Wizara ya Afya Zanzibar na Uongozi wa Jimbo la Jiangsu la Jamuhuri ya Watu wa China leo zimetiliana saini Mkataba wa kuupitia upya ule uliomaliza muda wake wa kuimarisha Mpango wa ushirikiano kati ya Zanzibar na Jimbo hilo katika kuimarisha Sekta ya Afya Zanzibar.
Mkataba huo pia umehusisha mpango wa Jimbo hilo kuendelea kuisaidia Zanzibar katika kuipatiaVifaa vya Hospitali, Dawa pamoja na Madaktari Mabingwa wanaoendelea kutoa huduma za Afya katika Visiwa vya Unguja na Pemba.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Juma Malik Akil aliiwakilisha  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kusaini Mkataba huo wakati  Serikali ya Jimbo la Jiangsu ya China ikawakilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Jimbo hilo anayesimamia Kamisheni ya Afya na uzazi wa Mpango Bibi Wang Yonghong.
Hafla hiyo fupi ilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na kushuhudiwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikoministi cha China {CCP } katika Jimbo la Jiangsu Bwana Luo Zhijun na mwenyeji wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Akitoa shukrani zake kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema huduma zinazotolewa na Madaktari mabingwa wa China wanaotoka katika Jimbo la Jiangsu zimeleta faraja kwa wananchi waliowengi hapa Zanzibar.
BaloziSeif alisema Timu ya Madaktari wa China  wanaopangiwa kutoa huduma za afya Zanzibar kwa sasa wamekuwa familia na wananchi wa Zanzibar wanaowahudumia kwa takriban miaka 52 sasa.
Alisema Jamuhuri ya Watu wa China kupitia Jimbo hilo imetoa mchango mkubwa  katika kuwasaidia Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika sekta ya huduma ya Afya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia ujumbe huo wa Viongozi 17 kutoka Jimbo la Jiangsu Nchini Jamuhuri ya Watu wa China kwamba uhusiano wa kihistoria kati ya pande hizo mbili utaendelea kudumishwa kwa ustawi wa mataifa hayo mawili.
Balozi Seif  kupitia ujumbe huo unaoongozwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikoministi cha China {CCP } katika Jimbo la Jiangsu Bwana Luo Zhijun aliyaomba Makampuni na Taasisi za uwekezaji katika Majimbo mbali mbali nchini humo kuwekeza miradi yao hapa Zanzibar.
Alisema Zanzibar kwa sasa tayari imeshaimarisha miundombinu mbali mbali inayotoa fursa kwa wawekezaji kuanzisha miradi yao  hasa katika sekta za Kilimo, Uvuvi, Utalii na Mawasiliano.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Juma Malik Akil alisema Mkataba huo wa ushirikiano utatoa fursa kwa pande hizo mbili kufanya uhakiki kwa maeneo waliokuwa wakishirikiana.
Dr. Malik alisema zaidi ya Dola za Kimarekani Laki Mbili na Nusu zinatarajiwa kutumika katika mpango huo wa kuimarisha ushirikiano ikiwemo Timu za Madaktari wanaopangiwa kutoa huduma hapa Zanzibar.
Katika utiaji saini huo Uongozi wa Jimbo la Jiangsu pia utatoa msaada wa Tani 500 za Dawa na Vifaa vya Hospitali katika azma yake ya kuendelea kuiunga mkono  Zanzibar katika Sekta ya Afya. 
 Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Juma Malik Akil kutoka kulia na  Mkurugenzi Mkuu wa Jimbo la Jiangsu China  anayesimamia Kamisheni ya Afya na uzazi wa Mpango Bibi Wang Yonghong wakitia saini Mkataba wa mpango wa kuimarisha uhusiano kati ya China na Zanzibar Wanaowashuhudia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kulia na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikoministi cha China {CCP } katika Jimbo la Jiangsu Bwana Luo Zhijun. Ofisi ya Makamu WA Pili wa Rais wa Zanzibar Vuga Mjini Zanzibar. 
 Dr. Juma Malik Akil na Bibi Wang Yonghong wakibadilishana hati mara baada ya kutia saini Mkataba wa mpango wa Ushirikiano huku Katibu Mkuu wa Chama cha Kikoministi cha China {CCP } katika Jimbo la Jiangsu Bwana Luo Zhijun akishangiria tukio hilo.
  Balozi Seif na Bwana Luo Zhijun wakiwa katika picha ya pamoja na Bibi Wang Yonghong na Dr. Malik mara baada ya kusaini Mkataba wa mpango wa ushirikiano wa pande hizo mbili.

 Balozi Seif kati kati akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Jimbo la Jiangsu na baadhi ya Mawaziri na Watendaji wakuu wa Serikali mara baada ya hafla ya utiaji saini. Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Afya Mh. Mahmoud Thabit Kombo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mh. Issa Haji Ussi, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Moh’d Mahmoud na Mshauri wa Rais wa Zanzibar Mambo ya Uchumi Balozi Moh’d Ramia.
Balozi Seif Ali Iddi akiagana  na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikoministi cha China {CCP } katika Jimbo la Jiangsu Bwana Luo Zhijun baada ya kumaliza hafla ya utiaji saini ofisini kwake vuga Mjini Zanzibar.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...