Benki ya Exim Tanzania imeboresha huduma yake ya utumaji na upokeaji wa pesa kimataifa kwa kuharakisha ukamilishaji wa miamala hiyo ambapo kwa sasa wateja wake watatumia saa nne badala ya muda wa saa 12 uliokuwa ukitumika hapo awali.
“Exim tumekuwa tukipambana kila siku kuhakikisha tunatoa huduma bora, za haraka na kwa usalama zaidi ili kuwaunganisha wateja wetu na fursa za kimataifa. Kwenye hili tunatoa hakikisho kwa wateja wetu kwamba iwapo kutatokea ucheleweshaji zaidi ya muda wa masaa manne basi tutalazimika kuwarejeshea gharama zao walizolipa kwa ajili ya huduma,’’ alisema Bw Tumaini Mwakafwaga ambaye ni mkuu wa kitengo cha operesheni za Benki hiyo jijini Dar es Salaam jana.
Hata hivyo alibainisha kuwa hakikisho hilo la muda wa masaa manne (guarantee) litahusu wateja wenye maombi (miamala) yasiyokuwa na utata, wenye nyaraka onyeshi (supporting documents) pamoja na wale wenye kiasi cha kutosha kwenye akaunti zao.
“Lakini pia kuna mazingira ambayo yanaweza kufanya tukashindwa kumrejeshea mteja gharama zake (refund) ikiwemo pale ambapo mfumo wetu wa kuendesha miamala utakuwa umekwama kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu yakiwemo majanga ya asili,’’ aliongeza Mwakafwaga.
Alisema watumiaji wa huduma hiyo watakuwa wakipokea taarifa kuhusu mwenendo mzima wa miamala yao kwa kuwa itakuwa ikifuatiliwa kwa ukaribu kila hatua inayopitia.
“Kiukweli timu yetu inayohusika na kuchakata (processing) miamala hii inauelewa wa kutosha pamoja na uwezo mkubwa wa kutimiza majukumu yao kwa haraka kuanzia muda ambao mteja anaanza kutumia huduma hii hadi hatua ya mwisho. Mameneja na wasaidizi wao wapo tayari kuhakikisha kila kitu kinaenda kwa wakati na kwa usahihi,’’ alisisitiza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...