyo Corporation ya nchini Japan imeonesha nia ya kuwekeza nchini katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia.
Hayo yameelezwa jana jijini Dar es Salaam katika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini kwenye kikao cha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Noria Shoji ambaye alifika wizarani hapo na ujumbe wake ili kujadili fursa za uwekezaji nchini hususan katika ufuaji umeme kwa gesi asilia.
Waziri Muhongo aliueleza ujumbe huo kwamba fursa za uwekezaji kwenye nishati hususan katika uzalishaji umeme kwa kutumia gesi asilia ni nyingi na hivyo Serikali inakaribisha wawekezaji wa ndani na nje.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akimsikiliza Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Koyo Corporation ya Japan, Norio Shoji wakati wa kikao cha kujadili fursa za uwekezaji nchini.
Alisema wawekezaji wanakaribishwa kujenga mitambo ya kufua umeme kwenye maeneo mbalimbali ambapo kuna matoleo ya gesi asilia na huku akiyataja maeneo hayo kuwa ni Mtwara, Lindi, Somangafungu na Mkuranga.
Waziri Muhongo alisema gesi asilia iliyogundulika ni ya kutosha kuzalisha umeme mwingi na hivyo wawekezaji wenye nia ya kuwekeza kwenye ufuaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia wanakaribishwa.
Awali, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo ya Koyo, Norio Shoji alisema lengo la ujio wake na ujumbe alioongozana nao, ni kutafuta ukweli wa mambo kuhusiana na masuala ya uwekezaji kwenye uzalishaji umeme kwa kutumia gesi asilia.
Wajumbe wa mkutano baina ya Wizara ya Nishati na Madini na Kampuni ya Koyo Corporation ya Japan ukiongozwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...