Na Allan Ntana, Kaliua
MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amemwagiza Kamanda wa Polisi
Mkoani Tabora Hamis Seleman na Mkuu wa wilaya ya Kaliua Hadija Nyembo
kuhakikisha wanakomesha vitendo vya mauaji vinavyozidi kushamiri
wilayani humo.
Agizo hilo amelitoa jana katika kikao maalumu cha baraza la madiwani
wa halmashauri ya wilaya hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Milenia
mjini Kaliua.
Alisema vitendo vya mauaji kwa raia wasio na hatia katika mkoa huo
vimekuwa vikishamiri siku hadi siku vikichochewa na imani za
kishirikina, wivu wa mapenzi na ugomvi wa mali huku matukio mengi
yakiripotiwa kutoka katika wilaya hiyo.
Alibainisha kuwa takwimu zinaonesha mkoa huo ni miongoni mwa mikoa
yenye matukio mengi ya mauaji jambo ambalo hawezi kuliacha liendelee
pasipo kuchukua hatua za makusudi za kukomeshwa kwa vitendo hivyo.
‘Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC), OCD Kaliua na Mkuu wa wilaya
hakikisheni mtu yeyote atakayeua mwenzake akamatwe mara moja na
afikishwe katika vyombo vya sheria’, aliagiza.
Aidha aliwaagiza madiwani, watendaji wote wa vijiji na kata kwa
kushirikiana na Kamati nzima ya ulinzi na usalama ya wilaya kusimamia
ipasavyo agizo hilo ili kuhakikisha matukio ya namna hiyo yote
yanakomeshwa na wananchi wanaishi kwa amani.
‘Ndugu zangu hatuwezi kukubali watu wandelee kuuana kama kuku,
watendaji wa vijiji na kata toeni ushirikiano katika hili, leteni
taarifa za wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kwa diwani au ofisi ya
Mkuu wa wilaya ili kukomesha mauaji hayo,’ aliongeza.
Aidha RC aliwataka madiwani wa halmashari hiyo kuhamasisha wazazi wote
kupeleka watoto wao shule ili wapate elimu kwa kuwa msingi mzuri wa
maisha ni elimu huku akiwaagiza kuchukua hatua kwa wote watakaokaidi.
Agizo la Mwanri kukomesha mauaji katika wilaya hiyo liliungwa mkono na
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Haruna Kasele, Mbunge wa
jimbo la Ulyankulu John Kadutu, Mbunge wa jimbo la Kaliua Magdalena
Sakaya na Mkuu wa wilaya hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri (wa tatu toka kulia) akiwa
katika kikao cha baraza la madiwani wa halmshauri ya wilaya ya Kaliua
jana,anayeongea katika kipaza sauti ni Mwenyekiti wa halmashauri ya
wilaya Haruna Kasele. (Picha na Allan Ntana)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...