Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema ujenzi wa barabara
za mzunguko (ring roads) zenye lengo la kupunguza msongamano wa magari katikati
ya jiji la Dar es Salaam utakamilika baadae Mwezi Juni mwaka huu.
Amesema
kufuatia Serikali kuanza kulipa madeni ya makandarasi amewataka makandarasi
wote kurudi kazini ili kufikia lengo la Serikali la kukamilisha barabara hizo
mwezi juni sambamba na ulipaji wa madeni yote.
“Tunawaomba
wale wenye nyumba pembeni mwa barabara za mzunguko ambao wapo kwenye orodha ya
kulipwa fidia waondoke maeneo hayo ili kuruhusu kazi ya ujenzi wa barabara
kuendelea”, amefafanua Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri
Prof. Mbarawa amekagua barabara za Tankibovu - Goba (km9), Goba – Mbezi Mwisho
(Km7), Kimara Baruti – Msewe - Chuo Kikuu (km2.6), Mbezi Mwisho – Malambamawili
– Kifuru - Kinyerezi (km14), na Tabata Dampo - Kigogo (km1.6).
Barabara
hizo zenye urefu wa Km 27.2 zimejengwa kwa gharama ya takriban sh. bilioni 56.3
ikiwa ni gharama za ujenzi na fidia ambazo zote zinalipwa na fedha za mfuko wa
barabara.
Kwa
upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Eng. Patrick
Mfugale amewataka madereva kulinda barabara hizo kwa kutoegesha magari katika
maeneo yasiyoruhusiwa na kukemea vitendo vya uchimbaji mchanga pembeni mwa
madaraja.
Waziri
Prof. Mbarawa pia amekagua ujenzi wa daraja la Kinyerezi lenye urefu wa mita 40
lililojengwa kwa gharama ya sh. Bilioni 2.3 ambao ujenzi wake umekamilika.
Barabara
za mzunguko jijini Dar es Salaam zinajengwa kwa kiwango cha lami ili kuvutia
magari mengi kutumia barabara hizo na kupunguza msongamano katikati ya jiji ambapo
hadi sasa Km 27 zimekamilika na Km 28 zinaedelea kujengwa.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (wa pili kulia), akimsikiliza
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Patrick Mfugale (wa
tatu kulia), huku Meneja wa TANROADS mkoa wa Dar es Salaam Eng. Julius
Ndyamukama akifatatilia maelezo hayo.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akifafanua hatua za
Serikali za kuhakikisha ujenzi wa barabara za mzunguko jijini Dar es Salaam
unakamilika mwezi juni mwaka huu.
Meneja
wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Dar es Salaam Eng. Julius
Ndyamukama akitoa taarifa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof.
Makame Mbarawa ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Kimara - Baruti – Msewe – Chuo
Kikuu yenye urefu wa Km 2.6.
Muonekano
wa daraja la kinyerezi lenye urefu wa mita 40 ambao ujenzi wake umekamilika
Muonekano
wa Barabara ya Tankibovu-Goba inayojengwa kwa kiwango cha Lami kama ilivyokutwa
leo mchana.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...