Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es salaam (Dawasco) limewanasa mama ntilie zaidi ya 6 wakiwa wanatumia huduma ya Maji kinyume cha utaratibu kwa kujiunganishia laini ya Majisafi na kukosa mita wala akaunti kutoka Dawasco kwenye eneo la mtaa wa Kisutu, Ilala jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwenye eneo la tukio Afisa Biashara wa Dawasco, Deogratius Ng’wandu amesema kuwa walibaini wizi huo wa Maji kwenye operesheni yake maalum ambayo inayoendelea kwenye maeneo yote ya Jiji la Dar es salaam na ndipo walipokuta Mama ntilie ambao walikuwa kwenye eneo hilo lilozungushiwa mabati lisilo na jengo ambapo walikuwa wakipika pamoja na kulima mbogamboga kwa kutumia Maji ya Dawasco.
“Tumekuta wakina Mama ntilie wakiwa wakitumia huduma ya Maji ambayo yameunganishiwa kinyume cha utaratibu ambapo yalikuwa hayana mita wala akaunti namba na Maji hayo yamekuwa yakitumika kupikia kufanya usafi pamoja na kulima mboga mboga ila wanadai hawamfahamu mwenye eneo hivyo tumewapeleka Polisi kwa hatua zaidi za kisheria” , alisema Ng’wandu.
Kwa upande wa mwenyekiti wa serikali ya mtaa Kisutu, Subira Ngeseyani ameomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwataja wezi wa Maji kwenye mita yao kama alivyoagiza mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mh. Paul Makonda ambapo aliagiza wenyeviti wa Serikali za mtaa jijini Dar es Salaam kushirikiana na Dawasco pamoja wananchi kubaini wezi wa Maji wanaofanya wateja halali kukosa huduma ya Maji.
“Wananchi wote ni jukumu letu kushirikiana na Dawasco kuwabaini wezi wa Maji kwenye mitaa yetu kama Mkuu wa Mkoa alivyoagiza ilikufanya wale wateja halali wanaostahili huduma ya Maji kupata kwani ni haki yao hivyo wote tushirikiane tuondoe tatizo la wizi wa Maji Jijini Dar es salaam”,Ngeseyani.
Kwa upande wa Mama ntilie hao Bi Aziza Hassan amekiri kuwa walikuwa wanatumia huduma ya Maji hayo kwenye eneo hilo ila walikuwa hawaelewi kuwa yameunganishwa kinyume cha utaratibu na mmiliki wa eneo pia kutokana na hali ngumu ya kimaisha walishindwa kuulizia kwani walijua gharama zakuunganishiwa kihalali ni kubwa.
“Kweli tumekuwa tukitumia huduma ya Maji kwenye eneo hili kwa shughuli zetu ila hatukuwa tukielewa kama yameunganishwa kinyume cha utaratibu hata hivyo kutokana na hali ngumu ya maisha tusingeweza kujiunganishia huduma ya Maji kwani ni gharama”, alisema bi Aziza.
Hata hivyo Dawasco imeendelea kuwasihi wakazi wa Jiji la Dar es salaam kuwafichua wezi wa Maji kwenye maeneo yao kama alivyoagiza Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam na pia watu wote ambao wamejiunganishia kinyume na utaratibu wajisalimishe na kutambulika kabla hawajakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...