Na Mwandishi Maalum, New York
Jumuiya ya Kimataifa imemuelezea aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Sita wa Umoja wa Mataifa,
Marehemu Boutros Boutros- Ghali, kama kiongozi ambaye siyo tu alifanya
kazi katika mazingira magumu
lakini pia alitoa mchango mkubwa katika kuijenga na
kuimarisha Taasisi hiyo ya Kimataifa.
“ Leo tumekusanyika
hapa kutambua na kuheshimu mchango
mkubwa wa mtangulizi wangu katika
kukijenga na kukiimarisha chombo hiki. Hapana shaka aliingia katika kipindi
kigumu mwishoni mwa vita baridi”
akaeleza Ban Ki Moon.
Jana ( alhamisi) Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likiongozwa
na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
litenga muda maalum wa kumuenzi
na kukumbuka mchango mkubwa wa
Marehemu Boutros Boutros Ghali.
Katibu Mkuu Ban Ki Moon, katika salamu zake amebainisha kwamba, pamoja na
mazingira magumu ya utekelezaji wa majukumu yake, na hasa ikizingatiwa kwamba alishika wadhifa
huo mwisho wa vita baridi,bado aliweza kuweka misingi mingi
mizuri ikiwamo ya uboreshaji wa
Operesheni za Ulinzi wa Amani kupitia kofia ya
Umoja wa Mataifa pamoja na utendaji wa sekretarieti ya Umoja wa Mataifa.
“ Alikuwa mpenda
Amani, usalama, haki za binadamu, mwanadiplomasia, msomi na mwanazuoni
aliyebobea ambaye hakuogopa
kusema ukweli na kusimamia kile alichokiamini.
Akasema Ban Ki Moon.
Marehenu Boutros
Boutros- Ghali ambaye amefariki siku ya
jumanne akiwa na miaka 93 alikuwa Katibu
Mkuu wa Kwanza kutoka Barani Afrika na Mwarabu wa Kwanza.
Wazungumzaji wengi
waliozungumza kwa niaba ya Kanda zao wanazoziwakilisha walieleza kwamba
Jumuiya ya Kimataifa ilikuwa imeondokewa na
mtu mashuhuri ambaye bado alikuwa na mchango mkubwa katika diplomasia ya kimataifa.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa
Kudumu wa Marekani katika Umoja
wa Mataifa, Balozi Samantha Power, katika salamu za serikali yake, amemuelezea
Boutros Boutros- Ghali kama
kiongozi ambaye alikuwa na uzoefu mkubwa
katika uendeshaji wa majadiliano .
Akataja baadhi ya mafanikio
yaliyotoka na usimamizi na uongozi wake ni pamoja na kuushawishi utawala wa Makaburu wa Afrika
ya Kusini kumwachia huru Marehemu Mzee Nelson Mandela.
Pamoja na kueleza
kwamba Boutrous Boutrous – Ghali
alikuwa kiongozi mwenye vipaji vipingi, na
aliyefanya mengi katika diplomasia
ya Umoja wa Mataifa, lakini pia akaeleza
wazi kwamba serikali yake ( Marekani) mara kwa mara ilitofautiana na Katibu Mkuu Boutros Ghali.
Na akaongeza kwamba
pamoja na kutofautiana huko bado
Marekani inaheshimu na kutambua mchango mkubwa wa Katibu Mkuu huyo wa Sita. Na
kusisitiza kwamba Jumuiya ya Kimataifa
inapashwa kuyaendeleza na kuyadumisha mema ya Marehemu Boutros Ghali.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...