NA BASHIR NKOROMO.
KITUO cha Ufundi cha Kilimo na Maendeleo Vijijini (Technical Centre for Agricultural and Rural Cooperation, CTA) chenye makao makuu mjini Wageningen, Uholanzi kimemteua Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete kuwa Balozi wa Heshima (Goodwill Ambassador) wa Maendeleo ya Kilimo katika Mabara ya Afrika, Karibiani na Pasifiki.
Katika barua iliyokabidhiwa na mjumbe wa Bodi ya CTA, Prof. Faustin Kamuzora, CTA wameainisha kuwa Dk. Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, Taifa, ameteuliwa kwa kutambua mchango wa juhudi zake katika kukiendeleza kilimo nchini Tanzania na barani Afrika.
Katika wadhifa wake huo mpya, CTA imemuomba Dk. Kikwete aweze kuiwakilisha katika makongamano ya kimataifa ambapo atazungumzia umhimu wa kukiendeleza kilimo kwa ajili ya kutoa fursa ya ajira zenye staha kwa vijana na wanawake katika nchi za barani Afrika, Karibiani na Pasifiki. Pia ataisaidia CTA katika kuandaa makala na kufanya mahojiano na waandishi wa habari katika nchi mbalimbali.
Dk. Kikwete amekubali uteuzi huo na kuahidi kushirikiana na CTA katika kutekeleza mambo ambayo ameombwa kuisaidia na taasisi hiyo ambayo ni ushirikiano wa Umoja wa Ulaya na Kundi la nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki wenye makao makuu mjini Brussels, Ubelijiji.
Prof. Kamuzora ambaye pia ni Katibu Mkuu, Mawasiliano ni mjumbe wa Bodi ya CTA akiwakilisha nchi za ukanda wa Afrika Mashariki kwa miaka mitano tangu 2013 hadi 2018.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...