Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotion Bw. Alex Msama akiwafafanulia jambo waandishi wa habari wakati alipozungumzia maandalizi ya tamasha hilo jijini Dar es salaam leo.
…………………………………………
 
WADAU wa muziki wa injili wa jijini Dar es Salaam wameingiwa na hofu juu ya Tamasha la Pasaka kama mwaka huu litafanyika ama litaishia mikoani kwa mara ya kwanza katika historia yake tangu lianzishwe mwaka 2000.
 
Hofu ya wadau hao Tamasha hilo inatokana na hatua ya waratibu wake Kampuni ya Msama Promotions ya jijini Dar es Salaam kuitaja  mikoa ya Geita,Mwanza na  Shinyanga pekee, hivyo wapenzi na mashabiki wa jijini Dar es Salaam kuhoji kulikoni.
 
Akizungumza jana , Anastazia Ferdinand Malinza wa Machimbo, Temeke jijini Dar es Salaam, alisema ameshtushwa kuona waratibu wanataja tamasha hilo mikoani tu na kujiuliza kuna kitu gani kimetokea.

 “Kwa miaka mingi tumezoea liwe Tamasha la Pasaka au Krismasi, limekuwa likianzia jijini Dar es Salaam ndipo liende kwingineko mikoani kulingana na uwezo wa waratibu, lakini safari hii tunasikia tu Geita, Mwanza na Wilaya ya Kahama mkoani Shiny
anga,” alisema Annastazia.

 Alisema akiwa mpenzi na shabiki wa tamasha hilo ambalo limekuwa likifanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee kwa miaka mingi na baadaye kuhamia uwanja wa Taifa kwa miaka ya hivi karibuni, kama litafanyika mikoani tu, wao wa Dar es Salaam watakuwa hawajatendewa haki.
 
“Kama Msama na Kamati yake wataamua tamasha hilo lifanyike mikoani tu, jamani watakuwa hawajatutendea haki kabisa kwa sababu ni tukio ambalo tumelizoea kila mwaka tumekuwa tukienda kupata baraka na watoto wetu,” alisema.
 
Alisema kama kweli Tamasha hilo halitafanyika jijini Dar es Salaam, litakuwa ni pigo kwa wapendwa ambao mara zote wamekuwa wakiliunga mkono tukio hilo ambalo mbali ya kubeba ujumbe wa neno la Mungu, pia kuyafariji makundi maalum.
 
Akizungumza  kwa njia ya simu jana kuhusu maoni hayo, Msama alisema ni kweli Tamasha hilo limekuwa likianzia jiji Dar es Salaam kila mwaka kabla ya kwenda mikoani, lakini mwaka huu wamepanga lifanyike mikoani tu kutokana na sababu maalumu.
 
Alisema, sababu ya kuifanya hivyo ni kutokana na matamasha mengi kufanyika jijini Dar es Salaam, hivyo mpango uliopo ni kuhamia mikoani kwa miaka mitatu mfululizo na kuwataka wadau wa mikoani kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...