Msemaji wa klabu ya Simba, Haji Sunday Manara akizungumza na vyombo vya habari juu ya uamuzi wa klabu yake hiyo, kumfungia kwa mechi tano beki wao wa kulia, Hassan Ramadhan Kessy kwa rafu mbaya aliyomchezea mshambuliaji wa Toto Africans, Edward Christopher, katika mchezo ambao Simba ililala bao 1-0 kwenye  uwanja wa Taifa, baada ya mchezaji huyo kutolewa nje kwa kadi nyekundu na kudaiwa kuigharimu klabu hiyo kwa kukosa pointi tatu muhimu

Uongozi wa klabu ya Simba umemsimamisha beki wao wa kulia, Hassan Ramadhan Kessy kwa rafu mbaya aliyomchezea mshambuliaji wa Toto Africans, Edward Christopher.

Katika mchezo huo ambao Simba ililala bao 1-0 kwenye  uwanja wa Taifa,  Kessy alitolewa nje na kudaiwa kuigharimu klabu hiyo kwa kukosa pointi tatu muhimu.
Pamoja na uongozi wa Simba kumchukulia hatua Kessy na kukosa mechi zote zilizobakia katika msimu huu, klabu hiyo pia imeshindwa kumchukulia hatua za kinidhamu kipa kutoka Ivory Coast, Vicent Agban ambaye aliamua kumzaba makofi mchezaji huyo aliyejiunga na Simba akitokea klabu ya Mtibwa Sugar.
Msemaji wa klabu hiyo, Haji Manara alisema kuwa hawana ushahidi wa tukio hilo amalo linadaiwa kutokea katika vyumba vya kubadilishia nguo mara baada ya mchezo huo kumalizika.
Pamoja na kushuhudiwa na baadhi ya wachezaji na Kessy kutoa taarifa polisi kwa ajili ya kupata matibabu, Manara, mratibu wa klabu hiyo, Abbas na kocha Jackson Mayanja walikanusha taarifa hizo.
Manara alisema kuwa Kessy alifanya rafu ya ‘kuua’ na klabu yenye heshima kubwa kama Simba imeamua kuchukua hatua kali ili kuwapa fundisho wachezaji wa aina ya Kessy ambao wanataka kufanya hivyo.

“TFF itamfungia mechi tatu kwani alipata kadi nyekundu ya moja kwa moja (straight red card),  tumeona adhabu hiyo ya kikanuni haitoshi kwetu, tumeamua kumfungia mechi nyingine na kama msimu utaruhusu, atarejea kucheza,” alisema Manara kwa kejeli huku akijua kuwa Simba imebakiza mechi tano tu kumaliza ligi.
Manara alisema kuwa Simba inahitaji wachezaji wenye nidhamu na weledi na siyo kuwa na wachezaji wa aina ya Kessy ambaye katika mchezo huo alionekana akilaumiwa hata na wachezaji wenzake.

Kocha wa klabu hiyo, Jackson Mayanja aliunga mkono adhabu hiyo na kusema ilikuwa mbaya sana. Mayanja ambaye aliwaomba radhi  mashabiki wa Simba kwa matokeo mabaya, alisema kuwa rafu ya Kessy haikuwa na sababu kwani alikuwa na mpira peke yake na kumsubiri Christoher na kupiga mpira huku akimpandishia mguu kichwani.
“Kwa kweli nimeshangazwa sana, sikuwepo uwanjani kwani nami nilikuwa nimeonewa na mwamyuzi, niliangalia kupitia televisheni na kusikitika,” alisema Mayanja.
Mganda huyo ameshauri kikosi kisibomolewe hata kama Simba itakosa taji msimu huu, ili kiboreshwe na msimu ujao kirejee na nguvu mpya.

Kuhusu kiungo Abdi Banda, kocha huyo amesema mchezaji huyo hajafukuzwa bali amejiondoa mwenyewe kwenye timu baada ya kususa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...