Serikali imesema
itachukua hatua kali kwa kampuni ya Halotel kama itashindwa kutekeleza
makubaliano ya mkataba wa kusambaza huduma za simu na mtandao katika ofisi za
Serikali katika kila Wilaya nchini kote.
Kauli hiyo imetolewa
na Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa wilayani Maswa
wakati akizungumza na watendaji wa sekta ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Mkoani Simiyu na kusisitiza kutoa ushirikiano unaostahili kwa kampuni hiyo.
“Makubaliano yetu kati
ya Serikali na Halotel ni kuunganisha ofisi za Umma kwa mtandao zikiwemo shule
tatu katika kila Wilaya, Hospitali, Mahakama na Ofisi za Polisi ili kuwezesha
mkakati wa mawasiliano vijijini kutekelezeka”, amesema Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa
ameeleza kuwa ifikapo mwaka 2017 kila eneo hapa nchini litakuwa na huduma ya
mawasiliano ya mtandao na kuwezesha wananchi wote kunufaika na huduma hizo.
Katika hatua nyingine
Prof. Mbarawa amekagua Ujenzi wa Barabara ya Lamadi-Bariadi KM 71.8 na Bariadi-Maswa
KM 49.7 na kuwapongeza makandarasi wanaojenga barabara hizo kwa kazi nzuri
wanayofanya.
“Nawapongeza kwa kazi
nzuri mnayoifanya, hakikisheni kazi yenu inauwiana na thamani ya fedha na
kuhakikisheni wafanyakazi wazawa wanapewa kipaumbele katika kazi wanazoziweza
na kupewa mikataba stahiki ya kazi wanazozifanya”, amesititiza Prof. Mbarawa.
Aidha, Waziri Prof.
Mbarawa amemuagiza mkandarasi anaejenga barabara ya Maswa-Mwigumbi KM 50.3
kuhakikisha nyumba zinazojengwa kwa ajili ya mkandarasi zinajengwa kwa ubora
ili zitumike kwa muda mrefu.
“Nakuagiza Meneja wa
TANROADS, hakikisha nyumba hizi baada ya mradi wa barabara kukamilika unazikabidhi
kwa jeshi la polisi ili waweze kuzitumia kwa ajili ya makazi na ofisi”, amesema
Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu Bw. Eraston Mbwilo amemwomba Waziri Prof. Mbarawa kuelekeza
nguvu za ujenzi wa ofisi na nyumba za watumishi katika mkoa huo.
Katika hatua nyingine,
Mkuu wa Wilaya ya Maswa Bi. Rosemary Kirigini amemuomba Waziri Prof. Mbarawa
kuwawezesha Wakala wa Majengo nchini (TBA) kukamilisha mradi wa Ujenzi wa Ofisi
ya Mkuu wa Wilaya hiyo unaojengwa sasa kwa miaka mitano ili kuipunguzia Wilaya
hiyo adha ya kutumia jengo chakavu ambalo si salama hasa kipindi cha mvua.
Waziri Prof. Mbarawa pia
amekagua Kiwanja wa Ndege kilichopo Mkoa wa Shinyanga na ofisi za Mamlaka ya
Hali ya Hewa (TMA) kiwanjani hapo na kusisitiza kuwa Serikali iko katika hatua
za kuboresha uwanja huo kuwa wa kisasa ili kuvutia mashirika mengi ya ndege
kutumiwa kiwanja hicho.
Waziri Prof. Mbarawa
yupo kwenye ziara ya kukagua miradi ya ujenzi kwenye sekta za barabara, nyumba,
viwanja vya ndege na mkongo wa taifa wa mawasiliano katika mikoa ya kanda ya
ziwa ambapo ametembelea Wilaya za Busega, Bariadi na Maswa mkoani Simiyu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa mkandarasi anayejenga
barabara ya Lamadi-Bariadi Km 71.8, mkoani Simiyu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (aliyevaa koti la bluu), akisikiliza maelezo
ya mkandarasi kuhusu ujenzi wa mtambo (hauonekani pichani) wa kusaga kokoto kwa
ajili ya ujenzi wa barabara ya Maswa-Mwigumbi Km 50.3.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akiongea na vibarua wanaofanya kazi kwenye
mradi wa barabara ya Maswa-Mwigumbi Km 50.3, mkoani Simiyu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiongea na wafanyakazi wa sekta za Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano kuhusiana na mkakati wa Wizara wa kuongeza mapato
mkoani Simiyu.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa, akitazama kifaa cha kupima
hali ya hewa katika uwanja wa ndege wa Shinyanga. Kushoto ni Meneja wa Mamlaka
ya Hali ya Hewa (TMA) mkoani Shinyanga Bw. Omary Khamis na katikati ni Meneja
wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga Eng. Augustino Philipo. Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...