Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana akizungumza na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania Mhe. Florence Tinguely Mattli (kulia) na ujumbe alioambatana nao wakati walipo mtembelea Mkuu huyo wa Mkoa ofisini kwake mwishoni mwa wiki.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana akizungumza na Balozi wa Uswisi nchini Tanzania Mhe. Florence Tinguely Mattli (wa pili toka kulia) na ujumbe alioambatana nao wakati walipo mtembelea Mkuu huyo wa Mkoa ofisini kwake mwishoni mwa wiki.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana amemuomba balozi wa Uswisi hapa nchini Mhe. Florence Tinguely Mattli kusaidia kuunga Mkono jitihada za Serikali ya Mkoa wa Dodoma za kuongeza ajira kwa vijana kupitia shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma mbalimbali.

Mhe. Rugimbana alimweleza balozi wa uswisi hapa nchini kuwa moja kati ya vipaumbele vyake kwenye Mkoa wa Dodoma ni kuzalisha ajira kwa vijana kupitia uundaji wa makambi ya vijana ya uzalishaji mali na shughuli za kiuchumi kupitia sekta za kilimo, ufugaji na utoaji huduma mbalimbali, jambo ambalo hata viongozi wakuu wa kitaifa wamekuwa wakisisitiza.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki alipokutana na balozi wa Uswisi nchini Tanzania Mhe. Florence Tinguely Mattli na ujumbe wake wakati walipomtembelea ofisini kwake kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo hapa Mkoani Dodoma na miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Serikali ya Uswisi

Katika kufanikisha azma hiyo Mhe. Rugimbana alisema kuwa serikali ya Mkoa wa Dodoma imejipanga kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa wadau mbalimbali wa maendeleo wanaofadhili miradi ya huduma za jamii na uzalishaji mali, na kuongeza kuwa kwa sasa serikali ya awamu ya tano imejikita katika kutaka wananchi kufanya kazi hususani vijana kuachana na mambo ambayo yanawapotezea muda bure kama michezo ya ‘pool’ badala yake wajikite kwenye shughuli za uzalishaji mali, lakini pia serikali inajukumu la kuwajengea vijana mazingira mazuri ya kuanzisha shughuli za uzalishaji mali.

Kwa upande wake balozi wa Uswisi hapa nchini Mhe. Florence Tinguely Mattli amemwambia Mhe. Rugimbana kuwa Nchi yake ya Uswisi na Tanzania zimekuwa na ushirikiano wa karibu wa muda mrefu na imekua ikifadhili miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za jamii. Aliongeza kuwa katika ushirikiano huo Mkoa wa Dodoma ni moja kati ya Mikoa waliyoipa kipaumbele.

Alisema nchi yake inaunga Mkono jitihada za serikali za kuongeza ajira kwa vijana kupitia mradi wa Kuongeza Fursa za Ajira kwa Vijana kupitia shughuli za uzalishaji mali za kilimo, mifugo na usafi wa mazingira ambao unawalenga vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 30 ambao hawana ajira, wale ambao hawakupata nafasi za kupata elimu na wale walio vijijini na hususani wale wenye malengo ya kupata ajira au kujiajiri kupitia fursa mbalimbali zilizopo kwenye maeneo yao.

Mradi huu unafadhiliwa na kutekelezwa na shirika la maendeleo na ushirikiano la Uswisi (SDC) kwa kushirikisha wadau wengine wa maendeleo kama vile shirika la kimataifa la maendeleo la Uholanzi (SNV) ambapo awamu ya kwanza itaanza 2016 hadi 2018 na utajumuisha mikoa ya ukanda wa kati ikijumuisha Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga na pia Morogoro kwa mwaka wa 2016 pekee umetengewa jumla ya Euro 1.4 Milioni

Balozi Florence Tinguely Mattli aliongeza kuwa mradi huo utahusu kuwawezesha vijana eneo la utaalamu na mafunzo ya ufundi na stadi za maisha, na pia uwezeshaji wa uanzishaji miradi ya uzalishaji mali baada ya mafunzo. Alisema kupitia miradi ya uzalishaji kwenye kilimo, ufugaji nishati na usafi na utunzaji Mazingira, vijana wataboresha hali za maisha yao na kujipatia ajira na kipato.

Alisema changamoto inayoikabili sekta ya ajira kwa vijana ni pamoja na mtazamo hasi na imani haba juu ya uwezo na utaalamu wa vijana hasa upande wa waajiri wa sekta binafsi, lakini pia sekta za uzalishaji mali alizozitaja hapo juu bado hazijaweza kutoa mchango unaoridhisha kwa Taifa, wakati zinafursa nyingi za kuzalisha ajira kwa vijana na kuchangia pato la taifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...