Ofisi
ya Bunge imebaini upotoshwaji mkubwa Katika habari iliyochapishwa na Gazeti la
Nipashe toleo la leo Aprili 16, 2016 yenye kichwa cha habari kisemacho “ Bunge
sasa laufyata mkataba wa Lugumi”. Habari hiyo imeandikwa kufuatia ufafanuzi
uliotolewa na Bunge jana kuhusu maagizo yaliyotolewa na Kamati ya Hesabu za
Serikali (PAC) dhidi ya utekelezaji wa mkataba wa Jeshi la Polisi na Kampuni ya
Lugumi Enterprises Ltd kuhusu mradi wa utambuzi wa alama za vidole
(AFIS) (Automated
Fingerprint Identification System.
Ndani
ya habari hiyo pia, Gazeti hilo limeeleza kuwa kamati ya PAC iliwahi kuliandikia
Jeshi la Polisi kulitaka liwasilishe mkataba huo mbele ya Kamati, jambo ambalo
si kweli bali ni upotoshwaji wa makusudi wenye lengo la kujenga hisia mbaya
kuhusu mwenendo wa shughuli za Bunge mbele ya Umma.
Ukweli
ni kwamba PAC haijawahi kuliandikia jeshi la Polisi kama inavyodaiwa na Gazeti
hilo. Nukuu ya maelezo ya PAC katika Hansard kwa Afisa Masuhuli kuhusu jambo
hilo inasema kama ifuatavyo:
“Kamati inamuagiza Afisa
Masuhuli kuwasilisha maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa Mkataba baina ya
Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi
Enterprises kuhusu mradi wa AFIS.
Maelezo hayo yawasilishwe kwa Ofisi ya
Katibu wa Bunge kabla ya Jumatatu tarehe 11 Aprili, 2016”.
Katika agizo
hilo PAC haikuwa imeandika kwa maandishi kuhusu agizo lake hilo hadi tarehe 12
Aprili, 2016 ilipo mweleza Katibu wa Bunge aweze kuwasilisha agizo hilo kwa maandishi
ili liweze kupata Kinga chini ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge
ambapo barua iliandikwa na kuwasilishwa kwa Afisa Masuhuli
ili kupatiwa maelezo hayo kabla ya tarehe 18 Aprili, 2016.
Aidha, Mwandishi pia amelituhumu Bunge kuwa lina nia ya kuficha
ukweli kuhusu jambo hili kwa kusema taarifa
ya ufafanuzi iliyotolewa na Bunge ni “kama
kufunika kombe mwanaharamu apite kwa kujaribu kupotosha maagizo ya yaliyotolewa
na kamati ya PAC ambayo inataka kuuona mkataba huo”
Ni vyema ikafahamika kuwa si jambo jema kwa
mwandishi au chombo chochote cha habari kulituhumu Bunge linapotekeleza
majukumu yake kwa kuwa Bunge linafanya kazi zake kwa kwa kuzingatia kanuni zake
za Kudumu ikiwa ni pamoja na Sheria.
Ofisi ya Bunge inalisihi Gazeti la Nipashe kuomba
radhi kutokana na taarifa yake hiyo iliyojaa upotoshwaji mkubwa kwa uzito ule
ule au kurekebisha taarifa yake kulingana na ukweli ulivyo haraka iwezekanavyo.
Imetolewa
na;
Ofisi ya Bunge,
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano,
S.L.P 9133,
DAR ES SALAAM.
16 Aprili, 216.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...