Na Athumani Shariff
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson
Lwenge ametaka watendaji wa Halmashauri nchini kuwashtaki watu wanaohujumu
miundombinu ya maji kama wahujumu uchumi.
Hayo aliyasema leo alipofanya ziara katika
kijiji cha Bumila kata ya Lupeta
Halmashauri ya Mpwapwa baada ya kupokea taarifa ya hali ya huduma ya
maji katika kijiji hicho.
“Naagiza Halmashauri muwatafute watu wote
waliohujumu miundombinu ya maji na washitakiwe kama wahujumu uchumi, hatuwezi
kuwaachia watu wanaosababisha wananchi wasio na hatia kukosa huduma muhimu ya
maji”
Miundombinu ya maji katika kijiji cha Bumila
imehujumiwa kwa mabomba zaidi ya 40 ya nchi 2 yenye urefu wa mita 6 kwa kila
kipande cha bomba kung’olewa na hatimaye maji kutokuwafikia wananchi.
Katika hali ya kulikabili tatizo la maji katika
kijiji hicho Mhandisi Lwenge ameiagiza Halmashauri ya Mpwapwa kuchimba kisima
katika kijiji cha Bumila haraka ili kuwaondolea adha wananchi wa kijiji hicho.
Katika hatua nyingine Waziri Lwenge amewataka
viongozi na watendaji wote nchini kushughulikia maswala ya maji badala ya
kuachiwa yeye Waziri wa Maji peke yake.
“Kila
mmoja wetu kwa nafasi yake ana jukumu la kufatilia maswala haya sio ya waziri
wa maji peke yake, Wilayani mkishindwa mpeleke Mkoani nao wakishindwa wataleta
Wizarani nasi tukishindwa tutapeleka kwa Magufuli kitu ambacho sitegemei”
Alisema Waziri Lwenge.
Akiwa Wilayani Chemba, Waziri Lwenge amekataza
tabia ya baadhi ya vijiji, kata na jamii za watu wanao wabagua jamii nyingine
katika miradi ya maji. Akiwa wilayani humo Lwenge aliagiza kuwa miradi yote ya
maji ni mali ya serikali hivyo jamii zote bila kujali mipaka ya kijiografia
kupata huduma hiyo.
“Maji yote ni mali ya serikali, hamna mtu wala
kikundi cha mtu chenye kumiliki maji, hivyo hairuhusiwi kwa mtu au kikundi cha
watu kujimilikisha maji na kubagua baadhi ya jamii ya watu wengine wasipate maj,
sisi sote ni watanzania”. Alisema Waziri Lwenge.
Ziara ya Waziri Lwenge ilianza katika
Halmashauri za Chemba na Kondoa na kuishia katika halmashauri ya Mpwapwa ikiwa
ni ahadi aliyoitoa bungeni kwa mbunge wa Chemba Juma Nkamia na Mpwapwa George
Lubeleje.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge akiongea na wakazi wa Itolwa Wilayani Chemba kabla ya kuhitimisha ziara yake katika wilaya hiyo.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Lwenge akikagua moja ya matanki ya maji katika mradi wa maji wa Ntomoko Wilayani Chemba
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Lwenge akimtwisha ndoo Rawiya Hassani mkazi wa Chiruku ndoo ya maji
Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge akifungua koki ya maji katika mradi wa maji wa Chiruku Wilayani Chemba. nyuma ni Mbunge wa Chemba Alhaji Juma Nkamia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...