JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 

KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Richard Sezibera Ikulu Jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo mengine Rais Magufuli amepokea taarifa ya maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe 02 Machi, 2016 Katika Jiji la Arusha, Nchini Tanzania. 

Rais Magufuli ndiye Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inayojumuisha nchi tano wanachama ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. 

Akizungumza mara baada ya mazungumzo hayo Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo Dkt. Richard Sezibera, amesema maandalizi kuhusiana na mkutano huo yanakwenda vizuri. 

Amesema pamoja na mambo mengine mkutano huo, utajadili masuala kadhaa yakiwemo mpango wa kuanzisha viwanda vya magari ndani ya Jumuiya ili kupunguza uingizaji wa magari kutoka nje ya nchi na Marais kuzindua pasi ya kusafiria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. 

Kuhusu hali ya Jumuiya, Dkt. Sezibera amesema inaendelea vizuri na ametaja baadhi ya mambo ambayo yamefanyika kuwa ni kutiwa saini kwa mkataba wa umoja wa forodha, makubaliano ya soko la pamoja na makubaliano ya sarafu moja. 

Mengine ni kuwepo kwa mazungumzo kuhusu uimarishaji wa miundombinu kama vile reli na umeme ndani ya Jumuiya, na mazungumzo kuhusu umoja wa kisiasa. 

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Dkt. Augustine Mahiga, amesema Tanzania ikiwa ni mwenyeji wa kikao hicho ipo tayari kupokea ugeni na kwamba pamoja na kufanyika kwa kikao hicho, marais wa Tanzania na Kenya watafungua barabara inayounganisha Tanzania na Kenya katika Mpaka wa Holili na kutakuwa na shughuli ya kuweka jiwe la msingi katika kituo cha pamoja cha mpakani kwa ajili ya kuwezesha upitaji wa mizigo na watu yaani "One Stop Boarder Post" 

Gerson Msigwa 
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU. 
Dar es salaam.
24 Februari, 2016.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Hongera ku-host mkutano huu muhimu. Tunasubiri kwa hamu mh. magufuli kuhudhuria mkutano wa kimataifa kwa mara ya kwanza akiwa Raisi wa Tanzania. Mwenyezi Mungu atuepushe na ile hali ya baba mwenye nyumba kuwaalika wageni nyumbani kwake alafu wageni wamekuja na yeye kajifungia chumbani kwake hadi wameondoka. alex bura dar.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...