17/5/2016.
SERIKALI kupitia wakala ya Serikali mtandao imesema kuwa inaendelea kulifanyia kazi suala la uanzishaji wa mfumo wa TEHAMA utakaowawezesha wananchi kupata huduma na taarifa mbalimbali za Serikali kupitia simu zao mkononi mahali popote walipo kwa njia ya mtandao.
Utaratibu huo pia utawawezesha wahitimu wa vyuo mbalimbali vya elimu nchini Tanzania kupata taarifa za ajira za Serikali na kuwawezesha kuomba nafasi hizo, kufuatilia majibu ya usaili walioufanya na kupata taarifa za kuitwa kazini kupitia namba za utambulisho watakazopewa kupitia ujumbe mfupi (sms).
Akizungumza na Wahariri wa vyombo vya Habari leo jijini Dar es salaam Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao (e-Government Agency) Dkt. Jabiri Bakari amesema kuwa mfumo huo utamuwezesha mwananchi kupata huduma za Serikali mahali popote alipo kufuatia mifumo ya TEHAMA kuwasiliana na kubadilishana taarifa.
Amesema kuwa dhana ya Serikali Mtandao ni kuwa na matumizi ya TEHAMA kwenye shughuli zote za Serikali kwa lengo la kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji kwenye huduma za Afya, Utalii, Malipo ya tozo za huduma,vibali, leseni ,elimu na huduma mbalimbali za Serikali.
Dkt. Jabiri amesema moja ya vitu vinavyosababisha usumbufu kwa wananchi kutokana na kukosekana kwa Serikali mtandao ni pale wanapohitaji kupata huduma za Serikali ikiwemo Hati ya kusafiria ambapo hulazimika kwenda Idara ya Uhamiaji kujaza fomu maalum na kisha kusubiri kwa muda wa zaidi ya wiki moja ili taarifa zao ziweze kuhakikiwa na taasisi nyingine za Serikali wakati suala hilo lingeweza kuchukua siku moja.
“Matumizi ya TEHAMA kwenye shughuli za Serikali hurahisiaha sana upatikanaji wa taarifa kwa kuwa mifumo inawasiliana na kubadilishana taarifa haimlazimu mwananchi kwenda kwenye taasisi zaidi ya tano kupata huduma yake” Amesisitiza Dkt. Jabiri.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...