Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi bin Ally leo ameruhusiwa kutoka katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Muhimbili ambako alikuwa amelazwa baada ya kufanyiwa upasuaji. 
Sheikh Abubakar ameishukuru Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na taasisi hiyo kwa kumpatia huduma nzuri za matibabu na kwamba afya yake hivi sasa imeimarika. Pia, amemshukuru Rais John Pombe Magufuli, Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kwa kufuatilia afya yake kwa karibu, viongozi mbalimbali na watu wengine waliofika kumjulia hali hospitalini hapo. 
“Siwezi kuwasahau madaktari walionipatia matibabu akiwamo Dk Mwanga, Dk Juma Mfinanga ambaye ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya moyo, Profesa Mohamed Janabi na wauguzi kwa kunipatia matibabu mazuri,” amesema Sheikh Abubakar wakati akizungumza katika hospitali hiyo. 
Katika hatua nyingine, Sheikh Abubakar amemuomba Rais Magufuli kuwatazama madaktari wa hospitali hiyo na kuwaongezea vitendea kazi zaidi ili waendelee kutoa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa. 
“Mwanzo nilikuwa siiamini hospitali hii kama ingeliweza kunipatia matibabu bora, lakini madaktari walinihakikishia watanitibu vizuri na kweli sasa afya yangu imeimarika. Kumbe tunaweza kutibiwa vizuri katika hospitali zetu za hapa nyumbani. 
"Kwa kuwa nilikuwa siiamini hospitali zetu mpaka leo nina tiketi ya ndege ambayo nilikuwa nimekata ili nikatibiwe nje ya nchi, lakini baada ya matibabu nimepata imani na hospitali zetu na kumbe Watanzania wanaweza kutibiwa hapa nyumbani badala ya kwenda nje ya nchi", alisema.
Naye Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kwamba serikali itaendelea kufuatilia afya ya sheikh huyo baada ya kuruhusiwa kurejea nyumbani. “Napenda kuwaahidi kwamba tutaendelea kufuatilia afya ya Sheikh Abubakar lengo kubwa ni kuhakikisha kwamba mambo yanakwenda vizuri,” amesema Ummy Mwalimu. 
Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akimualika Mufti Mkuu Sheikh Abubakar Zuberi bin Ally kuongea na wanahabari katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya madaktari kumruhusu kurejea nyumbani baada ya afya yake kuimarika.
Mufti Mkuu Sheikh Abubakar Zuberi bin Ally akizungumza na waandishi wa habari leo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya madaktari kumruhusu kurejea nyumbani baada ya afya yake kuimarika.

Masheikh wakiwashukuru madaktari bingwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI iliyopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya madaktari kumruhusu Mufti Mkuu Sheikh Abubakar Zuberi bin Allykurejea nyumbani baada ya afya yake kuimarika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Mungu azidi kukupa nguvu na uzima. Mufti mkuu wa Tanzania. Shehe Abubakari Zuberi uendelee kumtumikia mungu na umma wa waumini Tanzania

    ReplyDelete
  2. Ninakutakia afya njema, ninapendezwa sana na matamko ya Mufti kuhusu huduma zaafyahapa nyumbani. Ninakuomba Mufti na watendaji wengine tuiombee kheri nchi yetu na mafanikio makubwa na tuzidi kusonga mbele kwenye huduma hii na pia nyingine zote, including amani na upendo bila ukabila wala udini.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...