Na Rebecca Kwandu

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amewataka watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwa na utaratibu wa kutembelea maeneo yao ya kazi mara kwa mara ili kujionea hali halisi na kutatua kero zilizopo.

Akizungumza na walimu wa shule ya msingi Nzuguni B. wakati wa ziara aliyoifanya kutembelea shule  hiyo na shule ya sekondari Nzuguni A., Mhe. Jafo alisema watumishi hawawezi kufanya kazi kwa ubora iwapo watakuwa hawatembelei na kukagua maeneo yao ya kazi.

“ Kumekuwa na uzembe kwa Wakuu wa Idara kutokusikiliza matatizo ya chini, kutowatembelea watumishi waliopo chini yetu inawasababishia kukosa mahali pa kusemea shida zao na kuchanganyikiwa. Ni vizuri kuwa na utaratibu wa kuwatembelea watumishi tunaowaongoza ili kujua shida zao na kuzitatua. Alisisitiza Mhe. Jafo.

Aidha, aliwataka walimu wa shule za msingi Nzuguni B na Shule ya sekondari Nzuguni A kuweka utaratibu wa kuweka malengo na kujipima kuona walichokifanya ili kupata matokeo tarajiwa.

Wakati huo huo, Naibu  Waziri wa Nchi Jafo ametoa Mabati 164 ili kuchangia ujenzi wa Madarasa ya shule ya msingi Nzuguni B iliyopo kata ya Nzuguni katika halmashauri ya Mji wa Dodoma.

Mhe. Jafo alitoa Mabati hayo baada ya kufanya ziara ya kutembelea shule hiyo ili kujionea hali halisi ya maendeleo yake ikiwa ni moja ya taratibu alizojiwekea za kutembelea maeneo mbalimbali yanayohudumiwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI ili kujionea changamoto mbalimbali zilizopo katika utoaji wa huduma na kuzitafutia ufumbuzi.

Katika ziara hiyo Mhe. Jafo alikuta Idadi  kubwa ya watoto walioandikishwa kujiunga na darasa la kwanza hali iliyopelekea kukosekana kwa vyumba vya kutosha kwa ajili ya kujifunzia wanafunzi ambapo kwa kutatua kero hiyo, shule hiyo imeanza ujenzi wa vyumba vya madarasa na kwa upande wake alichangia bati 164 ili kuwezesha madarasa hayo kukamilika.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo akiwa katika ziara ya kutembelea shule ya msingi Nzuguni B. Kulia kwake ni Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Mstahiki Jaffari Mwanyemba aliyeongozana na Mhe. Naibu waziri katika ziara hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...