Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka watendaji wa Shirika la Reli nchini (TRL) na Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (RAHCO) kuhakikisha sehemu ya reli iliyosombwa na mafuriko wilayani Kilosa mkoani Morogoro inaunganishwa ndani ya siku tatu na huduma za treni kurejea.
Prof. Mbarawa amesema hayo baada ya kukagua sehemu ya reli hiyo kutoka Kilosa hadi Magulu- Kidete kuona athari zilizosababishwa na mafuriko yaliotokana na mvua zilizonyesha katika mikoa ya Iringa na Dodoma.
“ Fanyeni kazi usiku na mchana ili ikifika alhamisi mawasiliano ya reli kati ya mkoa wa Morogoro na Dodoma yawe yamerejea na abiria waendelee kupata huduma ya treni ,” amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amewahakikishia wananchi wa vijiji vya Munisagara, Mkadage, Mzaganza, Magulu na Kidete ambao usafiri wao pekee wa uhakiki ni wa kutumia reli watoe ushirikiano kwa serikali ili ukarabati na ujenzi wa reli hiyo ukamilike kwa haraka.
Amewataka wananchi waishio pembezoni mwa reli katika wilaya ya Kilosa kupanda miti ili kuzuia mmomonyoko wa udongo unaosababisha mafuriko kwa urahisi wakati wa mvua na kubomoa reli kila wakati.
“Pandeni miti, lindeni miundombinu ya reli na acheni vitendo vya uharibifu wa mazingira ili ujenzi wa mwaka huu uwe wa kudumu na reli isiathiriwe kirahisi na kuwasababishia kero wananchi,” amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Naye Diwani wa kata ya Kidete Bw. Mohamed Seleman Mbunda amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa wananchi wake watashirikiana na serikali kulinda mazingira ili kudhibiti mafuriko yanayoharibu miundombinu ya reli kila wakati wilayani humo.
Mafuriko wilayani Kilosa ni matokeo ya mvua zinazonyesha katika mikoa ya Iringa na Dodoma ambayo husababisha maji ya mto mkondoa kuacha mkondo wake na kubomoa tuta la reli katika eneo la Msagali hadi Kilosa kila wakati.
Mvua za hivi karibuni zilizonyesha mkoani Iringa na Dodoma zimesomba reli katika eneo la Magulu-Kidete kilomita 315 kutoka Dar es Salaam na kukata mawasiliano ya reli kwa siku tatu sasa.
Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amewataka watendaji wa TRL na RAHCO kutafuta suluhisho la kudumu katika madaraja 32 yaliyo katika mtandao wa reli ya kati ili yasiathiriwe na mvua wakati wote.
Waziri wa ujenzi, uchukuzi na
mawasiliano Profesa, Makame Mbarawa wa kwanza (kushoto), akitoa maelekezo kwa
viongozi wa shirika la reli Tanzania TRL na kampuni hodhi ya mali za reli RAHCO kuhusiana na ujenzi wa
reli
Sehemu ya tuta la reli lililosombwa
na maji katika kijiji cha magulu kama inavyoonekana kwa upande wa chini.
Sehemu ya tuta la reli lililosombwa
na maji katika kijiji cha Magulu
Waziri wa ujenzi, uchukuzi na
mawasiliano Profesa, Makame Mbarawa akipanda kiberenge tayari kwa ukaguzi wa
sehemu ya reli iliyosombwa na maji wilayani Kilosa.
Athari ya maji kijijini Magulu
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...