NA K-VIE MEDIA/Khalfan Said

NAIBU balozi wa Uingereza hapa nchini Bw. Matt Sutherland, (wa pili kushoto), ameisifu taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, (JKCI), kwa kuratibu kambi ya upasuaji wa moyo kwa kushirikiana na madaktari kutoka nje kwa mafanikio makubwa.
Pongezi hizo amezitoa jana  May 3, 2016, baada ya kutembelea kambi hiyo maalum iliyoko kwenye taasisi hiyo, na kujionea madaktari wakiendelea na kazi ya kuwafanyia upasuaji watoto wa Kitanzania kutoka sehemu mbalimbali nchini.
“Nimefurahishwa sana na uamuzi wa JKCI wa kuratibu zoezi hili kwa ushirikiano na wataalamu wa magonjwa ya moyo kutoka nje ya nchi, najua taasisi ya hiari kutoka Uingereza imekusanya fedha na kwa kushirikiana na madaktari wengine, wamewezesha zoezi hili kufanyika kwa mafanikio.” Alisema Balozi Sutherland. 
Taasisi ya Muntada Aid, ni taasisi ya Kiislamu yenye makazi yake nchini Uingereza, ambayo ndiyo iliyowezwesha kuwaleta madaktari na vifaa, na hatimaye kwa kushirikiana na madaktari na wataalamu wengine kutoka JKCI wameweza kufanya upasuaji wa watoto 20 hadi sasa.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Profesa  Mohamed Janabi alisema, chini ya uratibu wa taasisi yake, wataalamu kutoka Australia kupitia Open Heart International, wakishirikiana na wataalamu kutoka JKCI waliendesha kambi ya upasuaji wa moyo kwa watoto 15 kuanzia Aprili 25 hadi Aprili 30.
“Kambi hii ya sasa, inaundwa na wataalamu kutoka Saudi Arabia chini ya uratibu wa taasisi ya hiari ya Muntada Aid, yenye makazi yake nchini Uingereza, na hadi leo hii Mei 3, 2016, tayari watoto 20 wameshafanyiwa upasuaji na hivyo kufanya jumla ya watoto 40 wamefanyiwa upasuaji tangu kambi hizi mbili zianze.” Alifafanua Profesa Janabi kwenye mkutano na waandishi wa habari. Alisema, malengo yao ni kuwafanyia upasuaji watoto 70 Ifikapo Mei 7. 

“Tunawashukuru wenzetu hawa kwa kuja kutshirikiana nasi kwani upasuaji unaofanyika ni huu wa kisasa, ambapo hakuna kumpasua kifua mgonjwa bali tunafanya upasuaji kwa kutumia matundu na hili ni jambo muhimu kwa wataalamu wetu ambao wamepata fursa ya kujifunza kutoka kwao.” Alisema.

Kaimu Muuguzi Mkuu wa taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, (JKCI), Flora Kasembe, (wa pili kulia), akitoa maelezo ya namna wanavyohudumia wagonjwa waliolazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi cha JKCI, wakati Naibu Balozi wa Uingereza hapa nchini, Bw. Matt Sutherland, (wa pili kushoto), alipotembelea kambi ya upasuaji wa moyo iliyoendeshwa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na taasisi ya hiari ya Uinegereza ya Muntada Aid, Mei 3, 2016. Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Profesa Mohammed Janabi, Meneja Mradi wa Muntada Aid, Kabir Miah, Mkuu wa Upasuaji wa JKCI, Dkt.Peter Kisenge, na Daktari Bingwa wa Moyo wa JKCI, Dkt.Tulizo Shem.Profesa Janabi (kushoto) na Balozi Sutherland baada ya kutembelea chumba cha Coronary care unit

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 03, 2016

    Hii taasisi ya matibabu ya moyo inafanya kazi nzuri hapa nchini ikiwa ni pamoja na kushirikiana na madaktari bingwa wa nchi zingine.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...