Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kinyerezi jijini Dar es salaam ambao mwaka jana walipatiwa msaada wa kompyuta 25, Televisheni yakufundishia pamoja na printa kutoka taasisi ya inayojishughulisha na jamii ya Vodacom Tanzania Foundation kupitia mradi wake wa Smart Schools wameeleza kuwa wanafurahia kujifunza somo la kompyuta kwa vitendo tofauti na ilivyokuwa hapo awali kabla ya kupatiwa msaada huo.
Wakieleza hisia zao baada ya ujumbe wa taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation kutembelea shuleni hapo jana kujionea maendeleo ya wanafunzi hao tangu wapatiwe msaada huo walisema kuwa hivi sasa ndoto zao za kutoachwa nyuma katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia zinaanza kutimia.
Akiongea kwa niaba ya wenzake,mwanafunzi Christina Salum anayesoma kidato cha nne shuleni hapo alisema kuwa tangu wapate msaada huo na kujifunza somo la kompyuta kwa nadharia na vitendo wanafunzi wengi wameanza kuelewa matumizi ya kompyuta tofauti na hali ilivyokuwa hapo awali.
“Kwa sasa tukifundishwa kompyuta tunaweza kuelewa kwa haraka na mwamko wa wanafunzi kutaka kuelewa matumizi ya kompyuta umekuwa mkubwa na woga wa kudhani kuwa teknolojia ya matumizi ya kompyuta ni ngumu umeondoka ,tunashukuru Vodacom Foundation kwa kutuwezesha kutobaki nyuma katika ulimwengu wa kisasa wa sayansi na teknolojia.
Naye mwalimu anayefundisha somo hilo shuleni hapo , Lupakisyo Igomole amesema japo wanafunzi wanaelewa na wanapenda sana somo hilo bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya viti vya kukalia hali inayowalazimu kuwafundisha wanafunzi hao wakiwa wamekaa chini sakafuni.
Mkuu wa Vodacom Tanzania Foundation, Renatus Rwehikiza alisema kuwa changamoto hiyo itafanyiwa kazi ili kuwawezesha wanafunzi hao kusoma somo hilo katika mazingira rafiki zaidi wakiwa wamekaa kwenye viti .
Mkuu wa Vodacom Tanzania Foundation, Renatus Rwehikiza (kulia)akiwafafanulia jambo baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Kinyerezi jijini Dar es Salaam kuhusiana na somo la kompyuta alipotembelea shuleni hapo kupata mrejesho wa maendeleo baada ya kutoa msaada wa kompyuta 25, Televisheni yakufundishia pamoja na printa kupitia mradi wa Smart Schools mwaka jana.
Mwalimu wa masomo ya sayansi wa shule ya sekondari Kinyerezi jijini Dar es Salaam, Lupakisyo Igomole (kushoto) akiwafundisha kwa vitendo baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne wa shule hiyo kupitia kompyuta wakati walipotembelewa na oungozi wa taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation waliotoa msaada wa kompyuta hizo mwaka jana kupitia mradi wao wa Smart Schools.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Kinyerezi jijini Dar es Salaam,Wakijisome kupitia kompyuta wakati walipotembelewa na oungozi wa taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation waliotoa msaada wa kompyuta hizo mwaka jana kupitia mradi wao wa Smart School kutaka kujua maendeleo yao shuleni hapo.
Mwanafunzi wa kitado cha tatu katika shule ya sekondari Kinyerezi jijini Dar es Salaam, Aurelia Kitenge (kushoto) akimwelezea jambo Mkuu wa Vodacom Tanzania Foundation, Renatus Rwehikiza wakati alipotembelea shuleni hapo kwa ajili ya kujionea maendeleo ya mradi wao wa smart Schools ambao ulitoa msaada wa kompyuta hizo shuleni hapo.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...