Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb.) , akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Chuo cha Diplomasia wakati wa ziara yake Chuoni hapo. Chuo hicho ni moja ya Taasisi zilizo chini ya Wizara. Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia, Balozi Dkt. Mohammed Maundi (katikati) na wa kwanza kulia ni Mkurugenzi wa Taaluma Chuoni hapo, Dkt. Wetengere Kitojo . Naibu Waziri akiangalia vitabu vilivyopo kwenye Maktaba ya Chuo hicho
Naibu Waziri akiwaeleza jambo uongozi wa chuo hicho. 

Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa imejipanga kuhakikisha Chuo cha Diplomasia kinaboresha huduma zake za utoaji elimu na mafunzo ya masuala ya Diplomasia ili kukidhi mahitaji ya Watanzania katika taaluma hiyo.

Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Susan Kolimba alipofanya ziara katika Chuo hicho kilichopo Kurasini Jijini Dar es Salaam ambacho ni moja ya Taasisi zilizo chini ya Wizara.

Mhe.  Kolimba alisema kwamba Chuo cha Diplomasia ambacho kilianzishwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Msumbiji ni miongoni mwa vyuo vilivyojipatia sifa kubwa ndani na nje ya nchi kwa kutoa mafunzo katika masuala ya Diplomasia na hivyo Wizara haina budi kuhakikisha inaendelea kukiboresha ili kuhakikisha kinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Mhe. Dkt. Susan alisema kuwa, miongoni mwa masuala yanayotakiwa kufanyiwa kazi katika maboresho hayo ni pamoja na miundombinu ya Chuo kwa maana ya kuongeza majengo, vifaa vya kisasa vya kufundishia, maabara za kisasa za lugha, maktaba na kuongeza Wakufunzi.Aidha, Mhe. Kolimba aliueleza Uongozi wa Chuo hicho kuwa ni vema vipaumbele katika kukiletea chuo maendeleo vikaainishwa ikiwa ni pamoja na kuonyesha mikakati ya kila changamoto ili kupata suluhisho la haraka la changamoto hizo.

“Ninawapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya na tunaahidi kuwa pamoja nanyi wakati wote ili kuhakikisha Chuo chetu kinafikia viwango vinavyostahili” alisema Mhe. Kolimba.Vilevile alieleza kuwa ni vema Chuo kikaimarisha ushirikiano na Vyuo vingine vya ndani na nje kwa kuainisha maeneo muhimu ya ushirikiano yenye faida kwa pande zote. Pia alikitaka Chuo kuwa na mikakati itakayokiwezesha Chuo hicho kuweza kujiendesha kibiashara kama vyuo vingine nchini na kuacha utegemezi mkubwa katika bajeti ya Serikali.

Awali akimkaribisha Naibu Waziri Chuoni hapo, Mkurugenzi wa Chuo hicho, Balozi Mohammed Maundi alisema kuwa Chuo hicho kinaendelea kuboresha maeneo mbalimbali ya Chuo hicho ikiwemo kuanzishwa kwa Kozi ya Shahada mwaka 2015 na tayari chuo kimepata michoro ya majengo kwa Chuo kipya wanachotarajia kukijenga na sasa kinachohitajika ni fedha ili kukamilisha mpango huo ambao kwa kiasi kikubwa utamaliza changamoto zinazokikabili Chuo.

Chuo cha Diplomasia (CFR) ni chuo kilichoanzishwa kwa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Msumbiji mwaka 1978. Chuo kimekuwa kikitoa elimu katika ngazi ya Cheti, Diploma, Shahada na Shahada ya Juu. 
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...